November 28, 2017

MADHARA YA KUFUATA MATAMANIO

Shukurani zote Anastahiki Allaah, Mola wa ulimwengu wote. Rehma na amani zimshukie Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ahli zake na Masahaba wake.
Enyi Waislamu muogopeni Allaah kwa kadri Anavyopaswa kuogopewa. Allaah Amesema,
“Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu kama ipasavyo kumcha; wala msife ila nanyi ni Waislamu.” (Aal 'Imraan 3:102)
Ucha Mungu ni dalili ya Iymaan. Kwani kwa ucha Mungu ndipo mtu anaweza kudumu katika njia iliyonyooka (iliyo sawa)
Jueni kuwa muongozo sahihi ni muongozo wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Ubaya wa mambo yote ni uzushi, na kila uzushi ni uovu, na kila ovu linampeleka mtu motoni.
Enyi Waislamu! Allaah Amewaumba viumbe ili wamuabudu na wafungamane na Amri Zake na makatazo Yake. Allaah Anasema,
"Nami Sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi." (Adh-Dhaariyaat 51:56)
 
Allaah pia Anasema,
"Enyi watu! Muabuduni Mola wenu Mlezi Aliyekuumbeni nyinyi na wale wa kabla yenu, ili mpate kuokoka." (Al-Baqarah 2:21)

Mitume (‘Alayhimus Salaam) hawakutumwa, wala Vitabu havikuteremshwa, wala Pepo na Moto havikuumbwa ila kwa ukweli huu mtukufu, wa kuwatoa watu kutoka kuabudu matamanio yao na kuwaleta katika kumuabudu Muumba wao Peke Yake. Wametakiwa kuamini upwekwe Wake, kutekeleza amri Zake na kujiepusha na makatazo Yake katika vipengele vyote vya maisha. Wameamrishwa pia kurejea katika sharia Zake katika mambo yote na kujisalimisha katika maamuzi Yake katika hali zote. Vitabu vya Allaah na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa pamoja vinakusudia lengo hili, ili mtu aweze kufanya matendo yale tu yanayomridhia Allaah. Iwapo mtu atakwenda kinyume na lengo hili, anatahadharishwa na adhabu  hapa duniani na kesho Akhera. Allaah Anasema, 

“Jueni kuwa hakika ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na ardhini. Hakika Yeye Anajua mlio nayo. Na siku mtaporudishwa Kwake Atawaeleza waliyoyafanya. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.”
 (An-Nuur 24:63)
Ndugu katika iymaan! Msingi wa kumuasi Allaah ni kufuata matamanio na kujisalimisha na matamanio ya kupita na starehe za muda. Allaah Anahesabu kufuata matamanio kuwa ni kinyume cha uongofu. Anasema,

”Je! Tuwafanye walioamini na wakatenda mema kama wafanyao uharibifu katika nchi? Au Tuwafanye wacha Mungu kama waovu?.”
 (Swaad 38:28)
 
Na Akasema, 
"Basi ama yule aliye zidi ujeuri"
"Na akakhiari maisha ya dunia"

”Kwa hakika Jahannamu ndiyo makaazi yake!
 
"Na ama yule anayeogopa kusimamishwa mbele ya Mola wake Mlezi, na akajizuilia nafsi yake na matamanio" 
"Basi huyo, Pepo itakuwa ndiyo makaazi yake!”
(An-Naazi’aat 79:37-41)

Allaah pia Anasema kuhusu Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), 
"Wala hatamki kwa matamanio. Hayakuwa haya ila ni ufunuo uliofunuliwa" (An-Najm 53:3-4)
Inajulikana kutokana na uzoefu na ushahidi wa maandishi kuwa faida za dunia hii na zile za Akhera haziwezi kupatikana kwa kufuata matamanio na kujisalimisha na shauku bila kizuizi chochote. Kufanya hivyo kunapelekea machafuko (Shari’ah mkononi), mauaji, vita na maangamizi.

