April 5, 2018

NJIA KUMI ZA KUHIFADHI QUR-AAN - 1

Imekusanywa na Ukht Haliymah ‘Abdullaah

Kutoka kitabu:

كيف تحفظ القرآن في عشر خطوات – حسن أحمد بن أحمد همامHaifichiki kwa kila Muislam ubora wa kuhifadhi Qur-aan Tukufu na fadhla za aliyeihifadhi.

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

“Wale tuliowapa kitabu (Taurati, injili, Zaburi…) wakakisoma kama ipasavyo kukisoma (bila ya kupotoa tafsiri yake wala kutoa hili na kutia lile), hao huiamini hii (Qur-aan wakasilimu). Na wanaokikanusha (hicho kitabu chao wakapinduapindua tafsiri yake na wakaongeza na wakapunguza), basi hao ndio wenye hasara.” Al-Baqarah: 121.

“Kisha Tumewarithisha, (tumewapa) kitabu (hiki cha Qur-aan) wale Tuliowachagua miongoni mwao wanaodhulumu nafsi zao (kwa kuwa na maasia mengi kuliko mema). Na wako wa kati na kati, (wana mema kuliko mema). Na wako wanaokwenda mbele kabisa katika mambo ya kheri, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo fadhila kubwa.” Faatwir: 32.

“Kwa yakini wale wanaosoma kitabu cha Mwenyezi Mungu, na wakasimamisha Swalah, na katika yale Tuliyowapa wakatoa, kwa siri na kwa dhahiri, hao wanatumai (faida ya) biashara isiyododa (isiyobaga).” Faatwir: 29.

Katika hizi Aayah ni dalili ya ubora ya watu wa Qur-aan na kufaulu biashara yao na Allaah.
Ama Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam) ni nyingi tunachukua zifuatazo:

kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema, amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam):

“Hakuna hasadi ila katika vitu viwili; mtu ambaye Allaah Amempa hekima (elimu) anaisimamia usiku na mchana, na mtu ambaye Allaah Amempa mali naye anatoa sadaka usiku na mchana.”Muslim

Kutoka kwa ‘Uthmaan bin ‘Afaan (Radhiya Allaahu ‘anhu) anasema, anasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam):

“Mbora wenu ni aliyejifunza Qur-aan na akaifundisha.” Al-Bukhaariy

Kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amru bin Al-‘Aas (Radhiya Allaahu ‘anhu) kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam) amesema:

“Ataambiwa Swaahib al-Qur-aan soma kama ulivyokuwa ukisoma duniani hakika daraja yako peponi ni mwisho wa Aayah utakayosoma.” At-Tirmidhiy

Kutoka kwa Sahl bin Mu’adh kutoka kwa baba yake kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam) amesema:

“Mwenye kusoma Qur-aan na akaifanyia kazi yaliyomo atavalishwa mzazi wake taji siku ya kiyama mng’aro wake ni bora kuliko mwangaza wa jua katika nyumba za dunia lau ingekuwa kwenu mnadhani vipi kwa aliyeifanyia kazi.” Abu Daawuud

Imepokewa katika Al-Bukhaariy kwamba walikuwa wanatangulizwa watu wa Qur-aan (Ahlul Qur-aan) kuliko wengine katika Swallah na katika kuwazika mashahidi. Pia kuna mtu alimuoa mwanamke kwa Qur-aan aliyokuwa nayo kama mahari.


KUHIFADHI QUR-AAN NI KHASWA KWA UMMAH HUU

Allaah Amejaalia Ummah huu kuwa bora kuliko Ummah zingine na Akajaalia wepesi kuhifadhi Kitabu hiki kimaandishi na kifuani.

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

“Bali hizi ni Aayah waziwazi (zinazokubaliwa) katika vifua vya wale waliopewa ilimu, na hawazikatai Aayah Zetu isipokuwa madhalimu (wa nafsi zao).” Al-‘Ankabuut: 49

Na imekuja katika Hadiyth al-Qudsiy;

“Na imeteremshwa kwako Kitabu kisichooshwa na maji unasoma ukiwa umelala na ukiwa macho.”Muslim


WEPESI WA KUHIFADHI QUR-AAN

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

“Na kwa yakini Tumeifanya Qur-aan iwe nyepesi kufahamika (ili iwe kikumbusho). Lakini yuko anayekumbuka?” Al-Qamar: 17

Yaani tumemfanyia wepesi katika kuhifadhi je yupo anayeelekea akatafuta kuhifadhi akasaidiwa - Tafsiyr Al-Qurtubiy

Mtoto mdogo chini ya miaka kumi ameweza kuhifadhi Qur-aan yote pia asiyejua Lugha ya Kiarabu ameweza kuhifadhi na haya yashatokea.


KUHIFADHI QUR-AAN HAINA UMRI MAALUM

Wanadhani watu wengi kwamba kuhifadhi Qur-aan ina wakati maalum katika maisha ya mwanaadamu nayo ni kipindi cha udogoni wanarudiarudia methali mashuhuri “kuhifadhi udogoni ni kama nakshi katika jiwe” na wanatolea dalili pia kwamba kipindi cha ukubwa inashughulika akili kwa mambo ya kimaisha.
Maneno haya yanahitaji yatizamwe upya, ni kweli kuhifadhi udogoni ina faida zake lakini haiishii hapo, mwanaadamu Akiwezeshwa na Allaah akajitahidi na kufanya subra anaweza kwa uwezo wa Allaah kulifikia hilo hata katika umri mkubwa.

Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) ilikuwa Qur-aan inawashukia wakaihifadhi vifuani mwao na hawakuwa katika umri wa utoto mfano Makhalifa wanne, Ubay bin Ka’ab, Zayd bin Thaabit, Ibn Mas’uud na wengineo.

Imekuja kutoka kwa Ibn Mas’uud kwamba amesema, “Alifariki Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam) nami nina miaka kumi na nimeshasoma al-Muhkam na al-Mufaswal (yaani kuanzia Surat Al-Hujuraat mpaka An-Naas). Al-Bukhaariy

Maana yake alikamilisha kuhifadhi Qur-aan baada ya hapo kama Ubay bin Ka’ab na Zayd bin Thaabit.

‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alihifadhi Suratul Baqarah kwa miaka kumi na alipomaliza alichinja Ngamia kumshukuru Allaah na hii ni dalili kwamba kuhifadhi haina umri maalum wala wakati maalum.NJIA KUMI ZA KUHIFADHI QUR-AAN

1. HATUA YA KWANZA


IKHLAAS NA NIA YA KWELI

Qur-aan ni maneno ya Allaah na kheri ya maneno, Naye hampi hii zawadi na fadhla (ya kuhifadhi) ila kwa aliyemjua ukweli wa nia yake na ikhlaas kwake Yeye. Na mwanaadamu bila ya nia ya kweli na ikhlaas inakuwa kazi yake ni bure.

Anasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam):

“Kila tendo ni kwa niyah na kila mtu atalipwa kwa niyah yake.” Al-Bukhaariy

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) anasema:

“Mwenye kujifundisha elimu inayotakiwa kwa ajili ya radhi ya Allaah akaitafuta ili apate cheo cha kidunia hatopata harufu ya pepo.” At-Tirmidhiy

Tunamuomba Allaah Atutengenezee niyah zetu na matendo yetu na Ajaalie tufanye kwa ajili Yake.


Itaendelea inshaAllaah…

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only