UJUE UKWELI KUHUSU DUA YA ALBADIRI KATIKA DINI YA UISLAMU


Sheikh Muhmmad Issa, Mwananchi
Hivi karibuni, kumeibuka harakati za kuomba dua iitwayo Albadiri kwa ajili ya kuwalaani waliompiga risasi Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Tundu Antipas Lissu.
Kabla ya kujikita katika maudhui hii, nichukue fursa hii na mimi kutoa pole kwa yaliyompata na pia kwa familia yake na wale wote wanaomhusu. Kitendo cha kupigwa risasi binadamu yeyote yule hadharani kinapaswa kuchukiwa na kila mpenda amani.
Nikirudi katika hoja ya makala haya, wasiokuwa Waislamu na hata Waislamu wamekuwa wakisikia kisomo cha ‘Albadiri’ au wengine huiita ‘Alalbadiri’ na kwamba hutumika kumsomea mtu au watu waovu kama vile wezi, majambazi na wauaji, watu waliofanya dhulma fulani na mengineyo.
Niwajulishe wasomaji kwamba asili ya neno ‘Albadiri’ au ‘Ahlalbadiri’ ni maneno ya kiarabu Ahlul Badri. Ahlu ni kitu au watu. Badri ni mahali karibu na mji wa Madina nchini Saudi Arabia ambapo vita vya kwanza kati ya Waarabu wa Kikureshi na Waislamu vilipiganwa na Waislamu wakashinda. Soma zaidi Vita vya Badr
Jeshi la Waislamu lilikuwa na wapiganaji 313 na katika vita hivi wako waliouawa na wengine kujeruhiwa, lakini pia wako waliosalimika na kuishi miaka kadhaa baadae. Wote hao hujulikana kama Ahlul Badri yaani Maswahaba wa Mtume Muhammad (rehma na amani ziwe juu yake) ambao walipigana vita vya Badri. Hivyo tunaposema Ahl badr tunamaanisha wale watu walioipigana vita hii.


