KUTUMIA VIDOLE VYA MIKONO YOTE MIWILI KULETA TASBIHI INAFAA?

SWALI:

Assalam aleikum warahmatullah. Amma baada ya maamkizi mema, namshukuru Allah kwa kutujaliya mtandao kama huu na Awapatie tawfiq wanao fanya kazi hii. Swala langu ni kuwa kuleta tasbih/ dhikr kwa mikono yote miwili ni sawa? Kunao dalili la kulisisitiza jambo kama hili? Jazakallahu kheir. Assalam aleikum.


JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuleta dhikr kwa mikono yote miwili. Hakika dhikr inatakiwa iletwe kwa njia ambayo ametufunza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi aalihi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi aalihi wa sallam) alikuwa akileta dhikr na akihesabu kwa kutumia mkono wa kuume peke yake:

'Abdullaah bin 'Amr bin al-'Aasw (Radhiya Allaahu anhuma) anasimulia, "Nilimuona Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), akihesabu kumsabihi Allaah na vidole vya mkono wake wa kuume" (Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, an-Nasaaiy na Ibn Maajah).

Kwa hiyo ili kufuata Sunnah inabidi nasi tutumie mkono huo.

Na utaratibu mzuri wa kutumia vidole kama tulivyopata kutoka kwa Wanachuoni walioelewa masuala hayo ya kutumia vidole, wanasema ni kutumia matumbo ya vidole karibu na kucha kuhesabia na si ile mistari mitatu ya kila kidole kama ilivyozoeleka na wengi. Lakini atakayefanyakwa njia zote hizo maadam anatumia vidole vyake, basi katimiza Sunnah na ana ujira mkubwa kwahilo.

Na haipendezi kutumia mkono wa kushoto kwa kuhesabia dhikr unazofanya.

Na mambo mema yote yanafanywa kwa kutumia mkono wa kuume. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi aalihi wa sallam) alikuwa akipenda kufanya mambo yake yote kwa mkono wa kulia. Anasema Mama wa Waumini 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha):
"Alikuwa akipenda Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuanza kuutumia mkono wa kulia wakati akivaa viatu vyake, na kujichana kwake, na katika kujitwaharisha kwake, na katika kutenda mambo yake yote." Al-Bukhaariy Na Muslim.Na Allaah Anajua zaidi

0 Comments