June 10, 2018

001-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Fasili Ya Twahara Na Umuhimu Wake

Twahara katika lugha ya kawaida:
 
Ni usafi na kumalizana na uchafu au takataka za kihisia kama vile najisi kutokana na mkojo au kinginecho, na uchafu wa kidhahania kama kasoro (mapungufu) na maasi.
 
Na kutwaharisha ni kusafisha, nako ni kuthibitisha usafi katika mahala.
 
Na Twahara kishariy'ah:
Ni kuondosha kile chenye kuzuia Swalah kutokana na hadathi au najisi kwa kutumia maji (au kinginecho) au kuondosha hukumu yake kwa mchanga.
 
Ama hukumu ya Twahara, bila shaka Twahara ya kilichonajisika na kukiondosha ni jambo la wajibu ikiwa mtu atakumbuka na ataweza. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:
((وَثِيَابَكَ فَطَهِّرْ))
«Na nguo zako zitwaharishe»[1] 
 
 
Na Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
((أَن طَهِّرَا بَيْتِيَ لِلطَّائِفِينَ وَالْعَاكِفِينَ وَالرُّكَّعِ السُّجُودِ))
 
«Ya kwamba itakaseni Nyumba Yangu kwa ajili ya wanaoizunguka kwa kutufu na wanaojitenga humo kwa ibada, na wanaoinama na kusujudu»[2]
 
Ama kujitwaharisha na hadathi, hilo ni lazima ili kuruhusika kuswali, kwa neno lake Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
(( لا تقبل صلاة بغير طهور))
 
 ((Swalah haikubaliwi bila ya wudhuu))[3]
 
Ama umuhimu wake, bila shaka Twahara:
1- Ni sharti ya kusihi kwa Swalah ya mja. Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((لا تقبل صلاة من أحدث حتى يتوضأ))
((Haikubaliwi Swalah ya mtu mwenye hadathi mpaka atawadhe))[4]
 
. Kwani kuswali na Twahara ni kumtukuza Allaah. Na hadathi na janaba – ingawa si najisi zenye kuonekana – lakini hata hivyo ni najisi za kidhahania zenye kuwajibisha kuonekana kichafu kile kilichoingiwa nazo. Kwa hiyo kuwepo kwake, hutetereshaukamilifuwa kumtukuza Allaah, na huenda kinyume na msingi wa usafi.
 
2- Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amewasifu wenye kujitwaharisha. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)  Amesema:
 
 
 ُ ((إِنَّ اللّهَ يُحِبُّ التَّوَّابِينَ وَيُحِبُّ الْمُتَطَهِّرِينَ))
«Hakika Allaah Anawapenda wenye kutubia na Anawapenda wenye kujitwaharisha»[5]
 
Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amewasifu watu wa Msikiti wa Qubaa kwa neno Lake:
 
((فِيهِ رِجَالٌ يُحِبُّونَ أَن يَتَطَهَّرُواْ وَاللّهُ يُحِبُّ الْمُطَّهِّرِينَ))
 
«Ndani yake kuna watu wanaopenda kujitwaharisha, na Allaah Anawapenda wenye kujitwaharisha»[6]
 
3- Kwamba kutojali kujitakasa na najisi, ni moja kati ya sababu za kuadhibiwa kaburini. Imepokelewa na Ibn  'Abbaas akisema: Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipita kwenye makaburi mawili akasema:
 
((إنهما يعذبان  وما يعذبان في كبير أما  هذا  فكان لا  يستنزه من بوله))  
 
((Hakika wao (maiti) wanaadhibiwa, na hawaadhibiwi kwa jambo kubwa. Ama huyu, alikuwa hajitakasi na mkojo wake….))[7]  
 
 
 
[1]   Al-Mudath-thir: 4
[2]   Al-Baqarah: 125
[3]   Swahiyh Muslim
[4]   Al-Bukhaariy na Muslim
[5]   Al-Baqarah: 222
[6]   At-Tawbah: 108
[7]   Abu Daawuud, An-Nasaaiy, Ibn Maajah, ikiwa na isnaad Swahiyh

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only