MDHUKURU ALLAAH KWA WINGI NA OMBA MAGHIFIRAH BAADA YA KUTENDA MEMA KATIKA SIKU KUMI BORA ZAIDI ZA ALLAAH

Mdhukuru Allaah Kwa Wingi Na Omba Maghfirah Baada Ya Kutenda Mema
Katika Siku Kumi Bora Kabisa Za AllaahAnasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  

وَاذْكُرُوا اللَّـهَ فِي أَيَّامٍ مَّعْدُودَاتٍ ۚ  
Na mdhukuruni Allaah katika siku za kuhesabika.  [[Al-Baqarah:203]


Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) kasema: "Siku zinazohisabiwa ni siku za Tashriyq" (11, 12, 13 Dhul-Hijjah) [Al-Qurtwubiy: 3.3] Kwa maana ni siku ya pili, ya tatu na ya nne baada ya siku ya 'Iyd. Hivyo ndivyo Anavyotuamrisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kuwa tumdhukuru baada ya kusherehekea siku kuu yetu ya 'Iydul-Adhwhaa ('Iyd ya kuchinja). Na hivi ndivyo ilivyo desturi ya ‘ibaadah zetu kuwa zinamalizika kwa kuambatana na mema na si kwa maasi.

Mahujaji wanapotekeleza Hajj ipasavyo na wanapomaliza kisimamo cha 'Arafah, huwa wameghufuriwa madhambi yao yote kama ilivyotajwa katika Hadiyth ifuatayo:

عن عائشة رضي الله عنها عن النبي صلى الله عليه وسلم قال :((ما من يوم أكثر من أن يعتق الله فيه عبدأ من النار من يوم عرفة، وإنه ليدنو ثم يباهي بهم الملائكة فيقول: ما أراد هؤلاء؟))   مسلم  
 Kutoka kwa Mama wa Waumini 'Aishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: ((Hakuna siku ambayo Allaah Huwaacha waja huru zaidi kutokana na moto kama siku ya 'Arafah, na siku hiyo Allaah Hukaribia (Huteremka katika mbingu ya dunia
 [kwa namna inayomstahiki Yeye]) kisha kwa fakhari Husema kwa Malaika Wake: Wanataka nini hawa (waja wangu?))?[Muslim]

Na katika usimulizi ufuatao pia imetajwa kufughuriwa kwao madhambi:

عن أبي هريرة رضي الله عنه ((إن الله تعالى يباهي بأهل عرفات ملائكة السماء ، يقول : انظروا إلى عبادي ، أتوني شعثا غبرا من كل فج عميق ، أشهدكم أني قد غفرت لهم)) المصدرحلية الأولياء خلاصة الدرجةصحيح  الشيخ األباني 
Kutoka kwa Abuu Huraryah (Radhwiya Allaahu 'anhu) ((Allaah Huwafakharisha watu (waliosimama) 'Arafah kwa Malaika wa mbinguni na Husema: Watazameni waja Wangu waliokuja wamejaa nywele, wana mavumbi, wamekuja kutoka kila pande (za dunia) Nakushuhudieni kuwa Nimewaghufuria)) [Hilyat al-Awliyaa – Shaykh Al-Albaaniy kaipa daraja ya swahiyh]


Lakini juu ya kwamba wameghufuriwa, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Anawaamrisha Mahujaji wamdhukuru kwa wingi na waombe maghfirah Kwake baada ya kumaliza  Hajj:


  فَإِذَا أَفَضْتُم مِّنْ عَرَفَاتٍ فَاذْكُرُوا اللَّـهَ عِندَ الْمَشْعَرِ الْحَرَامِ ۖ وَاذْكُرُوهُ كَمَا هَدَاكُمْ وَإِن كُنتُم مِّن قَبْلِهِ لَمِنَ الضَّالِّينَ ﴿١٩٨﴾ 
Basi mtakapomiminika kutoka ‘Arafaat mdhukuruni Allaah kwenye Mash’aril- Haramu (Muzdalifah) na mdhukuruni Yeye kama Alivyokuongozeni kwani hakika mlikuwa kabla ya hapo ni miongoni mwa waliopotea.

 ثُمَّ أَفِيضُوا مِنْ حَيْثُ أَفَاضَ النَّاسُ وَاسْتَغْفِرُوا اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿١٩٩﴾
Kisha miminikeni kutoka pale wamiminikapo watu; na ombeni maghfirah kwa Allaah. Hakika Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu.


فَإِذَا قَضَيْتُم مَّنَاسِكَكُمْ فَاذْكُرُوا اللَّـهَ كَذِكْرِكُمْ آبَاءَكُمْ أَوْ أَشَدَّ ذِكْرًا Mtakapomaliza kutekeleza manaasik(‘ibaadah za Hajj) zenu, basi mdhukuruni Allaah kama mnavyowadhukuru baba zenu au kumdhukuru zaidi. [Al-Baqarah: 198-200]

Amri hii ya kuomba maghfirah na kumdhukuru kwa wingi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kila baada ya amali njema tunapata katika mafunzo ya Qur-aan na Sunnah.  Haya ni mafunzo kwetu kujidhalilisha kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  na kuishi daima katika hali ya matumaini na khofu (al-khawf war-rajaa). Na hivi ndivyo hali ya Waumini inavyopasa kuwa kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Alipoteremsha Aayah:

وَالَّذِينَ يُؤْتُونَ مَا آتَوا وَّقُلُوبُهُمْ وَجِلَةٌ أَنَّهُمْ إِلَىٰ رَبِّهِمْ رَاجِعُونَ ﴿٦٠﴾
60. Na ambao wanatoa vile walivyopewa na huku nyoyo zao zinakhofu kwamba hakika watarejea kwa Rabb wao [Al-Muuminuwn:60]  