Asili ya dua ya Ahlul Badri
Asili ya dua iitwayo Ahlul Badri ni imani potofu kwamba kumuomba Allaah kupitia majina ya masahaba waliopigana vita vya Badri ni kujikaribisha kwa Allaah kwa kutaja majina ya watu hao wema.
Kitendo hiki huwa kinaitwa ‘Al-istighaatha’ yaani kumuomba Alllaah msaada, faraja au nusura. Kwa hiyo hicho kiitwacho Alabadri kimechukuliwa kama dua maalumu ya kumuomba Allaah hasa mtu au watu wanapodhulumiwa.
Je, Albadiri inaruhusiwa katika Uislamu?
Hakika kumuomba Allaah msaada, faraja au nusura ni jambo ambalo siyo tu ni jambo lililoruhusiwa katika mafundisho ya Uislamu, bali ni jambo lililosisitizwa kwamba mtu au watu wanapofikwa na msiba au jambo kubwa basi wamuombe Allaah awape faraja au alete nusura yake.
Hiyo ndiyo inayoitwa Al-istighaatha ya kisharia ambapo ni kumuomba Allaah peke yake pasipo kumshirikisha na chochote kile kama malaika, mitume au wachamungu.
Kwa hiyo, kumuomba kiumbe jambo ambalo hana uwezo nalo, kama kumuomba Allaah awapatilize waliompiga risasi Lissu kupitia majina ya Ahlul Badri, ni kufanya kitendo cha uzushi katika dini ya Kiislamu na ushirikina wa wazi.
Katika Uislamu, wa kuombwa ni Allaah peke yake kama alivyosema yeye mwenyewe katika Qur’an kwamba: “Na watakapokuuliza waja wangu kuhusu mimi, waambie niko karibu. Ninajibu maombi ya muombaji pale anaponiomba…” (Qur’an Sura ya Pili aya ya 186).
Istighaatha za kisharia ziko za aina kuu mbili, zinazoruhusiwa kisharia na zilizoharamishwa na kwa pamoja zimegawanyika katika aina tatu. Moja ni kuomba msaada kwa mwanadamu aliye hai katika lile ambalo ana uwezo nalo. Mfano ni pale Nabii Musa alipoombwa msaada na ndugu yake Muisraeli dhidi ya adui yake kama ilivyokuja katika Qur’an 28:15. (Na akaingia mjini wakati watu wake wako katika mighafiliko, akakuta humo watu wawili wanapigana; mmoja ni miongoni mwa kundi lake, na mwengine miongoni mwa adui wake. Akamsaidia kumuokoa yule ambaye katika kundi lake dhidi ya yule ambaye ni katika adui wake, Muwsaa akampiga ngumi, akamuua. Akasema: “Hii ni kutokana na kitendo cha shaytwaan. Hakika yeye ni adui mpotoaji bayana.”)
Al-istighaatha nyingine kumuomba Allaah moja kwa moja ambako ndiko kunakohimizwa na Uislamu kama ilivyotajwa katika Qur’ana 8:9. (Na (kumbukeni) pale mlipomuomba uokovu Rabb wenu Naye Akakuitikieni kuwa: “Hakika Mimi Nitakusaidieni kwa Malaika elfu wafuatanao mfululizo.”)
Al-istighaatha nyingine zote ni haramu kama vile kuwaomba viumbe katika jambo ambalo hawana uwezo nao wawe wako hai au wamekufa. Kwa mfano, kwenda kumuomba mtu akuokoe dhidi ya dhulma ulizofanyiwa au kuwaomba waliokufa au watu walioko makaburini.
Istighaatha za aina hii ni aina za ushirikina ambazo Waislamu na wanadamu wengine kwa ujumla kujiepusha nazo. Hizi ni itikadi za kishirikina ambazo zimeingizwa katika Uislamu na hivi leo zinaonekana kama ni mafundisho ya Uislamu wakati ni uzushi tu watu kwa maslahi yao.
Miongoni mwa uzushi ulioenea sana ni hicho kiitwacho Alabadri au Ahlalbadri kiasi kwamba mtu akiaambiwa nitakusomea Albadiri basi huogopa sana na kwa kweli imechukuliwa kama aina za uchawi wa Waislamu wakati huo ni ushirikina wa watu tu na wala sio jambo la kidini.
Nini kinaruhusiwa katika kuomba?
Kinachoruhusiwa ni kumuomba Allaah moja kwa moja au kwa kutaja matendo mema ambayo muombaji ameyafanya katika kumtii Allaah ili kuvuta huruma yake amsaidie au kumuokoa katika shida aliyonayo.
Aina ya kumuomba Allaah kwa kutaja matendo mema aliyoyafanya mwanadamu inaitwa Tawassul. Tawassul inatokana na neno la Kiarabu Al-Wasiyla ambalo lina maana ya njia au nyenzo ya kufanyia jambo. Kwa hiyo matendo mema yanakuwa Wasiyla ya dua ya muombaji anapomuomba Allaah.
Mfano mzuri ni kisa cha watu waliokimbilia katika pango na mlango wa hilo pango ukafunikwa na jiwe kubwa wasiweze kutoka. Hawa wakaona wamuombe Allaah kwa kila mmoja kutaja mema yake aliyokuwa ameyatenda kuvuta huruma zake na kwa rehema zake jiwe likasogea pembeni wakafanikiwa kutoka.
Pengine hii ndiyo iliyochanganywa na watu wenye kusoma hicho kiitwacho kisomo cha Albadiri ambapo hutajwa majina ya maswahaba 313 na kisha kuombwa dua, kwani wanategemeza maombi yao kwa Allaah kupitia hao Ahlul Badri ambao kama tulivyoona ni maswahaba au wanafunzi wa Mtume Muhammad waliopigana vita vya Badri.
Nasaha kwa Waislamu
Tunapenda kutoa nasaha kwa Waislamu wote kwamba wasijihusishe na hicho kinachoitwa kisomo cha Albadiri kuwasomea waliompiga risasi Lissu. Kufanya hivyo hakuwatoi katika wale wenye kumuonea huruma Lissu, bali kunawatoa katika kufanya kitendo cha kumshirikisha Allaah.
Ikiwa ni kumuombea, wafanye hivyo kwa namna inayokubalika katika dini ya Uislamu na siyo njia hii ambayo Mtume wa Allaah hakuifundisha.
Allaah anasema katika Qur’an 5:35 kwamba: “Enyi mlioamini, muogopeni Allaah na tafuteni Wasiyla (kwenda kwake) na fanyeni juhudi katika nia yake ili mpate kufaulu”.
Kingine ni kwamba Waislamu wanapaswa kujiepuesha na mwenendo wa kulaani. Likitokea jambo baadhi kukimbilia kulaani. Tunapaswa kukumbuka kwamba Mtume wetu alitumwa kuwa rehema kwa walimwengu.
Allaah anasema katika Qur’an 21:107 kwamba: “Na hatukukutuma (ewe Muhammad) isipokuwa uwe rehma kwa walimwengu”.
Ndiyo maana Mtume watu alipoombwa na mtu mmoja: “Ewe Mjumbe wa Allah walaani washirikina. Akasema “Hakika Allah hakunituma kuwa mwenye kulaumu wala kulaani, lakini amenituma kuwa mlinganiaji na rehma”.
Waislamu humuomba Mola wao tu na ikibidi kuwaombea watu waovu dua, Waislamu wema huwaombea watu waovu Allaah awaongoe kwani wanafanya uovu au dhulma wanazozifanya kwa kutomjua Allaah hivyo mwisho wa dhulma ni wao kuongoka.
Ikibidi kuomba dua dhidi ya uovu au dhulma zinazofanyiwa Waislamu na watu wengine kwa ujumla, kinachotakiwa ni kumuiga Mtume Muhammad pindi alipoomba dhidi ya wakuu wa Makureshi kwa kusema “Ewe Mola wangu, nakukabidhi fulani …”.
Fundisho hapa ni kwamba Mtume hakupata kumuombea mtu yeyote mabaya bali alimuomba Allaah amfanye mtu huyo kile ambacho yeye anaona kinafaa. 
Imeandaliwa na Sheikh Muhammad Issa ni Naibu Katibu Mkuu Baraza la Sunnah Tanzania (Basuta). baadhi ya marekebisho yamefanya na Muislamu.Com

0 Comments