June 10, 2018

003-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Aina Za Najisi

Vitu ambavyo dalili ya kishariy'ah imeonyesha juu ya unajisi wake ni:

1, 2- Kinyesi cha mwanadamu na mkojo wake
Na viwili hivi ni najisi kwa makubaliano ya Maulamaa.
Ama kinyesi, ni kwa neno lake Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ((Akikanyaga mmoja wenu kinyesi kwa kiatu chake, basi udongo ndio kitwaharisho chake)). Pia zinaonyesha juu ya unajisi wake Hadiyth zote zenye kuamrisha kustanji, na zitakuja karibuni.

Ama mkojo, ni kwa Hadiyth ya Anas kwamba bedui mmoja alikojoa ndani ya msikiti, na baadhi ya watu wakamnyanyukia na kumwendea. Hapo Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia: ((Mwacheni msimkatishe))Akasema: Alipomaliza, aliagiza ndoo ya maji  akaimimina juu yake (sehemu iliyopatwa na mkojo).

3, 4- Madhii na wadii
Madhii:
Ni maji mepesi mno yenye kunatanata yanayotoka wakati wa matamanio kama wakati wa kuchezeana (mke na mume), au kukumbuka kuingilia kimwili (kufanya ngono) au kutaka kufanya. Maji haya hayachupi wala hayafuatiwi na mchoko, na huenda mtu asihisi kutoka kwake. Humtoka mwanamume na mwanamke, lakini kwa wanawake ni zaidi. Nayo ni najisi kwa makubaliano ya Maulamaa. Na kwa ajili hiyo, Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameamuru kuuosha utupu kwa kutoka maji hayo.
Katika Al-Bukhaariy na Muslim ni kwamba Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia aliyemuuliza kuhusu madhii: ((Atauosha uume wake na atatawadha)).

Ama wadii:  
Hayo ni maji mazito meupe yanayotoka baada ya kukojoa. Ni najisi kwa makubaliano (ijmaa) ya Maulamaa.
Imepokelewa na Ibn 'Abbaas akisema: "Manii, wadii na madhii. Ama manii, ni yale ambayo yakitoka, ni kuoga. Ama wadii na madhii, akasema: Uoshe utupu wako – au nyuchi zako – na tawadha wudhuu wako wa Swalah".

5- Damu ya hedhi
Ni kwa Hadiyth ya Asmaa binti Abu Bakr (Radhiya Allaahu 'anhuma), amesema: "Alikuja mwanamke fulani kwa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: Ewe Mtume wa Allaah! Mmoja wetu nguo yake ikiingiwa na damu ya hedhi, afanyaje? Akasema Mtume:(((Ataipikicha, kisha ataikwangua kwa ncha ya vidole na maji, kisha ataisuuza, na kisha atasali nayo)).

6- Kinyesi cha mnyama ambaye nyama yake hailiwi
Imepokelewa toka kwa 'Abdullah ibn Mas'uud, amesema: Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitaka kwenda haja kubwa akasema: ((Niletee mawe matatu))Nilimpatia mawe mawili na kinyesi cha (punda). Aliyachukua mawe mawili, akakitupa kinyesi na akasema: ((Hii ni najisi)).
Na kitendo hiki kimeonyesha kwamba kinyesi cha mnyama asiyeliwa nyama yake ni najisi.

7- Mate ya mbwa
Hakika Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Kukitwaharisha chombo cha mmoja wenu anapokilamba mbwa ni kukiosha mara saba, moja kati ya hizo kwa mchanga)).
Na bila shaka Hadiyth imeonyesha kwamba mate ya mbwa ni najisi.

