September 19, 2017

KISA CHA ASWHAABUL-KAHF (Watu Wa Pangoni) SEHEMU YA 2

Imekusanywa Na: www.muislamu.com


وَتَرَى الشَّمْسَ إِذَا طَلَعَت تَّزَاوَرُ عَن كَهْفِهِمْ ذَاتَ الْيَمِينِ وَإِذَا غَرَبَت تَّقْرِضُهُمْ ذَاتَ الشِّمَالِ وَهُمْ فِي فَجْوَةٍ مِّنْهُ ذَلِكَ مِنْ آيَاتِ اللَّهِ مَن يَهْدِ اللَّهُ فَهُوَ الْمُهْتَدِي وَمَن يُضْلِلْ فَلَن تَجِدَ لَهُ وَلِيًّا مُّرْشِدًا

Na unaliona jua linapochomoza linainamia kuliani mwao kutoka hapo pangoni; na linapokuchwa linawakwepa kushotoni, na wao wamo katika uwazi wa pango. Hizo ni katika Ishara za Allaah. Ambaye Allaah Anamwongoa basi huyo ni mwenye kuongoka. Na Anayemuacha kupotea basi hutampatia mlinzi wala mwongozi

 وَتَحْسَبُهُمْ أَيْقَاظًا وَهُمْ رُقُودٌ وَنُقَلِّبُهُمْ ذَاتَ الْيَمِينِ وَذَاتَ الشِّمَالِ وَكَلْبُهُم بَاسِطٌ ذِرَاعَيْهِ بِالْوَصِيدِ لَوِ اطَّلَعْتَ عَلَيْهِمْ لَوَلَّيْتَ مِنْهُمْ فِرَارًاوَلَمُلِئْتَ مِنْهُمْ رُعْبًا  
Na utawadhania wamacho, na hali wamelala. Nasi Tunawageuza kulia na kushoto. Na mbwa wao amenyoosha miguu yake ya mbele kizingitini. Kama ungeliwatokea hapana shaka ungeligeuka kuwakimbia, nawe umejaa khofu.

 وَكَذَلِكَ بَعَثْنَاهُمْ لِيَتَسَاءلُوا بَيْنَهُمْ قَالَ قَائِلٌ مِّنْهُمْ كَمْ لَبِثْتُمْ قَالُوا لَبِثْنَا يَوْمًا أَوْ بَعْضَ يَوْمٍ قَالُوا رَبُّكُمْ أَعْلَمُ بِمَا لَبِثْتُمْ فَابْعَثُوا أَحَدَكُم بِوَرِقِكُمْ هَذِهِ إِلَى الْمَدِينَةِ فَلْيَنظُرْ أَيُّهَا أَزْكَى طَعَامًا فَلْيَأْتِكُم بِرِزْقٍ مِّنْهُ وَلْيَتَلَطَّفْ وَلَا يُشْعِرَنَّ بِكُمْ  
Na kwa namna hii Tuliwainua usingizini wapate kuulizana wao kwa wao. Alisema msemaji katika wao: Mmekaa muda gani? Wakasema: Tumekaa siku moja au sehemu ya siku. Wakasema: Mola wenu Anajua zaidi muda mliokaa. Hebu mtumeni mmoja wenu na hizi fedha zenu ende mjini, akatazame chakula chake kipi kilicho bora kabisa akuleteeni cha kukila. Naye afanye mambo hayo kwa busara, wala asikutajeni kabisa kwa yeyote.

إِنَّهُمْ إِن يَظْهَرُوا عَلَيْكُمْ يَرْجُمُوكُمْ أَوْ يُعِيدُوكُمْ فِي مِلَّتِهِمْ وَلَن تُفْلِحُوا إِذًا أَبَدًا
Kwani wao wakikutambueni watakupigeni mawe, au watakurudisheni katika dini yao, na hapo hamtafanikiwa kabisa. [Al-Kahf: 17-20].

Tunaendelea na Kisa cha Asw-haabul-Kahf, baada ya kukimbilia pangoni vijana hao, na kulala humo kuwa muda wa miaka zaidi ya mia tatu, bila ya kujulikana na watu, na hivyo ni kutokana na Rahmah ya Allaah (سبحانه وتعالى).