Mama wa Waumini 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa), alimuuliza Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ilipoteremshwa Aayah hii: "Ee Rasuli wa Allaah, je, wale wale ambao wanaiba, wanazini na kulewa huku wakimkhofu Allaah?" Akajibu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Sio ee bint Abubakar, Bintis-Swiddiyq! Hao ni wanaoswali, wanafunga, wanatoa swadaqah na huku wanamkhofu Allaah 'Azza wa Jalla)) [Imaam Ahmad]


Tukiangaza katika Siyrah ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), tokea kuanza da'wahyake kama Rasuli wa Allaah, zile tabu alizopata, maudhi mbali mbali ya Makafiri wa Ki-Quraysh, watu wake kumtenga, kufukuzwa na kupigwa mawe na watu wa Twaaif, maafa mbali mbali yaliyomjaza huzuni kubwa, juhudi nzito za kupigana vita na Makafiri, na mengi mengineyo, hadi mwisho wa Fat-huMakkah (Ufunguzi wa (kuitwaa) Makkah), makundi kwa makundi  ya watu waliingia  katika dini ya Kiislam. Mafanikio hayo yamechukua muda wa miaka 23 tokea alipopewa Urasuli Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hadi kukaribia kufariki  kwake. Tujiulize, je, baada ya kufaulu huko, ni jambo gani Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Alimfunza afanye? Jibu ni uteremsho wa Suwrah tukufu ifuatayo:

 بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

إِذَا جَاءَ نَصْرُ اللَّـهِ وَالْفَتْحُ ﴿١﴾
Itakapokuja nusura ya Allaah na ushindi.

وَرَأَيْتَ النَّاسَ يَدْخُلُونَ فِي دِينِ اللَّـهِ أَفْوَاجًا ﴿٢﴾
Na utawaona watu wanaingia katika Dini ya Allaah makundi makundi.


فَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ وَاسْتَغْفِرْهُۚ إِنَّهُ كَانَ تَوَّابًا ﴿٣﴾
Basi sabbih kwa Himidi za Rabb wako na muombe maghfirah; hakika Yeye daima ni Mwingi mno wa kupokea tawbah.    [An-Naswr: 1-3]


Ni Suwrah ya mwisho iliyoteremshwa kikamilifu [kauli ya ibn 'Abbaas katika Swahiyh Muslim]

Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) mwenyewe na hata Maswahaba walitambua kuwa hii ni alama ya kukaribia mauti yake.

Mfano mwengine mzuri tunao wa kipenzi cha Allaah  (Khaliylul-Allaah) Nabiy 'Ibraahiym (alayhis-salaam) alipomaliza kujenga Ka'bah yeye na mwanawe Ismaa'iyl. Ka'bah hiyo inayozungukwa na mamilioni ya Waislamu kama ni ‘ibaadah tukufu tokea siku hizo hadi siku ya Qiyaamah. Lakini hawakutegemea kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)    Atawapokelea amali hiyo moja kwa moja, bali kwanza wamemuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Awatakabalie kisha Awaghufurie:


وَإِذْ يَرْفَعُ إِبْرَاهِيمُ الْقَوَاعِدَ مِنَ الْبَيْتِ وَإِسْمَاعِيلُ رَبَّنَا تَقَبَّلْ مِنَّا ۖ إِنَّكَ أَنتَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ ﴿١٢٧﴾
Na (taja) aliponyanyua Ibraahiym na Ismaa’iyl msingi wa Nyumba (Al-Ka’bah): “Mola wetu, Tutakabalie, hakika Wewe ni Mwenye kusikia yote, Mjuzi wa yote.

 رَبَّنَا وَاجْعَلْنَا مُسْلِمَيْنِ لَكَ وَمِن ذُرِّيَّتِنَا أُمَّةً مُّسْلِمَةً لَّكَ وَأَرِنَا مَنَاسِكَنَا وَتُبْ عَلَيْنَا ۖ إِنَّكَ أَنتَ التَّوَّابُ الرَّحِيمُ ﴿١٢٨﴾
 “Rabb wetu, Tujaalie tuwe wenye kujisalimisha Kwako pamoja na kizazi chetu wawe ummah wenye kujisalimisha Kwako na Tuonyeshe taratibu za ‘ibaadah zetu na Pokea tawbah zetu, hakika Wewe ni Mwingi wa kupokea tawbah, Mwenye kurehemu.      [Al-Baqarah: 127-128]


Vile vile Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha kuwa kila tunapomaliza Swalaah za fardhi     tuombe maghfirah mara tatu kwa kusema:

أَسْـتَغْفِرُ الله   
AtastaghfiruLLah
“Naomba maghfirah kwa Allaah”  

Ikiwa hali ni kama hizo tulizozitaja zote, basi na sisi tutakapomaliza kutenda mema katika siku kumi bora kabisa za Allaah, za Dhul-Hijjah, inatupasa tuombe maghfirah na tumdhukuru  kwa wingi  Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kwani hatujui kama ‘amali zetu zitakuwa zimetakabaliwa au laa. Desturi hii tuwe tunaidumisha daima tunapotoka kumaliza kutenda ‘amali na ‘ibaada zozote zile tuzifanyazo kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).   

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Atuwezeshe kuzidisha juhudi kufanya mema mengi tukiwa na matumaini na pia khofu ya kukubaliwa  amali zetu.  Aamiyn.

0 Comments