KUTUMIA TASBIHI (Kuhesabia Shanga) KATIKA KUMDHUKURU ALLAAH INAFAA?


SWALI LA KWANZA:
Asalam alaykum,
Naomba kuliza suali hili. kuna mtu aliniambia kuwa kusoma uradi kwa kushika mtasbihi ni ktk uzushi, na mwengine ameniambia kuwa sio kweli kwani swahaba ABUU HURAYRA alikuwa akivuta uradi kwa utumia kokwa za tende, kwa hiyo hakuna tofauti na mtasbihi. Sasa hapa nilikuwa naomba jibu la sawa kutoka kwenu wenye elimu, inafaa au haifai? Na kweli huyu sahaba alifanya hivi?
                
SWALI LA PILI:
A allakum. ningependa  kuuliza  kuhusu  utumiaji  wa  tasbih  ni  bidaah  na vipi  tutawaeleza  wazazi kuhusu   kutotumia.  mimi mzee  wangu  amenipa  yake  nitumie  jee  niifanyeje.


JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

JIBU LA KWANZA:
Shukrani kwa swali lako kuhusu mas-ala haya. Ni wazi kwa kila Muislamu kuwa jambo lake lolote analolifanya lazima liafikiane na sheria ya Kiislamu; Qur-aan na Sunnah.
Hilo ni kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ametuhimiza sana kufuata mwenendo wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kama ilivyo bayana katika Suratul Hashri Aayah ya 7:
"Na anachokupeni Mtume basi pokeeni, na anachokukatazeni jiepusheni nacho" (59: 7).
Kwetu sisi kumfuata Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) inafaa tujue alilotenda au kusema. Pia kipenzi chetu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametuambia:
"Nawausia kumcha Allaah, na kusikiliza muambiwayo na kutii hata akiwa Kiongozi wenu ni mtumwa wa Kihabashi. Kwani hakika atakayeishi katika nyinyi ataona khitilafu nyingi, basi jilazimisheni na kufuata mwendo wangu na mwendo wa Makhalifa wangu waongofu, yashikilieni kwa magego yenu mambo yao. Na nawatahadharisha nyinyi na uzushi katika mambo" (Abu Daawuud na at-Tirmidhiy).
Hebu tumsikilize tena kipenzi chetu anatueleza nini kuhusu haya mambo yanayozuliwa katika Dini:
"Mwenye kuzua katika hili jambo letu lisilokuwamo humo litakataliwa" (al-Bukhaariy na Muslim).

Katika riwaya ya Muslim:
"Mwenye kufanya amali isiyokuwa na hukumu yetu, itakataliwa".
Suala ambalo tunafaa sisi kama Ummah bora, Waislamu kujiuliza ni kuwa: Je, Mtume alitumia tasbihi ili kuleta uradi au alitumia kifaa gani? Je, Makhalifa waongofu walifanya hivyo? Je, Maswahaba wengine nao walifuata mwendo huo?

Awali ya yote hebu tutazame mas-ala ya kutumia vijiwe au shanga, au kokwa za tende n.k. katika kuleta tasbihi na nyuradi.
Hadiyth ifuatayo ndio wanayoitumia wengi wa wanaotumia tasbiyh:
"Bora ya chenye kukumbusha ni Tasbiyh"   Hii ni Hadiyth dhaifu.
Vilevile tunaona dalili nyingi za kuonyesha kinyume na hivyo wanavyofanya hao wenye kutumia Tasbiyh. Tutazame Hadiyth zifuatazo:

Imepokewa kwa Sa'd bin Abi Waqqaas (Radhiya Allaahu 'anhu): Wakati mmoja Sa'ad, akiwa pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) walimzuru mwanamke ambaye mbele yake kulikuwa na vijiwe au kokwa za tende ambazo alikuwa akitumia kumsabihi Allaah. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: Nakuambia kitu ambacho kitakuwa sahali na bora zaidi kwako kuliko unavyofanya. Akasema: Msabihi (SubhaanaLlaah) mara nyingi kama vile Alivyoviumba mbinguni, mara nyingi kama Alivyoviumba ardhini.. Mkabiri idadi kama hiyo, pia Mhimidi idadi kama hiyo na Mhalili .." (Abu Daawuud).

Sasa huyu mwanamke alikuwa atumie mbinu gani ya kuweza kuhesabu nyuradi hizo baada ya kuambiwa na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa njia hiyo si bora kufanywa na Muislamu. Katika mwenendo wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) tunapata kuwa yeye alikuwa akitumia vidole vyake vya mkono wa kulia ili kuhesabu Tasbihi, Takbiri, Tahmidi na Tahlili alizokuwa akifanya. Hii imepokewa na mtu kwa Banu Sulaym: Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alizihesabu mkononi mwangu au mkononi mwake kwa kusema: Tasbiyh (SubhaanaLlaah) inajaza nusu ya mizani, Tahmiyd (AlhamduliLlaah) inajaza kamili. Takbiyr (Allaahu Akbar) inajaza baina ya mbingu na ardhi, Funga ni nusu ya subira na  twahara ni nusu ya Imani(at-Tirmidhiy).

