VITA VYA BADR

Imekusanywa Na Muhammad Faraj Saalim As-Sa’iy

Badr ni jina la mji ulio kiasi cha kilomita mia na hamsini mbali na mji wa Madiynah, na mahali hapo hapakuwa na chochote isipokuwa bonde tu na kisima kilichokuwa milki ya mtu mmoja aitwae Badr, na kwa ajili hiyo mahala hapo pakaitwa ‘Badr’. Kwa vile vita hivyo vilipiganwa mahali hapo, ndiyo maana vikaitwa vita vya Badr.
Vita hivyo vilitokea asubuhi ya siku ya Ijumaa, Ramadhani ya kumi na saba mwaka wa pili baada ya Hijra (baada ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhamia Madiynah).
Sababu Za Vita
Chanzo cha vita hivi kilikuwa ni msafara wa biashara wa makafiri ukiongozwa na Abu Sufyan uliokuwa ukitoka nchi ya Sham ukirudi Makkah ukiwa na watu wasiozidi arobaini. Msafara huu ulikuwa umebeba mali nyingi sana ya watu wa Makkah, na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaona hii ni fursa nzuri ya kuipiga dola hiyo ya kikafiri kiuchumi, kijeshi na kisiasa, na pia kulipiza kisasi. Hasa kwa vile Waislam walipohama Makkah kwenda Madiynah, Makafiri waliwalazimisha kuziacha mali zao zote huko, na kuondoka bila chochote isipokuwa nguo zao na mnyama wa kumpanda. Bali wengine walinyang’anywa hata wanyama wao, na ikawabidi kutembea kwa miguu mpaka Madiynah na wengine waliviziwa njiani na kuuliwa.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia Waislam:
((Msafara huu wa Makuraysh umejaa mali zao, uendeeni, huenda Allaah akatulipa (haki zetu walizotunyang’anya) kwa kutuwezesha kuuteka.))
Nguvu Za Jeshi La Waislam
Si watu wengi waliojitolea kwenda, na hii ni kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakutilia mkazo sana kutoka huko. Hakumlazimisha mtu kwenda naye na wala hakumlaumu yeyote yule asiyetoka pamoja naye. Bali alimwacha kila mmoja ajiamulie mwenyewe ikiwa anataka kwenda au hataki. Na kwa ajili hiyo Maswahaabah wachache tu walimfuata.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaondoka akiwa na watu wapatao mia tatu na kidogo tu hivi. Inasemekana walikuwa mia tatu na kumi na tatu au kumi na nne na riwaya nyengine zinasema kuwa walikuwa mia tatu na kumi na saba. Themanini na sita kati yao ni Muhajiriyn (watu wa Makkah waliohamia Madiynah) na mia mbili thelathini na moja ni watu wa pale pale Madiynah.
Maswahaabah (Radhiya Allaahu ‘anhu) hawakujuwa kuwa msafara huu utakuja geuka kuwa ni moja katika mapambano makubwa baina ya Haki na Baatwil. Walidhania kuwa yatakuwa yale mapambano ya kawaida baina ya makundi ya wapiganaji wa Kiislam na misafara midogo midogo ya makafiri. Hawakujua kuwa Allaah amekwisha panga atimize jambo lililokuwa lazima litendeke.
Waliondoka wakiwa na farasi wawili tu, mmoja wa Zubair bin Awaam na mwengine wa Mikidaad bin Al-Aswad Al-Kindy (Radhiya Allaahu ‘anhu). Walikuwa pia na ngamia sabiini wakipokezana katika kuwapanda.
Jeshi La Waislam Linaondoka Kuelekea Badr
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaondoka Madiynah pamoja na Swahaabah zake hao (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuufuatia msafara huo wa Abu Sufyan. Akamchaguwa Ibni Ummi Makhtuum (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa ni mkuu wa Madiynah badala yake, lakini alipofika nje kidogo ya Madiynah, mahali panapoitwa Ar-Rawha, akamrudisha Swahaabah mmoja anayeitwa Aba Lubaba (Radhiya Allaahu ‘anhu), na kumtaka yeye awe khalifa wake pale Madiynah badala ya Ibni Ummi Makhtuum (Radhiya Allaahu ‘anhu).
Katika msafara huo, Mtume(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamchagua Mas-‘ab bin ‘Umair (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa ni mshika bendera, na bendera yenyewe ilikuwa ya rangi nyeupe.
Akaligawa jeshi makundi mawili:
1.     Kikosi cha Muhajiriyn (watu wa Makkah) na akampa bendera yao ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhu).
2.     Kikosi cha watu wa Madiynah, na akampa bendera yao Sa’ad bin Mu’aadh (Radhiya Allaahu ‘anhu).
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaondoka na jeshi lake hilo akiifuata njia ya Makkah, na alipofika mji uanoitwa Ar-Rawha akapumzika, na baada ya kupumzika mahala hapo akaondoka kuelekea mji wa Badr akiiacha njia ya Makkah kushotoni kwake na kuendelea na safari yake mpaka akalifikia bonde la Rahiyqan na baada ya kuendelea mbele kidogo, akawatuma Maswaahabah Basis bin ‘Umar na Uday bin Azzaghaabah (Radhiya Allaahu ‘anhu) watangulie na kupeleleza habari za msafara waliokusudia kuuteka.
Msafara Wa Abu Sufyan
Ama Abu Sufyan aliyekuwa kiongozi wa msafara wa biashara ya makafiri wa Makkah, alikuwa ni mtu mwenye kuchukua hadhari sana, alijuwa kuwa njia ya Makkah ina hatari nyingi, na kwa ajili hiyo, kila mara alikuwa akitanguliza wapelelezi ili wamletee habari za mbele ya safari, wakati huo huo alikuwa akimuuliza kila anayekutana naye, iwapo huko alikotoka ameona chochote kile kisichokuwa cha kawaida.