Enyi Waislam! Hakuwezi kuwa na Uislamu wa kweli iwapo akili hazitojisalimisha na kukubalikikamilifu matakwa ya Allaah. Na Allaah Anasema,

"Sema: Hakika Sala yangu, na ibada zangu, na uhai wangu, na kufa kwangu, ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote. Hana mshirika wake. Na hayo ndiyo niliyoamrishwa, na mimi ni wa kwanza wa Waislamu." (Al-An'aam 6:162-163)

Asili ya Uislam ni kujisalimisha kwa Allaah kwa utii, ina maana kusiwe na mashaka yoyote na kukubali kwa kuridhia maamuzi Yake na amri Zake katika vipengele vyote vya maisha. Huu ndio msingi wa Uislam. Yeyote atakaepinga sharia za Allaah kwa maoni yake hakujisalimisha kwa Allaah. Yeye ni mtumwa tu wa matamanio yake, na yeye ndie yule aliyetajwa kwa maneno ya Allaah,

”Je! Umemwona aliyefanya matamanio yake kuwa ndiye Mungu wake, na Mwenyezi Mungu Akamwacha apotee pamoja na kuwa ana ujuzi, na akapiga muhuri juu ya masikio yake, na moyo wake, na Akambandika vitanga machoni mwake? Basi nani atamwongoa huyo baada ya Mwenyezi Mungu? Hamkumbuki?” (Al-Jaathiyah 45:23)
Allaah pia Anasema,

"Na ikiwa hawakuitikii, basi jua kuwa wanafuata pumbao lao tu. Na nani aliye potea zaidi kumshinda anayefuata pumbao lakebila ya uwongofu utokao kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu Hawaongoi watu wenye kudhulumu."
 (Al-Qasas 28:50)
Kujisalimisha katika matakwa ya Allaah katika mambo yote si msingi tu wa Uislam; bali pia ni sharti la iymaan ya kweli. Allaah Anasema,

"La! Naapa kwa Mola wako Mlezi! Hawataamini mpaka wakufanye wewe ndiye muamuzi katika yale wanayo khitalifiana, kisha wasione uzito katika nyoyo zao juu ya hukumu utayotoa, na wanyenyekee kabisa." (An-Nisaa 4:65)
Katika Hadiyth, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema, “Hatoamini mmoja wenu hadi yawe matamanio yake ni yale niliyokuja nayo”        

Enyi Waislam! Ingawa sharia za Kiislam na kanuni zake zinawafikiana na mahitaji ya binaadamu, shari'ah hizi hazitegemei shauku na matamanio ya binaadamu. Allaah anasema,

"Na lau kuwa Haki ingelifuata matamanio yao, basi zingeli haribika mbingu na ardhi na waliomo ndani. Bali tumewaletea ukumbusho wao, nao wanajitenga mbali na ukumbusho wao." (Al-Mu-minuun 23:71)
Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyyah anasema,
“Ni Kitabu tu kutoka mbinguni kinachoweza kutatua matatizo ya watu. Lau kama watu wangeachwa kufuata rai zao, basi kila mmoja kati yao bila shaka angekuwa na rai”
Ndugu wapenzi! Muislamu anaweza kuwa dhaifu, akampa shetani fursa ya kumlazimisha kufanya madhambi. Iwapo atatubia kutokana na madhambi hayo, Allaah Atamkubalia toba yake; lakini iwapo atakufa kabla ya kutubia Allaah Anaweza Akampa adhabu Akitaka au Akamsamehe Akitaka. Hii ni hali ya watu karibu wote. Wana Adam wote ni wafanya madhambi na waliobora katika wafanya madhambi ni wale wenye kutubia.

Mtu wa kulaumiwa anayestahiki tishio la adhabu ni yule mwenye majivuno, anayejadili kwa kukubaliana na madhambi na matamanio yake, anayepinga makatazo ya Allaah kwa maoni yake, anakusudia  kuudhalilisha Uislam, anapiga vita akhlaaq zote zinazokwenda kinyume na  matamanio yake na kukubaliana na mambo yote yanayopendzesha matamanio yake tu. Mtu huyu anafuata njia za wanafilosofia wa zamani kwa kukubaliana na anayoyataka na asiyoyataka tu katika matamanio yake mpaka akapotea katika giza la starehe na makosa, kama chombo kilichochanganyikiwahakitambui kipi kilicho kizuri au kukataa kilicho kibaya.
Shaykhul-Islaam ibn Taymiyyah amesema,
“Kufuata matamanio katika masuala ya dini ni kubaya zaidi kuliko kufuata mambo mengine ya starehe  Hiyo ya mwanzo ilikuwa ndio hali ya wasioamini miongoni mwa washirikina. Hawa ndio wale waliokusudiwa na maneno ya Mtume katika hadiyth iliyosimuliwa na Hudhayfah, “Kutakuwa na watu katika milango ya moto watakaowaita watu kuingia humo. Atakayeitikia wito wao, basi watamtupa kwenye moto. Nikasema, “Ee Mtume wa Allaah, tujulishe kuhusu watu hao. Akasema: Sawa. Hao ni watu katika sisi na wanaozungumza lugha yetu.”
Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pia amesema, “Watu watazuka kutoka katika umma wangu ambao watakuwa wamejaa matamanio kama ugonjwa wa kuambukizwa na mnyama unavyozagaa mwili mzima na kuathiri mishipa na viungo  vyote” Abu Dawuud