 وَتَرَى الشَّمْسَ إِذَا طَلَعَت تَّزَاوَرُ عَن كَهْفِهِمْ ذَاتَ الْيَمِينِ وَإِذَا غَرَبَت تَّقْرِضُهُمْ ذَاتَ الشِّمَالِ وَهُمْ فِي فَجْوَةٍ مِّنْهُ ذَلِكَ مِنْ آيَاتِ اللَّهِ مَن يَهْدِ اللَّهُ فَهُوَ الْمُهْتَدِي وَمَن يُضْلِلْ فَلَن تَجِدَ لَهُ وَلِيًّا مُّرْشِدًا   
Na unaliona jua linapochomoza linainamia kuliani mwao kutoka hapo pangoni; na linapokuchwa linawakwepa kushotoni, na wao wamo katika uwazi wa pango. Hizo ni katika Ishara za Allaah. Ambaye Allaah Anamwongoa basi huyo ni mwenye kuongoka. Na Anayemuacha kupotea basi hutampatia mlinzi wala mwongozi

Sehemu lililokuwepo pango:
Hapa inaonyesha kwamba mlango wa pango hilo ulielelekea upande wa Kaskazini kwa sababu Allaah (سبحانه وتعالى) Anatuambia kwamba jua lilipokuwa linachomoza, mwangaza ulikuwa unaingia katika pango.
 ذات اليمين
 kuliani mwao
 وَتَرَى الشَّمْسَ إِذَا طَلَعَت تَّزَاوَرُ عَن كَهْفِهِمْ ذَاتَ الْيَمِينِ
Na unaliona jua linapochomoza linainamia kuliani mwao kutoka hapo pangoni.

Maana: Kivuli kilipungua upande wa kulia kama alivyosema Ibn 'Abbaas, Sa'iyd bin Jubayr na Qataadah.

 وَإِذَا غَرَبَت تَّقْرِضُهُمْ ذَاتَ الشِّمَالِ
 na linapokuchwa linawakwepa kushotoni

Maana: Jua liliingia katika pango lao kutoka upande wa kushoto wa mlango wa pango, ina maana kutoka upande wa Magharibi.

Ibn 'Abbaas, Mujaahid na Qataadah wamesema kwamba:
  تَّقْرِضُهُمْ
 Linawakwepa
Yaani Jua lilikuwa likiwaangazia kisha likiwaondokea. [Atw-Twabariy 17: 621,622].

Allaah (سبحانه وتعالى) Ametuambia haya na Ametaka tufahamu na tutafakari maana yake, lakini Hakutuambia sehemu iliokuwepo hilo pango, yaani nchi gani, kwa sababu hakuna faida kwetu kujua hilo na haipatikani lengo la kujifunza Shari’ah ndani yake. Na kama ingelikuwa inapatikanamaslahi ya kiroho au ya kidini basi Allaah (سبحانه وتعالىna Mjumbe Wake wangelitufundisha kwa kutupa maelezo yake kama alivyosema Mtume (صلى الله عليه  وآله وسلم):
((والذي نفسي بيده ما تركت شيئا يقربكم من الجنة ويباعدكم عن النار إلا أمرتكم به، وما تركت شيئا يقربكم من النار، ويباعدكم عن الجنة إلا نهيتكم عنه))     
((Naapa Kwa Yule Ambaye nafsi yangu iko katika mikono Yake, sikuacha jambo la kukukurubisheni na Pepo na la kukuwekeni mbali na moto ila nimekwisha kukuamrisheni nalo. Wala sikuacha jambo la kukukurubisheni na moto na kukuwekeni mbali na Pepo ila nimekwisha kukukatazeni nalo)).[Swahiyh ya Shaykh Al-Albaaniy رحمه الله ].
Ibn 'Abbaas anatafsiri kuhusu:
 تَّزَاوَرُ عَن كَهْفِهِمْ ذَاتَ الْيَمِينِ وَإِذَا غَرَبَت تَّقْرِضُهُمْ ذَاتَ الشِّمَالِ وَهُمْ فِي فَجْوَةٍ مِّنْهُ
...linainamia kuliani mwao kutoka hapo pangoni; na linapokuchwa linawakwepa kushotoni, na wao wamo katika uwazi wa pango.