Katika kuuliza uliza kwake akamuuliza mtu mmoja anayeitwa Majdi bin ‘Amru iwapo ameona jeshi kutoka mji wa Madiynah, akasema:
“Mimi sikuona majeshi, lakini niliona kundi kubwa la watu waliopumzisha ngamia wao mahali hapa”.
Abu Sufyan akaenda kupafanyia uchunguzi mahali pale alipoambiwa kuwa watu walipumzisha ngamia wao. Baada ya kuchambua kinyesi cha ngamia waliopumzishwa mahali hapo na kuona kokwa za tende ndani yake, akasema:
“Madamu choo chao kimejaa kokwa za tende, hapana shaka yoyote kuwa hawa ni ngamia wa watu wa Madiynah”.
Alipotambua hayo, akajua kuwa anaviziwa, na hapo hapo akageuza njia yake na kumtuma mtu mmoja aitwae Dhamdham bin ‘Amru Al-Ghafaariy atangulie mbio sana. Aende kuwazindua watu wa Makkah juu ya hatari inayoukabili msafara wao wenye vitu vya thamani kubwa sana.
Watu wa Makkah waliposikia hayo, wakasema:
“Muhammad anadhania kuwa atauteka msafara huu kwa urahisi kama alivyouteka msafara wa ‘Amru bin Al-Hadhramiy?” (Kisa cha kutekwa kwa msafara wa ‘Amru nimekielezea katika makala ya ‘Miezi Mitukufu’).
Makafiri wakaendela kusema:
“Haitokuwa hivyo kabisa! WaLlaah atakiona chake Muhammad safari hii”.
Jeshi La MakafiriWa Makkah
Makuraysh mara baada ya kujuulishwa juu ya hatari hiyo, wakakusanya jeshi la watu wapatao alfu moja na mia tatu, farasi wapatao mia moja na ngamia wengi sana. Wakaondoka hapo wakiongozwa na Abu Jahal bin Hishaam pamoja na vigogo vya Makuraysh.
Walisafiri kwa kasi kubwa sana kuelekea kaskazini mahali uliopo mji wa Badr. Walipoufikia mji uitwao Al-Juhufa, wakapata salamu kutoka kwa Abu Sufyan kuwa; msafara wake umekwishasalimika na hatari ya kutekwa, na akawataka warudi Makkah.
Kwa sababu mara Abu Sufyan alipotambua kuwa anafuatwa, akabadilisha njia na kupita njia ya pwani pwani badala ya kupitia njia ya mji wa Badr. Na kwa ajili hiyo akaokoka na kuwapelekea habari hizo wenzake.
Abu Jahal akasema:
“Wallahi haturudi, mpaka tufike Badr, tukae hapo siku tatu, tuchinje wanyama wetu, tunywe pombe yetu na waimbaji waimbe mpaka habari zetu ziwafikie Waarabu wote ili wapate kutujuwa ni nani sisi na ili watuogope”.
Tatizo La Jeshi La Waislam
Waislam walipata habari za kuwaponyoka kwa msafara wa Abu Sufyan na wakati huo huo wakapata habari za jeshi kubwa la watu wa Makkah lililowakabili lililoazimia kwenda mji wa Badr, na kwa ajili hiyo wakaingia katika tatizo kubwa sana.
Baadhi yao wakaingiwa na hofu, na wengine wakatoa wazo la kurudi Madiynah, na hii ni kwa sababu walikuwa wachache, hawana silaha za kutosha na hawakutoka kivita. Lakini ikawabidi kulikabili tatizo hilo kwa ushujaa mkubwa kabisa kwani iwapo watakimbia kupambana na jeshi la makafiri na kuliacha litambe hapo Badr, mji ulio katika eneo la karibu na mji wa Madiynah, huko kutawapa nguvu na kichwa kikubwa makafiri na watapata moyo zaidi, jambo ambalo halitakuwa na mwisho mwema. Wakati huo huo haiba ya jeshi la Waislam itaondoka.
Mwanachuoni mkubwa Al-Mubaarak Fury anasema katika kitabu chake Ar-Rahiyqul Makhtuum:
“Jeshi la Waislam lingekuwa mfano wa mwili bila ya roho, na makafiri wangepata moyo wa kujaribu kuushambulia mji wao wa Madiynah bila ya hofu yoyote ile”.
Allaah Anasema:
{{(Atakunusuru) kama alivyokutoa Mola wako katika nyumba yako kwa haki, na kundi moja la walioamini halipendi (utoke).
Wakabishana nawe katika haki baada ya kubainika kwenda huko kama kwamba wanasukumwa katika mauti na huku wanaona.
Na Allaah alipo kuahidini kuwa moja katika makundi mawili ni lenu. Nanyi mkapenda lisilo na nguvu ndio liwe lenu; na Allaah anapenda ahakikishe Haki kwa maneno yake, na aikate mizizi ya makafiri.
Ili ahakikishe Haki na auvunje upotovu na wangechukia wakosefu.}}
[Suuratul-Anfaal: 5-8]
Mtume (Swalla Allaahu ‘AlayhiWaAalihiWa Sallam) Anashauriana Na Sahaba Zake (Radhiya Allaahu ‘Anhum)
Kutokana na mabadiliko haya ya ghafla na ya hatari, ilimbidi Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aitishe mkutano wa mashauriano na wakuu wa jeshi la Waislam ili kuwajuulisha juu ya hali ya mambo ilivyo na kutaka ushauri wao.
Ama wale aliowashauri katika wakubwa wa jeshi lake, kwanza aliinuka Abu Bakar (Radhiya Allaahu ‘anhu) akatoa hutoba nzuri ya kumuunga mkono Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) juu kulazimika kwao kupigana na makafiri.
Kisha akainuka ‘Umar bin Khatwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) na kutoa hotuba nzuri vile vile.
