April 13, 2018

KULALA NA JANABA NA KUAMKA NA SWAWM

SWALI: 
asalam aleikum
swala langu ni ikiwa mtu amelala na janaba siku ya ramadhan  akamka asubuhi  je saum ina swih ama itakuwa haifaiJIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Asli katika mas-ala ni kuwa Swawm ya mtu mume au mke haibatiliki kama ataamka wakati wa Alfajiri na janaba iwe janaba kwa sababu ya kulala na ahli yake au kwa kutoa kama ilivyothibiti katika Hadiyth kutoka kwa Mama wa Waumini ‘Aaishah na Mama wa Waumini Ummu Salamah (Radhiya Allaahu ‘anhumaa) wamesema:
“Kwa hakika Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa ’ala aalihi wa sallam) alikuwa inamdiriki Alfajiri hali ya kuwa na janaba kutokana ahli zake, kisha hukoga na kufunga” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, Kitaab cha Swawm, mlango mwenye kufunga na kuamka na janaba].

Ingawa pamoja na kanuni ya ki-Uswuwl inayothibitisha kuwa kauli ya Mtume hutangulizwa kuliko kitendo chake; yaani kauli yake ndiyo hufanyiwa kazi endapo itagongana na kitendo alichofanya yeye, na kwa sababu kuna Hadiyth kutoka kwa Abu Hurayrah anayosema kuwa alisikia kuwa mwenye kuamka na janaba hana Swawm, lakini kama anavyoeleza Imaam An-Nawawiy katika sharh ya Swahiyh Muslim, kuwa Abu Hurayrah alipofikishiwa maelezo ya wake za Mtume na 'Abdur-Rahmaan bin Haarith kuthibitisha kwao kuwa Mtume aliamka na janaba na akajitwaharisha na kuendelea kufunga, Abu Hurayrah akajibu kuwa wao (wake za Mtume) ni Wajuzi zaidi, na akarejea na kauli yake na kuwafikiana na kauli za wake za Mtume. Imaam An-Nawawiy anasema kwa kuzilinganisha Ahaadiyth hizo zote, kuwa iliyo sahihi ni kuwa Swawm ya mwenye kuamka na janaba ni sahihi kabisa. Msimamo huu vilevile ndio wamekubaliana Wanachuoni wengi. Imaam Muslim katika Swahiyh yake, kaweka mlango unaohusu Ahaadiyth hizo, na kuuita, باب صحة صوم من طلع عليه الفجر وهو جنب "Mlango wa kusihi Swawm kwa iliyomchomozea Alfajiri akiwa na janaba", kuthibitisha naye kuwa Swawm ya mwenye kuamka na janaba ni sahihi.

Hivyo basi hukumu ni kuwa Swawm haijabatilika, bali ipo na inaendelea kwa kila atakayelala usiku na kuamka na janaba, na mwenye kulala mchana na kuota ndoto ya utu uzima, awe mwanamume au mwanamke.

Kitachomlazimu ni kukoga josho pindi aamkapo na kuendelea na Swawm yake na hana kulipa wala fidia kwani hana kosa lolote.

Na Allaah Anajua zaidi

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only