Maana, jua liliingia katika pango bila ya kuwagusa, kwa sababu lingeliwagusa, lingeliwaunguza miili yao na nguo zao. [Atw-Twabariy 17: 620].

 ذَلِكَ مِنْ آيَاتِ اللَّهِ
Hizo ni katika Ishara za Allaah.
Ni Ishara ya Allaah (سبحانه وتعالى) Kuwaongoza katika pango na ni miujiza Yake kuwajaalia kuwa hai, na jua na upepo ukipita katika pango kuwahifadhi miili yao.

Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema:
 مَن يَهْدِ اللَّهُ فَهُوَ الْمُهْتَدِي وَمَن يُضْلِلْ فَلَن تَجِدَ لَهُ وَلِيًّا مُّرْشِدًا
Ambaye Allaah Anamwongoa basi huyo ni mwenye kuongoka. Na Anayemuacha kupotea basi hutampatia mlinzi wala mwongozi.

Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Aliyewaongoza hawa vijana katika uongofu wa haki, kwani yule Anayemuongoa hakuna wa kumpotoa na Anayempotoa hakuna wa kumuongoa.

 وَتَحْسَبُهُمْ أَيْقَاظًا وَهُمْ رُقُودٌ وَنُقَلِّبُهُمْ ذَاتَ الْيَمِينِ وَذَاتَ الشِّمَالِ وَكَلْبُهُم بَاسِطٌ ذِرَاعَيْهِ بِالْوَصِيدِ لَوِ اطَّلَعْتَ عَلَيْهِمْ لَوَلَّيْتَ مِنْهُمْ فِرَارًاوَلَمُلِئْتَ مِنْهُمْ رُعْبًا  
Na utawadhania wamacho, na hali wamelala. Nasi Tunawageuza kulia na kushoto. Na mbwa wao amenyoosha miguu yake ya mbele kizingitini. Kama ungeliwatokea hapana shaka ungeligeuka kuwakimbia, nawe umejaa khofu.

Kulala kwao katika pango:

Baadhi wa wafasiri wa Qur-aan wamesema kuwa Allaah (سبحانه وتعالى) Alipowafanya walale, kope za macho yao hazikufunga. Kubakia kwa macho yao kuwa wazi ilikuwa ni bora kwa sababu ya kuhifadhi macho yao, kama inavyosemekana kuwa mbwa mwitu akilala anafunga jicho moja na moja huliacha wazi, kisha anabadilisha jicho jingine huku amelala.

  وَتَحْسَبُهُمْ أَيْقَاظًا وَهُمْ رُقُودٌ  
 Nawe utawadhania wamacho, na hali wamelala.

 وَنُقَلِّبُهُمْ ذَاتَ الْيَمِينِ وَذَاتَ الشِّمَالِ
 Nasi tunawageuza kulia na kushoto.

Ibn 'Abbaas kasema: Kama wasingelikuwa wanageuka, ardhi ingeliwafanya waoze. [Atw-Twabariy 17: 620].
 وَكَلْبُهُم بَاسِطٌ ذِرَاعَيْهِ بِالْوَصِيدِ
 Na mbwa wao amenyoosha miguu yake ya mbele kizingitini.

Ibn 'Abbaas, Mujaahid, Sa'iyd bin Jubayr na Qataadah wamesema: Waswiyd ina maana kizingiti. Ibn 'Abbaas kasema: “pembeni mwa mlango”. Pia imesemwa kuwa ni ardhini. Lakini usemi wa rai ya uhakika ni kuwa ni kizingiti cha mlango (wa pango). [Atw-Twabariy 17: 624-625].

Kama vile iliyvotajwa katika Aayah ya Suratul-Humazah: 8
 إِنَّهَا عَلَيْهِم مُّؤْصَدَةٌ
Hakika huo utafungiwa nao.