Kisha akainuka Al-Mikdaad bin ‘Amru (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema:
“Ewe Mtume wa Allaah, nenda kama atakavyokuonyesha Allaah, na sisi tuko nyuma yako. WaLlaah hatukuambii kama walivyomuambia wana wa Israili Mtume wao Muusa: {{Nenda wewe na Mola wako mkapigane vita sisi tutakaa hapa (tunangoja)}}. Bali tunakwambia: ‘Nenda wewe na Mola wako ukapigane na sisi pamoja nanyi tutapigana …”
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Vyema)) Kisha akamuombea du’ah.
Hawa watatu wote walikuwa katika Muhajiriyn ‘Watu wa Makkah’, ambao ni wachache katika jeshihilo, na Mtume(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akapenda kujua rai ya viongozi wa watu wa Madiynah waliokuwa wengi katika jeshi hilo, akasema: ((Nipeni shauri lenu enyi watu))
Akikusudia watu wa Madiynah. Sa’ad bin Mu’aadh (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa mmoja wa viongozi wa watu wa Madiynah akatambua hayo, akasema: “WaLlaah kama kwamba unatukusudia sisi ewe Mtume wa Allaah?”
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Ndiyo))
Sa’ad (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema:
“Sisi tumekuamini na kukusadiki, na tukashuhudia kuwa uliyokuja nayo ndiyo haki, na tukakupa ahadi zetu na neno letu kuwa tutakusikiliza na kukutii, kwa hivyo endelea tu kama unavyotaka kwani WaLlaah kama utatutaka tuivuke bahari hii, ukaivuka, basi tutaivuka pamoja nawe na hapana hata mmoja kati yetu atakayebaki nyuma, sisi hatuogopi kupambana na adui kesho, sisi ni watu wenye kusubiri katika vita na wakweli katika mapambano na InshaAllaah Allaah atakuonyesha ndani yetu yale yatakayokufurahisha macho yako, kwa hivyo tuongoze kwa baraka za Allaah”.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akafurahishwa sana na maneno ya Sa’ad (Radhiya Allaahu ‘anhu), akasema:
((Nendeni na nakupeni bishara njema, Allaah ameniahidi moja wapo ya makundi mawili. Wallahi kama kwamba ninaona wapi wataanguka kila mmoja kati ya maadui.))
Majeshi Ya Kiislam Yanafanya Upelelezi
Walipowasili mahali panapoitwa Addiya, karibu na Badr, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na Sahibu yake wa pangoni Abubakar As-Swiddiiq (Radhiya Allaahu ‘anhu), wakatoka na kuanza kufanya uchunguzi nje ya kambi yao, na katika kutembea kwao, wakakutana na mzee mmoja wa Kiarabu na kumuuliza juu ya habari za jeshi la Makuraysh na juu ya habari za jeshi la Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ili asiweze kutambua ni katika kundi gani wao.
Yule mtu akawaambia:
“Kabla sijakujibuni, nambieni kwanza nyinyi mnatokea wapi?”
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:
((Ukituambia na sisi tutakuambia…?))
Yule mtu akasema:
“Nimesikia kuwa jeshi la Muhammad na Sahibu zake lilitoka siku kadhaa wa kadhaa, ikiwa habari hizo ni sahihi, basi leo watakuwa washafika mahali kadhaa.”
Akapataja mahali lilipo jeshi la watu wa Madiynah.
“Na nimesikia kuwa Makuraysh wametoka siku kadhaa wa kadhaa, na ikiwa maneno niliyoambiwa ni kweli, basi leo watakuwa washafika mahali kadhaa wa kadhaa.”
Akapataja mahali lilipo jeshi la Makuraysh.
Baada ya kumaliza kusema, akawauliza:
“Nyinyi mnatokea wapi?”
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuambia:
((Sisi tunatokana na maji.))
Kisha akaondoka.
Yule mtu akawa anajiuliza:
“Hawa wanatoka katika maji ya Iraaq au maji gani?”
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakusema uongo, kwani viumbe vyote vinatokana na maji. Allaah anasema:
{{Na tukafanya kwa maji kila kitu kilicho hai.}} [Suuratul-Anbiyaa:30]
Waislam Wanapata Habari Muhimu Kuhusu Jeshi La Makuraysh
Mchana wake siku hiyo, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwatuma watu watatu kwenda kupeleleza juu ya habari za jeshi la Makuraysh, nao ni: ‘Aliy bin Abi TwaalibAz-Zubayr bin ‘Awaam na Sa’ad bin Abi Waqaas (Radhiya Allaahu ‘anhu). Walipokwenda penye kisima cha Badr wakawakuta watoto watatu wanachota maji kwa ajili ya kuwapelekea jeshi la Makuraysh, wakawateka na kwenda nao kambini ili kuwauliza masuali.
Walipofika nao kambini Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali, kwa hivyo wao wakaanza kuwauliza mateka wao.
Vijana hao wakasema kuwa wametumwa na Makuraysh ili kuwachotea maji. Maswaahabah walikasirishwa na jibu hilo, kwani walitamani wawe watu wa msafara wa Abu Sufyan. Wakawapigasana mpaka wakasema kuwa wao ni watu wa Abu Sufyan na si watu wa jeshi la Makuraysh. Baada ya kutamka hayo, wakawaachilia.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumaliza kusali akawaambia;
{{Waliposema kweli mliwapiga, na walipokudanganyeni mkawachilia. Walisema kweli WaLlaahi, kwani wao ni watu wa jeshi la Makuraysh.))
Kisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawuliza wale vijana:
((Nipeni habari za Makureshi.))
Wakasema:
“Wapo katika ng’ambo ya bonde lile la mbali”.
Akawauliza:
((Wako wangapi?))
Wakasema:
“Wengi”
Akawauliza:
((Idadi yao ngapi?))
Wakasema:
“Hatujuwi”
Akawauliza:
((Wanachinja wanyama wangapi kila siku?))