8- Nyama ya nguruwe
Ni najisi kwa makubaliano ya Maulamaa kwa kuelezewa wazi katika neno Lake Subhaana:
« Sema: Sioni katika yale niliyofunuliwa mimi kitu kilichoharamishwa kwa mlaji kukila isipokuwa kiwe ni nyamafu, au damu inayomwagika, au nyama ya nguruwe, kwani hiyo ni uchafu» [6:145]

9- Nyamafu
Nao ni mzoga wa mnyama aliyejifia mwenyewe bila ya chinjo la kishariy'ah. Ni najisi kwa ijmaa ya Wanachuoni kwa neno lake Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam: ((Inapotiwa rangi ngozi ya nyamafu, basi imetwaharika)).
Haviingii katika hukumu hii:
(a) Maiti ya samaki na nzige.
Kwani viwili hivi ni Twahara kwa neno lake Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):((Tumehalalishiwa maiti mbili na damu mbili. Ama maiti mbili ni samaki na nzige. Ama damu mbili ni ini na wengu)).
(b) Maiti ya asiye na damu ya kuchuruzika
Kama vile nzi, nyuki, sisimizi, chawa na kadhalika kwa neno lake Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Akiangukia nzi katika chombo cha mmoja wenu, basi amzamishe wote au amtupe, kwani hakika katika bawa lake moja kuna ugonjwa na katika jingine kuna ponya)).
(c) Mfupa wa mfu, pembe yake, kucha yake, manyoya yake na magoya yake.
Hivi vyote asili yake ni Twahara. Al-Bukhaariy katika Swahiyh yake (1/342) ameeleza: Amesema Az-Zuhriy - kuhusu mifupa ya mzoga wa mnyama kama vile tembo na wengineo - : Niliwakuta watu katika Maulamaa watangu wema wakichania nywele na wakijitia mafuta kwa vitu hivyo, hawaoni kwa hilo ubaya wowote.

10- Kilichokatwa toka kwa mnyama aliye hai
Kilichokatwa toka kwa mnyama aliye hai, kina hukumu ya nyamafu kwa neno lake Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Kilichokatwa toka kwa mnyama aliye hai, basi hicho ni nyamafu)).

11- Mabaki ya maji yaliyonywewa na mnyama mkali au mnyama asiye mkali ambaye nyama yake hailiwi.
Unajisi wake unaonyeshwa na kauli yake Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam alipokuwa akiulizwa kuhusu maji yanayokuwa jangwani (nyikani), na yale yanayonywewa mara kwa mara na wanyama wakali au wasio wakali akasema: ((Maji yakiwa kullatayni, hayabebi uchafu (najisi)).
Ama paka na walio chini yake, basi mabaki yake ni Twahara kwa neno lake Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Hakika yeye si najisi, bali ni katika wanaowazungukeni wa kiume na kike)).

12- Nyama ya mnyama asiyeliwa
Hii ni kwa Hadiyth ya Anas (Radhiya Allahu 'anhu)   amesema: "Tuliipata nyama ya punda – yaani siku ya Khaybar – na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akanadi: ((Hakika Allaah na Mtume Wake Anakukatazeni nyama ya punda, kwani hakika ni uchafu)) (najisi).
Na kwa Hadiyth ya Salamah bin Al Akwa'a, amesema: Ilipoingia jioni ya siku waliyofunguliwa Khaybar, waliwasha mioto mingi. Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia:((Moto huu ni wa nini? Mmeuwashia kwa jambo gani?)) Wakasema: "Kwa nyama".Akasema: ((Kwa nyama ya nini?))Wakasema: Kwa nyama ya punda wa mjini. Akasema:((Imwageni na kivunjeni))Akasema mtu mmoja: Ewe Mtume wa Allaah! Je, tuimwage na tukioshe? Akasema: ((Au hilo)).
Katika Hadiyth hizi mbili, kuna dalili juu ya unajisi wa nyama ya punda wa mjini (kienyeji) kwa neno lake Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth ya kwanza: ((Kwani hakika ni uchafu)) (najisi), na katika Hadiyth ya pili kwa kukivunja chombo kwanza, kisha kuruhusu kutumika  kwa kukiosha mara ya pili.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only