November 9, 2017

ASBAABUN-NUZUUL (Sababu Ya Kuteremshwa) MU'AWWIDHATAAN

Al-Mu’awidhataan ambayo ni ‘Qul-A'uudhu bi Rabbil-Falaq Na Qul-A'uudhu Birabbin-Naas’

Wafasiri wa Qur-aan wamesema kwamba kijana wa kiyahudi alikuwa akimhudumia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaja Myahudi na kumlaghai kijana huyo hadi akachukua kitana cha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumpa huyo Myahudi baadhi ya meno ya kitana hicho na kukitumia kumlogea Mtume.


Aliyefanya uchawi huo ni Myahudi aliyeitwa Labiyd bin Al-A'swam ambaye alikitumbukiza katika kisima cha watu wa Zurayq kilichoitwa 'Dharwaan'. Akaumwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), zikanyonyoka nywele zake (ukapita muda wa miezi sita) akihisi kuwa anaonana na wake zake (kwa kujimai) lakini kumbe hajimai nao. Akaanza kugeuka bila ya kutambua yaliyomuathiri.

Siku moja alipokuwa amelala, walimjia Malaika wawili; mmoja akaketi mbele ya kichwa chake, na mwengine miguuni mwake. Akauliza aliyeketi kichwani mwake: "Mtu huyu ana nini?" Malaika mwengine akajibu: "Twubb" Akauliza: "Ni nini hiyo 'Twubb?" Akasema: "Amerogwa" Akauliza: "Nani aliyemroga?" Akasema: "Labiyd bin Al-A'swam Myahudi". Akauliza: "Amemroga kwa nini?" Akasema: "Kitana na nywele".  Akauliza: "Viko wapi? Akasema: Katika ganda la mtende na jiwe chini ya kisima cha Dharwaan.

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akatanabahi ugonjwa wake akasema: ((Ewe 'Aaishah! Nimehisi kwamba Allaah Amenijulisha ugonjwa wangu)). Kisha akamtuma 'Aliy na Az-Zubayr na 'Ammaar bin Yaasir, wamwage maji yote ya kisima, wakamate jiwe na kutoa ganda la mtende na meno ya kitana yaliyofungwa mafundo kumi pamaoja na sindano. Hivyo Allaah Akateremsha Surah mbili Akajaaliwa kila akisoma Aayah fundo moja lilifunguka hadi mafundo yote yakafunguka akarudisha siha yake. Kisha Jbiryl ('Alayhis-Salaam) akasema: "Bismillaahi Arqiyka, Min Kulli shay-in yuudhiyk, wa min haasidin wa 'Aynu-LLaahi Yashifyka" (Kwa jina la Allaah, Nakukinga na kila jambo linalokuletea adha, na kila hasidi na Jicho la Allaah Likuponyeshe??).Wakasema: "Ewe Mjumbe wa Allaah, Je tuwaue makhabithi? Akajibu: ((Kwa vile Allaah Amenipa shifaa, nachukia kuwadhuru watu)) [Huu ni upole wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)]

Ikhtiliaaf za rai zimepatikana kutoka kwa Ma'ulamaa mbali mbali kuhusu sababu ya kuteremeshwa Surah hizi. Kuna wanaopinga sababu hiyo ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kurogwa, na kuna wanounga mkono. Sababu mbali mbali zimetolewa, tutanukuu hapa rai na hoja za pande hizo.

Wanaopinga wanasema:


Kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Hawezi kumfanya Mjumbe Wake alogwe kwa vile yeye ni kigezo cha mfano mzuri wa maisha ya Kiislamu, na pia inapingana na Qur-aan.


Wanaounga mkono wanajibu:

Wamekanusha hivyo kwani wanaona kwamba mas-ala ya uchawi na kuathirika imewasibu Mitume mingine kama Nabii Muusa ('Alayhis-Salaam) kama tunavyoona kwenye Surah Al-A’araaf na Surat Twaahaa.