Wakasema:
“Siku nyingine wanachinja ngamia tisa na siku nyingine kumi”.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema kuwaambia Maswahaabah (Radhiya Allaahu ‘anhum):
((Idadi yao ni baina ya watu mia tisa na elfu.))
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawauliza tena wale vijana:
((Nani katika vigogo vya Makuraysh wamo miongoni mwao?))
Wakasema:
“’Utbah na Shaiba watoto wa Rabia, Abu Al-Bakhtari bin Hishaam, Hakiym bin Hizaam, Naufil bin Khuwailid, Al-Haarith, Taimah, An-Nadhar bin Haarith, Zaamah bin Aswad, Abu Jahal bin Hishaam, na Umayyah bin Khalaf”.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema kuwaambia Swahaabah zake (Radhiya Allaahu ‘anhum):
((Makkah imekutupieni (imekuleteeni) vipande vya maini yao [vigogo vyao na vipenzi vyao].))
Kuteremka Kwa Mvua
Waislam wakasogea mbele kidogo mpaka wakakaribia bonde la karibu na mahali yalipopiga kambi majeshi ya Makuraysh.
Allaah aliwateremshia Waislam utulivu wakalala vizuri, hata wengine wakaota na kuamka wakiwa na janaba. Lakini mahali hapo hapakuwa na maji ya kuogea ili wapate kujitahirisha na wala ya kunywa, na Shaytwaan akaanza kuwatia wasi wasi:
“Vipi mtapigana kesho wakati miili yenu haina tohara, vipi mtapigana kesho mkiwa na kiu…?”
Allaah akawateremshia mvua iliyowasaidia sana. Kwa sababu kutokana na mvua hiyo waliweza:
·         Kujitahirisha,
·         Kuondoa uchafu wa shetani, na
·         Kuzipa nguvu nyoyo zao.
Na maji ya mvua pia yakawasaidia kuufanya mchanga chini yao uwe mgumu ili waweze kutembea vizuri bila ya kuteleza wakati wa mapambano.
Allaah Anasema:
{{Alipo kufunikeni kwa usingizi uwe ni uaminisho kutoka kwake, na akakuteremshieni maji kutoka mbinguni ili kukusafisheni kwayo na kukuondoleeni uchafu wa Shaytwaan, na kuzipa nguvu nyoyo zenu, na kuitia imara miguu yenu.}} [Suuratul-Anfaal: 11]
Jeshi La Waislam Linatangulia Kukamata Sehemu Muhimu
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaliamrisha jeshi lakeliondoke pale walipo haraka sana ili wawahi kusogea mbele karibu na mahali yalipo maji ya mji wa Badr. Wakasogea mpaka wakafika mwanzo wa visima vya maji ya Badr na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawaamrisha kupiga kambi hapo.
Mmoja katika Maswaahabah aitwaye Al-Khabaab bin Mundhir (Radhiya Allaahu ‘anhu), akamuuliza Mtume(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
“Ewe Mtume wa Allaah, mahala hapa tuliposimama, Allaah amekuamrisha na hatuna haki ya kusonga mbele zaidi au ni katika hila za kivita tu na rai yako mwenyewe?”
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:
((Bali ni hila za kivita na rai yangu mwenyewe.))
Akasema:
“Ewe Mtume wa Allaah, mimi naona kuwa hapa si makaazi mazuri, bora tusogee mbele mpaka mwisho wa visima vya maji ya Badr, tuvizunguke kisha tujenge mahodhi, tuyajaze maji, kisha tupambane nao, sisi tutakuwa tunakunywa na wao wasipate kunywa”.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:
((Rai uliyotowa ni nzuri.))
Wakaondoka hapo na kusogea sehemu ya juu ya mahali yalipo maji, na usiku wakaanza kutengeneza mahodhi na kuyajaza maji.
Makao Makuu Ya Jeshi
Baada ya kumaliza kazi yao hiyo, Sa’ad bin Mu’aadh (Radhiya Allaahu ‘anhu) akatoa rai pajengwe mahali patakapokuwa makao makuu ya jeshi lao, ili waweze kujitayarisha na kuikabili hali ya hatari yoyote itakayotokea iwapo jeshi lao litashindwa katika vita hivyo.
Akasema:
“Ewe Mtume wa Allaah, unaonaje tukakujengea kipaa mfano wa hema (‘Ariish), kisha tukakuwekea tayari wanyama wa kupanda, kisha sisi tutapambana na adui, ikiwa Allaah atatujaalia tukawashinda, hayo ndiyo tunayoyapenda. Ama ikiwa kinyume na hivyo, basi wewe utapanda wanyama wako na utakwenda kujiunga na wenzetu tuliowaacha nyuma, kwani hao tuliowaacha nyuma mapenzi yao juu yako ni makubwa pia  kama sisi. Wangelijuwa kuwa utapambana na adui, basi wasingerudi nyuma kabisa na wangepigana jihadi pamoja nawe.”
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuombea kila la khayr kwa rai yake hiyo, na Waislamu wakajenga mfano wa hema juu ya kilima, sehemu ya Kaskazini ya uwanja wa mapambano, sehemu ambayo mtu anaweza kuviona vita bila ya taabu huku vikipiganwa.
Usiku Kabla Ya Mapambano
Usiku kabla ya mapambano, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alilipanga vizuri jeshi lake. Kisha akawa anatembea huku akiwaonyesha Swahaabah (Radhiya Allaahu ‘anhum), mahali watakapokufa maadui mbali mbali, kabla hata vita havijaanza. Alikuwa akisema:
((Hapa ataanguka fulani, hapa atauliwa fulani …))
Alipokuwa akiwapanga watu wake, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipita mbele ya Sawad bin Aziya (Radhiya Allaahu ‘anhu) akamgonga kwa nguvu tumboni pake kwa bapa la mkuki na kumwambia:
((Simama vizuri ewe Sawaad.))