Pia Yusayrah (Radhiya Allaahu 'anha) anasimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), aliwaamuru (wanawake wa Muhajirina) wawe ni wenye kushikilia sana katika kumdhukuru Allaah kwa kusema: Allaahu Akbar, SubhaanaLlaah, Laa ilaaha illa Llaah, na wasimsahau Allaah na rehma Yake. Wahesabu hizo kwa vidole vyao kwani vidole vitaulizwa na vitazungumza (Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, an-Nasaa'iy, Ibn Maajah na al-Haakim kwa Isnadi iliyo sahihi).
Naye 'Abdullaah bin 'Amr bin al-'Aasw (Radhiya Allaahu anhuma) anasimulia, "Nilimuona Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), akihesabu kumsabihi Allaah na vidole vya mkono wake wa kuume" (Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, an-Nasaa'iy na Ibn Maajah).
Na kutoka kwa Asswalt bin Bahraam amesema, Ibn Mas'uud alimpitia mwanamke mmoja aliyekuwa na Tasbiyh akimsabihi Allaah kwa Tasbiyh hiyo akaikata na akaitupa, kisha akampitia mwanamume aliyekuwa akimsabihi Allaah kwa vijiwe akampiga kwa mguu wake kisha akasema;
"Mumetangulia, mumefanya uzushi kwa dhulma, na mumewashinda Maswahaba wa Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa elimu"

[Sanad yake ni sahiyh mpaka kwa Asswalti, naye ni "thiqah" (mkweli mwenye kutegemewa) katika wanaowafuatia Taabi'iyn (wenye kufuatia Maswahaba).]
Hivyo, badala ya kutumia tasbihi tuwe ni wenye kutumia mkono kwani hajapatikana hata Swahaba mmoja aliyefanya hivyo. Ni salama kwetu zaidi kutumia vidole vyetu na ndio Sunnah ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye tumeamriwa kumfuata.
Tufahamu kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anatuambia: "Leo Nimekukamilishieni Dini yenu, na Kukutimizieni neema Yangu na Nimekupendeleeni Uislamu uwe Dini yenu" (5: 3).

Imaam Maalik aliielezea Aayah hii kwa kusema: "Lolote ambalo halikuwa Dini wakati wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) haliwezi kuwa Dini sasa". Hii ina maana Dini imekamilika hatuwezi kuikamilisha zaidi ya hapo wala sisi hatuna daraja ya kuja kumkosoa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa yeye alifanya khiyana hakufikisha mengine ambayo alikuwa afaa atufikishie hivyo sisi Waislamu wa sasa tumekuja tukakamilisha hayo.
Tujiepushe na vizushi vyote nasi tutasalimika kabisa.

JIBU LA PILI:
Shukrani kwa swali lako la pili. Ukitazama hapo juu kwa jibu la swali la kwanza utakuta kuwa utumiaji wa Tasbihi ni Bid'ah na inafaa kwetu sisi wafuasi wa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) tuache kuzitumia. Na badala yake tutumie vidole vyetu vya mikono ambavyo navyo tunapata baraka kwa kufanya hivyo.
Inafaa kwetu sisi tutumie hekima katika kuwaelimisha wazazi wetu kuhusu hilo na mengineyo kwani bila ya hivyo kutakuwa na fitna na mzozo mkubwa zaidi. Wapo wazee ambao wanaelewa wanapoambiwa na kurekebishwa kwa njia nzuri na wapo walio wakaidi. Ni vigumu kwa mtu ambaye huenda kwa miaka 50 anafanya jambo fulani kisha ukaja ukamuarifu na utegemee aache hayo mara moja na akufuate! Lakini pia wapo wenye uoni na kutaka haki, ambao hawatazami haki inatoka wapi au kwa nani; wao ni wenye kujisalimisha na kufuata mara moja. Allaah Aliyetukuka Anasema kuhusu kutumia hekima na busara na mawaidha mazuri:

"Waite waelekee kwenye Njia ya Mola wako kwa hikima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora" (16: 125).

Ikiwa mzazi wako ni mkaidi tumia upole na njia ya taratibu wala usikate uhusiano naye kabisa. Usimsahau katika Swalah na du'aa zako kwani kwa kufanya hivyo pia utakuwa unamsaidia kwa kiasi kikubwa. Wema ni kitu muhimu sana kuwafanyia wazazi kama alivyotuamuru Aliyetukuka:
"Na Mola wako Ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema. Mmoja wao akifikia uzee, naye yuko kwako, au wote wawili, basi usimwambie hata: Ah! Wala usiwakemee. Na sema nao kwa msemo wa hishima. Na uwainamishie bawa la unyenyekevu kwa kuwaonea huruma. Na useme: Mola wangu! Warehemu kama walivyonilea utotoni" (17: 23-24).

Ama tasbihi aliyokupa unaweza kuiweka ikiwa bado ana ukaidi na kutochukua hadiya kutoka kwake inaweza kuleta zogo zaidi na kukatika kwa mahusiano, lakini usiitumie. Ikiwa ameelewa kuwa haifai basi yeye mwenyewe ataitupa na wala hatakupatia wewe.
Njia nzuri ya kutumia vidole kama tulivyopata kutoka kwa Wanachuoni walioelewa masuala hayo ya kutumia vidole, wanasema ni kutumia matumbo ya vidole karibu na kucha kuhesabia na si ile mistari mitatu ya kila kidole kama ilivyozoeleka na wengi. Lakini atakayefanya kwa njia zote hizo maadam anatumia vidole vyake, basi katimiza Sunnah na ana ujira mkubwa kwa hilo.
Na Allaah Anajua zaidi

0 Comments