KISA CHA JULAYBIYB NA SWAHAABIYYAH ALIYEMTII MTUME (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)Swahaba aliyeitwa Julaybiyb alijulikana sana  kuwa alikuwa ni mtu duni asiyemiliki mali na hakuwa ni mzuri kwa sura na umbo, na alikuwa ni mtu wa kuchekesha watu. Kwa hivyo hakuna aliyetaka kumuozesha binti yake. Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alimuuliza Julaybib kama anataka kuoa, naye akamjibu: "Ewe Mjumbe wa Allah, nani atakayekubali nimuoe mimi? Sina nyumba wala wala mali wala chochote katika mapambo ya dunia".

Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akamtuma mtu mmoja aende nyumba ya Answaariy fulani ambao walikuwa ni familia yenye kujulikana kwa kabila lao maarufu kubwa lenye kujulikana kwa heshima na wenye hali nzuri. Alipopiga hodi, alifungua mlango mama wa binti huyo. Swahaba akamjulisha kuwa ametumwa na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kuleta posa kwa binti yake. Mama huyo alifurahi sana kudhania kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ndiye anayetaka kumposa binti yake.

Swahaba Alipomjulisha kuwa sio kwa ajili ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم, bali ni kwa ajili ya Julaybiyb, mama huyo alisema: "Nani? Julaybib? Hapana! Hatumuozeshi yeye binti yetu!". Mara yule binti alisikia mazungumzo hayo akaja kuuliza vizuri: "Nani anayetaka kuniposa?" Mama mtu akamuelezea kuwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amemtuma mtu aje kumposa yeye kwa ajili ya Julaybiyb. Binti huyo alimwambia mama yake: "Vipi mama unakataa amri ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم? Fuata amri yake kwani hakuna kitakachonidhuru". (Katika usemi mmoja ni kwamba hapo hapo Aayah ifuatayo iliteremshwa [Ibnu Kathiyr 7:692-694]) na katika usemi mwingine aliwaambia wazazi wake: "Hamkusikia kauli ya Allaah سبحانه وتعالى :


((وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَمْرًا أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ وَمَن يَعْصِ اللَّهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُّبِينًا))
((Haiwi kwa Muumini mwanamume wala Muumini mwanamke kuwa na khiari katika jambo, Allah na Mtume Wake Wanapokata shauri katika jambo lao. Na mwenye kumuasi Allah na Mtume Wake basi hakika amepotea upotofu ulio wazi))[Al-Ahzaab:36]

Ikabidi wamuozeshe binti yao kwa Julaybiyb. Kisha katika vita fulani alitoka Mtume صلى الله عليه وآله وسلم na Maswahaba miongoni mwao ni Julaybiyb na baada ya ushindi wa vita hivyo, Mtume صلى الله عليه وآله وسلمaliwauliza Maswahaba kabla ya kurudi: ((Je, kuna mtu aliyekosekana?))

Wakataja baadhi ya Maswahaba waliokosekana kisha Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akawauliza tena wakasema: "Hakuna mtu mwingine aliyekosekana: Lakini Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akasema: ((Lakini mimi naona kwamba Julaybiyb amekosekana)) yaani hayupo na sisi. (Nendeni mkamtafute miongoni mwa waliouliwa)).

Wakaenda Maswahaba kumtafuta wakamkuta ameuawa akiwa karibu yake makafiri saba ambao aliwahi kuwaua yeye Julaybiyb. Maswahaba wakamjulisha Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ambaye alikwenda na kusimama karibu naye kisha akasema: ((Ameua saba kisha wakamuua. Yeye ni wangu na mimi ni wake)).

Alisema hivyo mara mbili au tatu, kisha Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akambeba kwa mikono yake na kwenda kumzika. Na akamuombea Du'aa mke wake:
((الَّلهُمَّ، صَبَّ عَلَيْهَا [الخير] صَبَّا، وَلاَ تَجْعَل عَيْشَها كَدَّا))
((Ewe Allah, Mjaze kheri (nyingi) zilizojaa na Usimjaaliye maisha yake kuwa ni ya shida [tabu na mashaka]))

Imesemekana kwamba hakuweko mjane aliyekuwa ana maisha mema kama maisha ya mke wa Julaybiy رضي الله عنه.
[Kisa kimesimuliwa na Imaam Ahmad Muslim na An-Nasaaiy]

0 Comments