Sawad (Radhiya Allaahu ‘anhu) akamwambia:
“Umeniumiza ewe Mtume wa Allaah na Mola wako amekuleta kwa ajili ya kusimamisha haki na uadilifu, kwa hivyo uniache na mimi nikulipizie katika mwili wako”.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akalifunua tumbo lakena kumwambia:
((Jilipie kisasi chako.))
Sawad akalikumbatia tumbo la Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) huku akilibusu.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:
((Kipi kilichokupeleka ukafanya hivi?))
Akasema:
“Ewe Mtume wa Allaah, mambo ndiyo kama unavyoyaona na mimi nilipenda tendo langu la mwisho kabla sijafa liwe kuugusa mwili wako”.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuombea du’ah nzuri.
Baada ya kuwapanga watu wake sawa na kuwataka wasianze kupigana mpaka atowe amri yake, akawaambia:
((Wakianza kuja, anzeni kuwarushia mishale na msitoe panga zenu mpaka wawe karibu nanyi kabisa.))
Jeshi La WatuWa Makkah
Usiku ule baadhi ya Makuraysh walijaribu kutaka kunywa maji penye mahodhi waliyoyajenga Waislam, lakini kila aliyejaribu kuyasogelea aliuliwa, isipokuwa mtu mmoja aitwae, Haakim bin Hizaam, huyu aliachwa na alisilimu baadaye na akawa Mwislam mwema.
Makuraysh walimtuma ‘Umair bin Wahaab Al-Jahamiy aende kuchunguza nguvu za jeshi la Waislam. Akawa anazunguka mbali na jeshi hilo akiwa juu ya farasi wake, huku na kule, kisha akarudi kwa wenzake na kuwaambia:
“Jeshi lao ni kiasi cha watu mia tatu na zaidi kidogo, lakini naona kesho balaa litakuwa kubwasana, maana watu hawa hawana pa kukimbilia, na hawana cha kupoteza, wanajuwa kuwa wao watauliwa tu. Hawana isipokuwa panga zao tu, na nyuma yao jangwa tupu, kwa hivyo inaelekea watapigana kwa ushujaa na hawatokubali mmoja wao auliwe bila ya yeye naye kuuwa mtu mmoja kati yenu, kwa hivyo tizameni wenyewe”.
Pakatokea mzozo mkubwa baina ya Makuraysh, wengi wao wakamtaka Abu Jahal arudi na jeshilakeMakkah, na kwamba hapakuwa na haja ya kupigana na jeshi la Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Lakini Abu Jahal kwa haraka akafanikiwa kuuzima moto huo na kumlaumu ‘Umair kwa kumwambia:
“Umeingiwa na hofu wewe ulipouona uso wa Muhammad, pale ulipokuwa ukiyachunguza majeshi yake ndiyo sababu ukaja na uwoga na unataka kututia na sisi uwoga huo.”
Akaweza kuwaingiza watu wake mori wa vita, kwa kuwakumbusha kuuliwa kwa ‘Amru bin Al-Hadhramiy na kwamba lazima walipe kisasi chake.
Majeshi Yanakabiliana
Asubuhi ya siku ya Ijumaa, tarehe kumi na saba, mwezi wa Ramadhaan, mwaka wa pili baada ya Hijrah, majeshi hayo mawili yakapambana. Allaah aliwafanya Waislam walione jeshi la makafiri kuwa ni wachache ili wasiwaogope na akawafanya makafiri wawaone Wasilam pia kuwa ni wachache ili wasiwaogope na kurudi nyuma, yote haya ili kitendeke kile anachokitaka Subhaanahu wa Taala.
Allaah anasema:
{{Na mlipo kutana akakuonyesheni machoni mwenu kuwa wao ni wachache, na akakufanyeni nyinyi ni wachache machoni mwao, ili Allaah atimize jambo lilio kuwa liwe. Na mambo yote hurejezwa kwa Allaah. Enyi mlio amini! Mkikutana na jeshi, basi kueni imara, na mkumbukeni Mwenyezi Mungu sana ili mpate kufanikiwa.}} [Suuratul-Anfaal: 44-45]
Majeshi yalipoanza kupambana, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaingia ndani ya lile hema, yeye na Abu Bakar (Radhiya Allaahu ‘anhu) peke yao, na hapana mwengine aliyeingia humo gheri yao, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaanza kuomba du’ah huku akisema:
((Mola wangu hawa Makureshi wamekuja kwa jeuri na kiburi chao, wakikupinga na kumkadhibisha Mtume wako. Mola wangu nitimizie yale uliyoniahidi, Mola wangu watu hawa wakishindwa leo, basi hutaabudiwa tena…))
Kila vita vikipamba moto, naye huongeza kuomba du’ah.
Akawa anaendelea kuomba mpaka nguo yake ya begani ikamwanguka, na As-Swiddiik (Radhiya Allaahu ‘anhu) akaiokota na kumvisha tena huku akimwambia:
((Inatosha ewe Mtume wa Allaah, ushamuomba vya kutosha Mola wako.))
Kisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasimama penye mlango wa ‘Ariish aliyojengewa akawa anaisoma aayah ya 45 ya Suuratul-Qamar:
“Sayuhzamu l jam-‘u wa yuwalluwna ddubur”
Na maana yake ni:
{{Wingi wao huo karibuni watashindwa na wataendeshwa mbio na watageuza migongo.}}
Mubaraza (Mapigano) Kabla Ya Mapambano
Kwa kawaida kabla ya kuanza mapambano, Waarabu walikuwa na tabia ya kuanzisha Mubaraza, na maana yake ni, mtu mmoja au wawili au watatu hutoka kutoka kila upande na kuanza kupambana wao kwanza kila mmoja na mwenzake mpaka wauwane, kisha vita ndiyo vinaanza. Mapigano haya kwa kawaida ndiyo yanayotowa picha ndogo ya mwisho wa vita.