Wanaona kwamba ni tukio la hakika ambalo limethibiti kwa Hadiyth sahihi, na kulikanusha itakuwa ni kukanusha Hadiyth nyingi zinazotoa mafunzo ya du'aa mbali mbali za kujikinga na shari, wasiwasi, majini, maradhi, mfano du'aa unapoingia kulala kusoma Suratul-Ikhlaasw na Al-Mu‘awwidhataan huku unapuliza katika viganja vya mikono na kujipangusa mwilini. Hali kadhaalika unapoumwa. Vile vile Hadiyth iliyotaja watu sabini alfu watakaoingia Peponi wakiwa miongoni mwao ni wale ambao wanapoumwa au wanapofikwa na madhara yoyote hawatafuti tiba ila kuwa na Tawakkul na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala).  [Muslim]


Na riwaya hiyo ya kulogwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) imepokewa na wapokezi wengi wa kuaminika hivyo haina mashaka yoyote. Waliopekea ni Al-Bukhaariy, Muslim, an-Nasaaiy, Ibn Maajah, Imaam Ahmad, Abdur-Razzaq, Humaydiy, al-Bayhaqiy, atw-Twabaraaniy, Ibn Sa’d, Ibn Mardayah, Ibn Abi Shaybah, al-Haakim, Abd bin Humayd na wasimulizi wengi kutoka kwa mama wa waumini ‘Aaishah, Zayd bin Arqam na Abdullaah bin ‘Abbaas.

Ama madai ya wanaoipinga Hadiyth hii miongoni mwa Waislam, kama ambavyo wasio Waislam wanaitumia kutaka kumfanyia istihzai na kudhalilisha Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kusema kama anarogeka basi hata atakayosema yatakuwa ni maneno ya aliyelogwa na hivyo si wahyi tena! Na kama yatakuwa si wahyi, basi iweje Mola wake aruhusu hilo?

Jibu la madai kama hayo ya kiakili tu bila ushahidi, ni kuwa, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yeye kama Mtume, hakuna mabadiliko yoyote yaliyotokea kwake alipologwa kwa upande wa utekelezaji wake wa majukumu na wajibu wake kama Mtume. Hakuna mapokezi yoyote yaliyoeleza kuwa labda kwa kulogeka kwake, basi alisahau Aayah za Qur-aan au kuzigeuza au kuzikosea n.k. katika hayo masiku aliyodhurika na uchawi. Wala hakuna popote panaposemwa kuwa labda alikuwa akipayuka katika Khutbah zake, au kutoa maelezo ya wahyi ambayo hakushushiwa au japo kusahau kuswali na huku akidhani keshaswali…au mengi ya mfano wa hayo. Na kama yangetokea hayo au mfano wake, basi yasingefichikana na bara Arabu zima lingejua hilo au angalau Madiynah na Makkah wangepata habari hizo, lakini hakukutokezea lolote. Kwani pamoja na kupewa mitihani hiyo na Mola wake, kama ambavyo Mitume wengine walivyopata mitihani mbalimbali, haikuwa na maana zaidi ya kupewa majaribio na pia kuwe ni mafunzo kwetu sisi Ummah wake. Na vilevile tupate kujua namna ya kujitibu kwa kutumia Mu‘awwidhatayn kama ambavyo alivyofundishwa yeye Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Jibriyl (‘Alayhis Salaam); mafunzo yaliyotoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).

Tukio hili kwa wale wenye Iymaan thaabit na wenye kukubaliana na mapokezi yaliyothibiti na ambao hawatangulizi akili zao mbele ya nuswuus zilizo sahihi, ni tukio sawa sawa na matukio mbalimbali yaliyowahi kumpata Mtume na ambayo yamesimuliwa katika Hadiyth mbalimbali sahihi na hata hao wenye kupinga la kulogwa Mtume nao wamekubali hizo riwaya zingine za kudhurika Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mfano wa hizo, ni kama alivyojeruhiwa na kuumizwa vibaya katika vita vya Uhud, au alivyoshambuliwa kwa mawe kule Twaaif, au alivyodungwa na ng’e, au kupewa sumu katika nyama na kuila, na mengine ambayo yamethibiti usahihi wa mapokezi yake kwenye vitabu vya kuaminika. Iweje wakubali baadhi na wakatae baadhi!! Bila shaka ni kuchezewa na akili zao zenye mipaka.

Hapa tutakuwa tumejua sababu ya kuteremshwa Surah hizo; al-Falaq na an-Naas au maarufu kama Al-Mu‘awwidhataan.

Na Allaah Anajua zaidi

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only