Mbwa wao alilala chini katika mlango. Na hivyo ni tabia ya mbwa. Na kazi yake mbwa kulinda kama alivyosema Ibn Jubayr.  Mbwa huyo alikaa nje ya mlango kwa sababu Malaika hawaingii nyumba iliyo na mbwa kama ilivyosimuliwa katika Al-Bukhaariy, wala hawaingii katika nyumba iliyo na picha za viumbe zilizochorwa au vinyago.

Neema hiyo ya kulala ilimfikia mpaka mbwa wao. Na hii ni mfano wa faida ya kuambatana na watu wema. Ilisemekana, kwamba huyo mbwa alikuwa wa mpishi wa mfalme ambaye aliawaamini vijana hao kuhusu Dini yao ya Tawhiyd. Na Allaah Anajua zaidi.

 لَوِ اطَّلَعْتَ عَلَيْهِمْ لَوَلَّيْتَ مِنْهُمْ فِرَارًا وَلَمُلِئْتَ مِنْهُمْ رُعْبًا
Kama ungeliwatokea hapana shaka ungeligeuka kuwakimbia, nawe umejaa khofu

Maana yake ni: Vile Allaah Alivyowafanya waonekane wanatisha ili mtu asiwakaribie kuwagusa na kuwaamsha mpaka muda Alioutaka Allaah (سبحانه وتعالى) walale uishe. Hii ni Hikma na Rahmah Yake Allaah (سبحانه وتعالى).

Walipoamka wakamtuma mmoja wao sokoni kununua chakula,

 وَكَذَلِكَ بَعَثْنَاهُمْ لِيَتَسَاءلُوا بَيْنَهُمْ قَالَ قَائِلٌ مِّنْهُمْ كَمْ لَبِثْتُمْ قَالُوا لَبِثْنَا يَوْمًا أَوْ بَعْضَ يَوْمٍ قَالُوا رَبُّكُمْ أَعْلَمُ بِمَا لَبِثْتُمْ فَابْعَثُوا أَحَدَكُم بِوَرِقِكُمْ هَذِهِ إِلَى الْمَدِينَةِ فَلْيَنظُرْ أَيُّهَا أَزْكَى طَعَامًا فَلْيَأْتِكُم بِرِزْقٍ مِّنْهُ وَلْيَتَلَطَّفْ وَلَا يُشْعِرَنَّ بِكُمْ أَحَدًا  
Na kwa namna hii Tuliwainua usingizini wapate kuulizana wao kwa wao. Alisema msemaji katika wao: Mmekaa muda gani?  Wakasema: Tumekaa siku moja au sehemu ya siku. Wakasema: Mola wenu Anajua zaidi muda mliokaa. Hebu mtumeni mmoja wenu na hizi fedha zenu ende mjini, akatazame chakula chake kipi kilicho bora kabisa akuleteeni cha kukila. Naye afanye mambo hayo kwa busara, wala asikutajeni kabisa kwa yeyote.

Maana ya kauli hiyo ya Allaah (سبحانه وتعالى) ni: Tulivyowafanya kulala, tumewafufua na miili yao, nywele na ngozi zao, bila ya kuharibika kiungo chochote cha mwili wao na hakuna kilichopunguka katika kuonekana kwao. Hii ni baada ya miaka 309, ndio maana wakawa wanaulizana,
 كَمْ لَبِثْتُمْ
Mmekaa muda gani?

Kwa sababu walipoingia katika pango ilikuwa mwanzo wa siku na walipoamka ilikuwa mwisho wa siku ndio maana wakasema,
 قَالُوا لَبِثْنَا يَوْمًا أَوْ بَعْضَ يَوْم
 Wakasema: Tumekaa siku moja au sehemu ya siku.

 قَالُوا رَبُّكُمْ أَعْلَمُ بِمَا لَبِثْتُمْ
Wakasema: Mola wenu Anajua zaidi muda mliokaa.

Maana: Allaah Anajua zaidi hali yenu. Walikuwa hawana hakika muda waliolala, lakini Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Ajuaye. Wakaelekea kutafuta mahitajio yaliyo muhimu kwao nayo ni chakula na kinywaji, hivyo wakasema:

 فَابْعَثُوا أَحَدَكُم بِوَرِقِكُمْ هَذِهِ إِلَى الْمَدِينَةِ
Hebu mtumeni mmoja wenu na hizi fedha zenu ende mjini.