Katika mapigano haya, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwatoa upande wa Waislam, ‘Aliy bin Abi Twaalib, Ubaidah bin Haarith na Hamzah (Radhiya Allaahu ‘anhum). Kwa upande wa makafiri wakatoka, Utbah na ndugu yake Shaibah, na Al-Waliid mtoto wa Utbah – wote wakiwa watu wa aila moja. Katika mapigano hayo, Hamza (Radhiya Allaahu ‘anhu), alimuuwa mpinzani wake Shaibah, na ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu), alimuuwa mpinzani wake Al-Waliid bila taabu na bila kuchukuwa muda mferu. Ama Ubaidah (Radhiya Allaahu ‘anhu), yeye na mpinzani wake, wote wawili waliumizana wakaanguka chini, lakini ‘Aliy na Hamzah (Radhiya Allaahu ‘anhu) wakawahi kumrukia Al-Waliid na kumuuwa kisha wakamuokoa mwenzao na kumvuta nyuma na kumrudisha katika kambi ya Waislam. Lakini hatimaye kutokana na damu nyingi iliyomwagika alifariki dunia siku nne baada ya tukio la Badr kwa homa ya manjano.
Mashambulio
Mapigano haya yalimaanisha mwisho mbaya wa jeshi la washirikina. Kwa sababu wamepoteza watatu katika wapiganaji wao wakubwa kwa mpigo mmoja, na kwa kawaida Waarabu walikuwa na itikadi ya kuvipima vita kutokana na mapigano ya mwanzo (Mubaraza). Kwa ajili hiyo wakawavamia Wasilam kwa ghadhabu na kwa nguvu zao zote, na Waislam wakapambana nao kwa ujasiri mkubwa kabisa.
Wakati huo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawatokea Waislam na kuwaambia:
((Naapa kwa yule ambaye nafsi ya Muhammad ipo mikononi pake, yeyote atakayepigana nao leo kisha akauliwa akiwa katika hali ya subra, bila ya kurudi nyuma, basi Allaah atamuingiza Peponi.))
‘Umair bin Al-Hamaam (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa akila tende, mara baada ya kusikia maneno hayo akasema:
“Hivyo baina yangu na baina ya kuingia Peponi ni kupigana na kuuliwa na watu hawa na tende hii ndiyo inanichelewesha?”.
Akazitupa tende zake, akaingia vitani, akapigana mpaka akauliwa.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasogea mbele, akachota gao la mchanga, akawakabili Makuraysh, kisha akasema:
((Zimeangamia nyuso zao.))
Kisha akawarushia nao.
Allaah Anasema:
{{Hamkuwauwa nyinyi lakini Allaah ndiye aliye wauwa. Na wewe hukutupa, pale ulipotupa, walakini Allaah ndiye aliye tupa, ili awajaribu Waumini majaribio mema yatokayo kwake. Hakika Allaah ndiye Msikizi na Mjuzi. Ndio hivyo! Na hakika Allaah ni Mwenye kudhoofisha vitimbi vya makafiri.}} [Suuratul-Anfaal: 17 18]
Kisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia Swahaabah zake (Radhiya Allaahu ‘anhum):
((Wakazieni vizuri, inukeni muifuatilie Pepo ambayo upana wake tu ni sawa na mbingu na ardhi.))
Kisha akaondoka na kurudi penye ‘Ariish yake ile aliyojengewa.
Mapambano makali yakaanza baina ya makundi mawili hayo, na ushindi ukawa wa Waislam. Wakauliwa waliouliwa katika vigogo vya Makuraysh na wakatekwa waliotekwa.
Haya ni mapambano ya pekee ambayo Malaika walishiriki, akiwemo Jibriyl ('Alayhis Salaam). Baadhi ya Maswaahabah walisema:
“Siku hiyo tulikuwa tukiona vichwa vikikatika tu na kuruka huku na kule, hatujuwi nani anayevikata”.

{{Mlipo kuwa mkimuomba msaada Mola wenu Mlezi, naye akakujibuni kuwa: Kwa yakini Mimi nitakusaidieni kwa Malaika alfu wanao fuatana mfululizo.
Na Allaah hakufanya haya ila kuwa ni bishara na ili nyoyo zenu zituwe. Na haupatikani ushindi ila kutoka kwa Allaah. Hakika Allaah ni Mwenye nguvu, na Mwenye hikima.
Alipo kufunikeni kwa usingizi uwe ni uaminisho kutoka kwake, na akakuteremshieni maji kutoka mbinguni ili kukusafisheni kwayo na kukuondoleeni uchafu wa Shaytwaan, na kuzipa nguvu nyoyo zenu, na kuitia imara miguu yenu.
Mola wako Mlezi alipo wafunulia Malaika: Hakika Mimi ni pamoja nanyi, basi watieni nguvu walio amini. Nitatia woga katika nyoyo za walio kufuru. Basi wapigeni juu ya shingo na wapigeni kwenye kila ncha za vidole.
Hayo ni kwa sababu wamemuasi Allaah na Mtume wake. Na mwenye kumuasi Allaah na Mtume wake basi Allaah ni Mkali wa kuadhibu.
Ndio hivyo! Basi ionjeni! Na bila ya shaka makafiri wana adhabu ya Moto.}}
[Suuratul-Al Anfaal: 9–14]
Kifo Cha Abu Jahal
Abu Jahal alipoona majeshi yake yanaanza kurudi nyuma akawa anapiga kelele huku akisema:
“Wasikutisheni hao, msiogope kwa kuwa ‘Utbah na Al-Waliid wameuliwa, leo hatuondoki hapa mpaka turudi nao Makkah tukiwa tumewafunga kamba wote hawa”.
