SWALAH YA WITR INASWALIWA VIPI NA VIPI KUTIA NIA?

SWALI:
nategamea muko katika hali ya afya njema na ramadhan karim  mimi nina suala langu kuhusu salaa ya witri .witri inasaliwa rakaa moja ,tatu ,tano,ambazo rakaa zisizogawika kwa mbili ama sivyo na wengine wanasema utakaposali rakaa tatu haifai kusali kama sala ya magharibi yaani usalii rakaa mbili ukae atahiyat ikisha umalize rakaa ya mwisho utoe salamu na wengine wanasema usali rakaa zote tatu moja kwa moja ya mwisho ndio utoe salamu yaani usikasali rakaa mbili ikisha ukae atahiyat  ikisha umalize rakaa moja kwa ufupi yaani usisali kama sala ya magharib kwa hiyo naomba jibu kutoka kwa wanalhidaaya
 na utakaposali unatia nia gani ya witri? nadhani nitapata jibu kutoka kwenu inshaalah a/a

JIBU:
Sifa zote njema anastahiki Allah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum)  na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Witr ni kuswali Rakaa moja, au tatu, au tano, au saba, au tisa au kumi na moja. Swalah hii huswaliwa usiku baada ya Swalah ya 'Ishaa ikiwa ni kabla ya kulala au baada ya kulala na kuamka kabla ya Alfajiri.
Mafunzo ya Sunnah yanatufundisha kuwa Rakaa zozote utakazojaaliwa kuswali, basi umalizie na Rakaa moja au tatu za Witr ambazo huswaliwa hivi:
Kuswali Rakaa mbili kwanza kisha utoe salaam. Kisha unamalizia na Rakaa moja na kutoa salaam.
Au kuswali Rakaa zote tatu kwa tashahhud (kikao) moja ya mwisho tu na kutoa salaam.
Haifai kuswali Rakaa tatu zote pamoja kwa kuleta Tashahhud mbili kama vile Swalah ya Magharibi, bali ni kuitofautisha na Swalah ya Magharibi kutokana na kauli ya Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
(( ولا تشبهوا بصلاة المغرب))
 ((… wala msiishabihishe (hiyo witr) na Swalah ya Magharibi)) [Al-Haakim, Al-Bayhaqiy, Ibn Hibbaan, Ad-Daraaqutniy?]  

Hii ni kuhusu Swalah ya Tahajjud ambayo ni sawa na Swalah ya Taarawiyh au kwa jina lingine niQiyaamul-Layl.

JIBU LA PILI KUHUSU NIA
Nia ya ibaada yoyote haitajwi kwa sauti, bali huwekwa moyoni. Na hayo ndio mafunzo sahihi  ya Sunnah. Kutaja nia kwa sauti ni Bid'ah. Unapojitayarisha kwenda kuswali Taarawiyh au Swalah yoyote nyingine kwa kufanya wudhuu, na kutoka kwenda msikitini, huwa tayari umeshatia nia moyoni kwa lile unaloliendea, hivyo inatosheleza kuwa nia yako imeingia moyoni.
Na Allah Anajua zaidi

0 Comments