Ash-Shaatwibiy amesema,
“Kile wanachofanya ni kuwa wanafuata hukumu za akili zao tu na kushirikisha hayo na Shari’ah za Allaah katika kukubaliana au kutokubaliana na jambo. Iwapo wangesita hapo, mambo yangekuwa ni mepesi zaidi bali wamekiuka mipaka yote mpaka wakatangaza vita dhidi ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kukipinga kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume Wake.”
Enyi Waislamu! Hakuna nafasi kwa akili ya  mtu binafsi mbele ya ushahidi wa maandiko, na kunatakiwa kusiangaliwe mawazo ya yeyote mbele ya maamuzi ya Allaah na yale ya Mtume Wake. Allaah anasema,

"Haiwi kwa Muumini mwanamume wala Muumini mwanamke kuwa na khiari katika jambo, Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapo kata shauri katika jambo lao. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake basi hakika amepotea upotofu ulio wazi."
 (Al-Ahzaab 33:36)

Kuonyesha kuchukizwa na Shari’ah ya Allaah na kutafuta Shari’ah nyingine kinyume na Zake kunafisidi amali. Allaah Anasema,

"Hayo ni kwa sababu waliyachukia Aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, basi Akaviangusha vitendo vyao." (Muhammad 47:9)

Ibn Rajab anasema,
“Madhambi yanafanywa kwa sababu ya kupendelea matamanio zaidi kuliko mapenzi ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Uzushi katika dini ni matokeo ya kupendelea matamanio zaidi kuliko Shari’ah za Allaah, na hii ni hatari zaidi. Iwapo akili imeshazoeshwa matamanio, kuitoa akili hiyo nje ya matamanio ni kugumu"

Ndugu katika Iymaan! Allaah Ameumba mipaka katika  uwezo wa akili ya binaadamu. Haiwezekani kwa akili ya binaandamu kufahamu kila kitu kwa usahihi wake. Ujuzi wa kila kitu ni sifa maalumu  ya Allaah Peke Yake. Ufahamu wa binaadamu una kasoro na (binaadam) hawawezi kukubaliana na nadharia yoyote. Ndio sababu ukawaona wanaanza kufuata mawazo/rai fulani leo na wanaachana nayo kesho na kufuata mtazamo mwengine, na kesho kutwa wanahamia katika rai nyingine tofauti. Iwapo kila maamuzi yanayochukuliwa kwa akili za binaadamu ni sahihi kungekuwa na uhakika wa kutosha wa maisha mazuri ya watu wote katika dunia yao na Akhera yao, kusingekuwa na haja ya kutumwa Mitume na kusingekuwa na haja ya ujumbe mtukufu.
Imekuwa kwa hivyo ni lazima kwa Muislam kuwa macho katika kufuata njia ya hatari yenye makosa  ya kukataa sehemu yoyote ya maamrisho ya Allaah na kuchukizwa nayo au kupendelea zaidi matamanio na kujadili juu ya Shari’ah (Ya Allaah). Wafuasi wa Sunnah wamekubaliana ya kuwa yeyote anayefanya mambo yaliyokatazwa ambayo yako chini ya ushirikina, basi mtu huyo atachukuliwa kuwa hakuamini; na yeyote ataeyachukulia mambo yaliyokatazwa kuwa yanafaa – hata kama hayafanyi- mtu huyo hakuamini, iwapo mambo hayo yanaangukia katika mambo ambayo ni lazima yajulikane katika dini.