Anasema ‘Abdur-Rahmaan bin Auf kuwa nilipokuwa nimesimama vitani nikageuka kutizama kuliani kwangi na kushotoni kwangu nikidhania watakuwepo watu wazima ili tusaidiane vita vikipamba moto. Lakini nikavunjika moyo nilipowaona watoto wadogo wawili wamesimama mmoja kushotoni pangu na mwengine kuliani pangu. Nikasema moyoni mwangu: “Leo sina pa kuegemea”. Yule mtoto aliye kuliani pangu akaniomba niiname apate kuniuliza ili yule mwenzake asisikie. Akaniuliza:
“Ami! Yupi kati yao Abu Jahal?”
Nikamuuliza:
“Ewe mwana wa ndugu yangu, unamtakia nini Abu Jahal?”
Akanijibu:
“Nimesikia kuwa anamtukana Mtume wa Allaah, WaLlaahi nikimuona basi sitomwacha, lazima nitamuuwa”
Yule mtoto aliye kushotoni pangu akaniuliza vile vile kama mwenzake, na nikamjibu kamamwenzake na akasema yale yale aliyosema mwenzake.
Nilipomuona Abu Jahal nikawaambia:
“Yule rafiki yenu mnayemtafuta”
Wakamkimbilia na panga zao, wakamvamia na kumpiga kwa mapanga mpaka wakamuuwa.
Mara baada ya kumuuwa wakakimbia mpaka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumpa habari njema hizo. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawauliza:
((Yupi kati yenu aliyemuuwa?))
Kila mmoja akasema:
“Mimi ndiye niliyemuuwa”.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia:
((Hebu nione panga zenu.))
Baada ya kuzitizama akasema:
((Kweli, nyote mmeshirikiana katika kumuuwa.))
Kisha akasema:
“Allaahu laa ilaaha illa huwa” mara tatu.
Kisha akasema:
“Alhamdu lillaahi lladhiy swadaka wa’adahu, wa naswara ‘abdahu, wa hazama l-ahazaaba wah–dahu”.
Katika vita hivi waliuliwa Makuraysh sabiini, na wengine sabiini walitekwa, na katika waliouliwa alikuwemo Firauni wa Umma huu – Abu Jahal na ‘Utbah bin Rabia na mwanawe Al-Waliyd na nduguye Shaiba na wengi wengineo.
Na miongoni mwa mateka alikuwemo Al-‘Abbaas – Ami yake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na ‘Aqiyl bin Abi Twaalib, na Nawfal bin Al-Haarith, na Umayya bin Khalaf na wengi wengineo.
Hawa wote walikuwa upande wa Makuraysh.
Mizoga Ya Makafiri
Baada ya vita kumalizika, Waislam wakawazika wenzao waliokufa Mashahid na idadi yao walikuwa kumi na nne. Kisha wakaichukua mizoga ya Mushrikina na kuitupa katika kisima kisichokuwa na maji kilicho karibu na mahali palipotokea mapambano hayo.
Mtume (Swalla Allaahu ‘AlayhiWaAalihiWa Sallam) Anawafokea Maadui Wake
Usiku wa manane Waislam walimsikia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa amesimama penye kile kisima walichotupa mizoga ya Mushrikina akiwafokea huku akisema:
((Enyi mlio kisimani, ubaya ulioje mliokuwa nao jamaa zangu nyinyi kwa Mtume wenu! Mlinikadhibisha wakanisadiki watu (kweli), mkanitoa katika mji wangu, wakanipokea watu (kweli), mkanipiga vita wakanisaidia watu (kweli). Je! Sasa nyinyi mmekwisha pata kweli yale aliyokuahidini Mola wenu? Ama mimi nimepata kweli yale aliyoniahidi Mola wangu.))
Maswahaabah wakamuuliza:
“Ewe Mtume wa Mwenyei Mungu unazungumza na watu washakuwa mizoga?”
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:
((Wao wanasikia kuliko nyinyi haya niliyowaambia isipokuwa hawawezi kujibu.))
Bishara Njema
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwatuma watu kwa haraka sana waende Madiynah ili kuwapa habari njema hizo za ushindi wao juu ya Makafiri.
Usaamah bin Zayd (Radhiya Allaahu ‘anhu) anasema:
“Zilitufikia habari tulipokuwa tukimzika Bibi Ruqayya (Radhiya Allaahu ‘anha) binti wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), mke wa ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhiya Allaahu ‘anhu).
Zayd bin Harithah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipoingia msikitini, watu walimzunguka huku akisema kwa furaha:
“Amekwisha uliwa ‘Utbah bin Rabia na Shaibah bin Rabia na Abu Jahal.” Akawa anawataja mmoja mmoja katika vigogo vya Makuraysh waliouliwa Badr.
Zayd (Radhiya Allaahu ‘anhu) anasema:
“Nikamuuliza, Babangu unasema kweli?”
Akanijibu:
“Naam, kweli mwanangu”
Kuondoka Mji Wa Badr
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), akaondoka hapo Badr pamoja na mateka wao na ngawira zao na alipofika karibu na Madiynah alisimamisha msafara katika bonde la Safra akawagawia Waislam ngawira yao sawa sawa na kila anapoukaribia mji wa Madiynah, alikuta makundi kwa makundi ya watu waliosimama pembezoni mwa njia wakimpongeza.
Allaah anasema:
{{Kumbukeni pale mlipo kuwa nyinyi kwenye ng'ambo ya karibu ya bonde, na wao wakawa ng'ambo ya mbali, na msafara ulipo kuwa chini yenu. Na ingeli kuwa mmeagana mngeli khitalifiana katika miadi. Lakini (mkakutana) ili Allaah atimize jambo lilio kuwa lazima litendeke, kwa sababu aangamie wa kuangamia kwa dalili zilizo dhaahiri, na asalimike wa kusalimika kwa dalili zilizo dhaahiri. Na Allaah ni Mwenye kusikia Mwenye kujua.
