April 1, 2018

072-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Mwenye Kukosa Vitwaharisho Viwili (Maji Na Mchanga)

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

Mlango Wa Twahara

072-Mwenye Kukosa Vitwaharisho Viwili (Maji Na Mchanga)


Kauli sahihi zaidi kati ya kauli mbili za Maulamaa kuhusiana na mtu aliyekosa vitwaharisho viwili (maji na mchanga) ni kuwa ataswali katika hali aliyonayo katika wakati wa Swalaah na wala hatoirejesha.

Huu ni mwelekeo wa Ash-Shaafi’iy, Ahmad na Ibn Hazm. Ibn Taymiyyah ameukhitari mwelekeo huu. [Al-Mughniy (1/157), Al-Majmu’u (2/321), Al-Muhallaa (2/138) na Al-Fataawaa (21/467)]

Hoja yao ni Kauli Yake Allaah Mtukufu:
((فاتقوا الله مااستطعتم))
((Basi mcheni Allaah mwezavyo)) [At- Taghaabun ( 64:16]

Na Neno Lake Allaah Mtukufu:
((لا يكلف الله نفسا إلا وسعها))
((Allaah Haikalifishi nafsi yoyote ila kwa uwezo wake)) [Al-Baqarah (2:286)]

Na kauli yake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((إذا أمرتكم بأمر فائتوا منه مااستطعتم))
((Nikiwaamuruni jambo, basi lifanyeni kwa uwezo wenu)) [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (7288) na Muslim (3199)].

Wamesema: “Huyu amefanya alichoweza katika Swalaah, na jambo la kujitwaharisha ambalo hakuliweza, limemwondokea. Na kwa hilo, anakuwa ametekeleza aliloamuriwa, na mwenye kutekeleza aliloamuriwa, basi hatolipa”.

Ninasema: “Na huenda mwelekeo huu unatiliwa nguvu na Hadiyth ya Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha) aliyesema:
“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimtuma Asyad bin Al-Khudhayr – na hali mimi nasikia – kukitafuta kidani nilichokipoteza. Ukafika wakati wa Swalaah, nao wakaswali bila wudhuu. Kisha wakamjia Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakamweleza hilo, na hapo ikateremshwa Aayah ya tayammum”[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (5882) na Muslim (795)].

Na ushahidi hapa ni kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwakubalia – wakati walipokosa maji – kuswali bila wudhuu na wala hakuwaamuru kurejesha Swalaah. Na endapo kama watakosa mchanga vile vile, basi hukmu ni hiyo hiyo. Na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

Na kwa upande mwengine, Abuu Haniyfah, Asw-haabur Ra-ay (Mahanafi), Maalik na Al-Awzaa’iy, wao wanaona kwamba hatoswali mtu mpaka apate maji ya kutawadhia au mchanga wa kutayamamia, hata kama wakati utatoka. [Al-Awsatw (2/45), Al-Istidhkaar (3/150) na Al-Muhallaa (2/139)]

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only