Waache wale wanaotafuta uongofu wasome maneno ya Allaah kwamba,
"Na kwa hakika hii ndiyo Njia yangu Iliyo Nyooka. Basi ifuateni, wala msifuate njia nyingine, zikakutengeni na Njia yake. Haya amekuusieni ili mpate kumcha Mungu." (Al-An'aam 6:153)
Enyi Waislamu! Mazingatio yamesifiwa kwa binaadamu. Kama si hivyo, kusingekuwa ni wajibu ulioamrishwa maalum juu ya binaadam. Allaah Ameelezea mazingatio ya binaadamu katika aya nyingi katika Kitabu Chake. Amemuamrisha binaadamu kufikiri na kufahamu. Yeye pia amefahamisha sababu mbali mbali katika Amri Zake nyingi Anamalizia kwa Kusema, “ Ili mpate kufahamu”.      
Ingawa ni Allaah Mwenyewe Aliyeumba ufahamu kwa binaadamu, Amewafanya tofauti baina mmoja na mwengine. Ameumba hisia na matamanio ya kimaumbile ya binaadamu lakini Akaifanya Sharia iwe ni hakimu wa yote hayo, Yeye (Allaah) Anaweza kumuweka mtu katika mtihani. Yule atakayejisalimisha kwa Allaah peke yake ndie Muislam wa kweli ambaye anamtii Allaah na kwa hivyo, anastahiki Pepo. Lakini yule anayejivuna na akatumia akili na kuasi amri za Allaah, yeye ameahidiwa adhabu.
Wanachuoni wametaja tabia za watu wa matamanio na wale waliopendelea zaidi maoni yao juu ya Shari’ah sahihi za Kiislam na amri zake. Kuwa tabia hizi zilikuwepo kwa watu wa matamanio wa umma za mwamzo, na vile vile zipo kwa ummah wa mwisho.  Moja ya tabia hizi ni kufuata aya zisizo wazi (mutashaabihaati) katika Qur’aan. Allaah Anasema,
"Yeye ndiye Aliyekuteremshia Kitabu hichi. Ndani yake zimo Aya muhkam, zenye maana wazi. Hizo ndizo msingi wa Kitabu hichi. Na ziko nyengine za mifano. Ama wale ambao nyoyoni mwao umo upotovu wanafuata zile za mifano kwa kutafuta fitna, na kutafuta maana yake; na wala hapana ajuaye maana yake ila Mwenyezi Mungu. Na wale wenye msingi madhubuti katika ilimu husema: Sisi tumeziamini, zote zimetoka kwa Mola wetu Mlezi. Lakini hawakumbuki hayo isipokuwa wenye akili." (Aal 'Imraan 3:7)                                                                     
Tabia nyingine ya watu hawa ni kuwa wanawatukana Waislam wa mwanzo, kama Masahaba ambao wanajulikana (ni maarufu) kwa elimu yao na ucha Mungu wao na wameigwa na wale waliokuja baada yao. Watu wa matamanio wanawasifu wale wanaokubaliana na shauku zao kamawanafalsafa.

Watu wa matamanio pia wanajulikana kwa kudharau amri za Uislam na kutojali kwao katika kuzipinga. Baadhi yao hata wamefikia kiwango cha kuzifanyia mzaha amri hizi na kuwafanyia mzaha wale waliofungamana na amri hizo na kuwatoa makosa na kuwalaumu.
Tabia nyingine ya watu wa matamanio ni kuwa wao hawafuati Sunnah katika matendo yao ya ibada, desturi zao na hali zao. Pamoja na hayo, utamuona mmoja wao akijifananisha na wanachuoni watukufu/maarufu wa Sunnah. Wao ni kama wale Allaah Aliowaeleza katika Qur’aan kama,

"Na katika watu wapo wanao bishana juu ya Mwenyezi Mungu bila ya ilimu, wala uongofu, wala Kitabu chenye nuru. Anayegeuza shingo yake ili kupoteza watu waache Njia ya Mwenyezi Mungu. Duniani atapata hizaya, na Siku ya Qiyaama Tutamwonjesha adhabu ya kuungua. (Ataambiwa): Hayo ni kwa sababu ya iliyo tanguliza mikono yako. Na hakika Mwenyezi Mungu si dhaalimu kwa waja.” (Al-Hajj 22:8-10)
                                                                                     

Ya Allaah! Zithibitishe nyoyo zetu katika dini na uwaongoze wale Waislamu waliokwenda upande.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only