Kumbuka alipo kuonyesha usingizini mwako kwamba wao ni wachache - na lau angeli kuonyesha kuwa ni wengi, mngeli ingiwa na woga, na mngeli zozana katika jambo hilo.
Lakini Allaah kakuvueni. Hakika Yeye ni Mwenye kuyajua yalio vifuani.}}
[Suuratul-Anfaal: 42–43]
Matukio Mbali Mbali
Baada ya kumalizika vita, Masa-‘ab bin ‘Umair (Radhiya Allaahu ‘anhu) alimuona ndugu yake Abu ‘Aziiz aliyekuwa upande wa makafiri akiwa ametekwa na amefungwa kamba. Akamwambia yule aliyemfunga kamba:
“Mfunge vizuri huyo kwa sababu mamake ana mali nyingi, anaweza kumkomboa”
Ndugu yake akamwambia:
“Huko ndiko kuwapa usia mwema ndugu yangu?”
Mas-‘ab akamwambia:
“Huyu aliyekukamata ni ndugu yangu kuliko wewe”.
Baada ya kutupwa maiti za makafiri kisimani, Abu Hudhaifah (Radhiya Allaahu ‘anhu) mwana wa ‘Utbah bin Rabia alikuwa na huzuni sana. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza:
((Unaona vibaya juu ya babako, (kwa vile ni kafiri na ametupwa kisimani na wenzake)?))
Abu Hudhaifah akasema:
“Laa wallahi, ewe Mtume wa Allaah, isipokuwa babangu alinifanyia fadhila nyingi sana na alikuwa akinipenda, nikadhani kwa ajili hiyo naye atasilimu, na nilipomuona kuwa amekufa kafiri, ndio nikahuzunika”.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuombea du’ah kumtakia kila la khayr.
Wale watoto wawili waliomuuwa Abu Jahal nao wana kisa chao. Walipokuja kutaka kushiriki katika vita, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamkubali ndugu mkubwa na akamkataa yule mdogo.
Yule mdogo akasema:
“Ewe Mtume wa Allaah, kwa nini umemkubali kaka yangu na mimi hukunikubali?”
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:
((Kwa sababu umri wako ni mdogo.))
Akasema:
“Lakini sisi siku zote tukipigana mieleka, mimi namshinda kaka yangu.”
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:
((Hebu piganeni mieleka nikuoneni.))
Wakapigana na yule mdogo akamshinda mkubwa wake, kisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamkubali.
‘Umar bin Khatwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) alimuuwa siku hiyo mjomba wake Al’Aas bin Hisham, aliyekuwa upande wa makafiri.
Hitimisho
Allaah anasema:
{{Na Allaah alikunusuruni katika (vita vya) Badr. Hali nyinyi mlikuwa dhaifu. Basi mcheni Allaah ili ili mpate kushukuru (kila wakati kwa neema zinazokujieni).}} [Suuratul-‘Imraan: 123]
Allaah, hapa anatujuulisha kuwa Yeye tu ndiye wa kutegemewa, na si viumbe vyake dhaifu. Yeye tu ndiye mwenye kuleta ushindi, na anayestahiki kukimbiliwa wakati wa dhiki, badala ya kuwakimbilia viumbe vyake dhaifu.
Na hili ni somo kwa wale ndugu zetu ambao mara wanapokumbwa na tatizo dogo, wanaikimbilia ile du’ah ya Hal Badiri (Ahlul-Badr) ambayo ndani yake mna majina ya Maswahaabah walioshiriki katika vita hivyo, na kuomba msaada kutoka kwao.
Allaah anasema:
{{Na Allaah alikunusuruni katika (vita vya) Badr. Hali nyinyi mlikuwa dhaifu.}}
Allaah aliwapa ushindi Waislam katika vita hivi juu ya uchache wao, wakati katika vita vya Hunain, kwa mara ya mwanzo Waislam walipigana vita idadi yao ikiwa kubwa zaidi kuliko ya makafiri lakini waliendeshwa mbio na makafiri mpaka Allaah alipowateremshia utulivu wake. Hakupata Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutoka na jeshi kubwa kuliko la siku hiyo, alitoka na watu elfu kumi na mbili, hata Waislam wakawa wanasema:
“Hatutoshindwa leo kwa sababu ya uchache wetu” [kwa vile tuko wengi leo hatutoshindwa]
Allaah anasema:
{{Bila shaka Allaah amekunusuruni katika mapigano mengi, na siku ya Hunaiyn (pia) ambapo wengi wenu ulikupandisheni kichwa, lakini haukukufaeni chochote, na ardhi ikawa dhiki juu yenu ingawa ilikuwa yenye wasaa, kisha mkageuka mkarudi nyuma.}} [Suuratut-Tawbah: 25]
Anasema Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) kuwa:
“Katika vita vya Yarmuuk, ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliwaambia Waislam:
“Mtakapotaka msaada katika vita hivi, basi muandikieni Abu ‘Ubaidah”.
Vita vilipoanza, wakamuandikia Abu ‘Ubaidah aje kuwasaidia, na kwamba wako katika hatari. Abu ‘Ubaidah akawaandikia hivi:
“Imenifikia barua yenu ikitaka msaada kutoka kwangu, lakini mimi nitakujulisheni yule atakayeweza kukusaidieni mkapata ushindi kuliko nitakavyoweza kukusaidieni mimi; - Allaahu ‘Azza wa Jallah – ombeni msaada kutoka kwake mkitaka kupata ushindi. Kwa sababu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipewa ushindi na Allaah siku ya Badr akiwa na watu wachache kuliko nyinyi. Itakapokufikieni barua yangu hii, piganeni nao na wala msiniandikie mimi.”
Anasema Iyaadh Al-‘Ash-ary (Radhiya Allaahu ‘anhu), mwenye kuisimulia Hadiyth hii:
“Tukapambana nao na tukawashinda, na tukapata ngawira nyingi siku hiyo”.

0 Comments