Walikuwa na pesa zao za Dirhams; zilokuwa zikitumika wakati huo. Walizitoa baadhi yake katika swadaqah na baadhi waliweka kwa ajili ya matumizi. Wakamtuma mmoja wao aende mjini (mji wao waliokuwa wakiishi) ili kutafuta chakula kilicho safi kabisa.

 فَلْيَنظُرْ أَيُّهَا أَزْكَى طَعَامًا  
 ...akatazame chakula chake kipi kilicho bora kabisa..

أَزْكَى hapa inamaanisha: Kilichotakasika. Maana yake ni kama ilivyotajwa katika Aayah zifautazo:   

  وَلَوْلَا فَضْلُ اللَّهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ مَا زَكَا مِنكُم مِّنْ أَحَدٍ أَبَدًا
Na lau kuwa si fadhila za Allaah na Rahmah Yake   juu yenu, asingelitakasika miongoni mwenu kabisa hata mmoja. [An-Nuwr:  21].

 قَدْ أَفْلَحَ مَن تَزَكَّى
Hakika amekwishafanikiwa aliyejitakasa [Al-A’laa: 14].

 فَلْيَأْتِكُم بِرِزْقٍ مِّنْهُ
 akuleteeni cha kukila..
 وَلْيَتَلَطَّفْ
 Naye afanye mambo hayo kwa busara..

Kwa maana: Ajihadhari asije kutambulikana anapokwenda kununua chakula na anaporudi.

 وَلَا يُشْعِرَنَّ بِكُمْ أَحَدًا
wala asikutajeni kabisa kwa yeyote.

Aayah zinaendelea:

 إِنَّهُمْ إِن يَظْهَرُوا عَلَيْكُمْ يَرْجُمُوكُمْ أَوْ يُعِيدُوكُمْ فِي مِلَّتِهِمْ وَلَن تُفْلِحُوا إِذًا أَبَدًا
Kwani wao wakikutambueni watakupigeni mawe, au watakurudisheni katika dini yao; na hapo hamtafanikiwa kabisa.

  إنّهُمْ إِن يَظْهَرُوا عَلَيْكُمْ  
 Kwani wao wakikutambueni
 يَرْجُمُوكُمْ أَوْ يُعِيدُوكُمْ فِي مِلَّتِهِمْ
watakupigeni mawe, au watakurudisheni katika dini yao

Walikusudia ni watu wa ule mji wa Decianus, ambao waliogopa kuwa wakiwajua watawaadhibu kwa kuwatesa kwa kila aina ya mateso ili warudi dini yao ya kuabudu masanamu, au wawatese mpaka wawaue. Lakini vijana hao, ilikuwa ni bora kwao kufa kuliko kurudia dini ya ushirikina kwani walitambua kuwa hawatofaulu duniani wala akhera, ndio maana wakasema,

 وَلَن تُفْلِحُوا إِذًا أَبَدًا
 na hapo hamtofanikiwa kabisa.


Mafunzo na Hidaaya:

  1. Kudhihirisha upole wa Allaah (سبحانه وتعالى) kwa Awliyaa (Vipenzi) Wake kwa kuwakirimu wanapohajiri kwa ajili Yake.
  2. Uongofu umo katika Mikono ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwa hiyo aliyeongoka ameongozwa na Allaah (سبحانه وتعالى) na aliyepotea (kwa kujipotosha mwenyewe) basi, amepotezwa na Allaah (سبحانه وتعالى). Inatupasa tumuombe Allaah (سبحانه وتعالى) Hidaaya na tujikinge Kwake dhidi ya upotofu. 
  3. Udhihirisho wa Qudra (Uwezo) wa Allaah (سبحانه وتعالى) na Ujuzi Wake na Hikma Yake.    
  4. Inampasa Muislamu kutafuta chakula na kinywaji cha halali na mengineyo.
  5. Kufariki katika shirki na kufru kunamzuia mtu kupata kufaulu siku ya Qiyaamah.


Itaendelea in Shaa Allaah ...3

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only