June 10, 2018

006-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Je, Damu Inazingatiwa Kuwa Ni Katika Najisi?

Damu ina vigawanyo:
  
1- DAMU YA HEDHI:

Damu hii ni najisi kwa makubaliano ya Maulamaa. Dalili ya unajisi wake imekwisha elezewa nyuma.

2- DAMU YA MWANADAMU[1]

Ni damu iliyosababisha mahitalifiano juu ya hukumu yake. Lililo mashuhuri kwa watu wa madhehebu ya kifiqhi ni kwamba damu ni najisi, lakini wao hawana hoja. Isipokuwa damu imeharamishwa kwa matini ya Qur-aan katika neno Lake Aliyetukuka:

((قُل لاَّ أَجِدُ فِي مَا أُوْحِيَ إِلَيَّ مُحَرَّمًا عَلَى طَاعِمٍ يَطْعَمُهُ إِلاَّ أَن يَكُونَ مَيْتَةً أَوْ دَمًا مَّسْفُوحًا أَوْ لَحْمَ خِنزِيرٍ فَإِنَّهُ رِجْسٌ ))
« Sema: Sioni katika yale niliyofunuliwa mimi kitu kilichoharamishwa kwa mlaji kukila isipokuwa kiwe ni nyamafu, au damu inayomwagika, au nyama ya nguruwe, kwani hiyo ni uchafu».[2]

Kwa hiyo, wao wamewajibisha unajisi wake kutokana na kuharamishwa kwake, kama walivyofanya katika pombe, na wala hayafichikani yaliyomo ndani yake. Lakini amenukuu zaidi ya Mwa- nachuoni mmoja katika Maulamaa kuwa wanakubaliana wote (ijmaa) juu ya unajisi wake. Maelezo zaidi yatakuja katika hilo.

Ni wakati ambapo kundi la waliokuja baadaye akiwemo Ash-Shawkaany, Swiddiyq Khaan, Al-Albaaniy, Ibnu ‛Uthaymiyn (Allaah Awarehemu) wameelekea kusema kuwa damu ni twahara kwa kutothibiti ijmaa kwa upande wao. Wao wametoa dalili vilevile kwa haya yafuatayo:
1- Asili ya vitu ni twahara mpaka iwepo dalili kuwa ni najisi. Na sisi "hatujui" kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliamuru kuosha damu nyingine isiyo ya hedhi ingawa mtu hupatwa mara nyingi na majeraha na mfano wake. Na lau kama damu ni najisi, basi Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) angelibainisha, kwa sababu hali ya mambo inahitajiahilo.

2- Ni kwamba Waislamu bado wanaswali wakiwa na majeraha yao, na wanaweza kuchuruzikwa na damu nyingi ambayo si ya kusamehewa. Na wala haikupokelewa toka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba aliamuru kuiosha, na wala haikupokelewa kwamba wao walikuwa wakijilinda nayo kwa hadhari kubwa.

- Amesema Al-Hasan: "Waislamu bado wanaswali wakiwa na majeraha yao".[3]
Na katika kisa cha Swahaba Muanswaar aliyekuwa amesimama usiku akiswali. Mshirikina alimpiga mshale, akauweka, kisha akaunyofoa, mpaka akampiga mishale mitatu. Kisha alirukuu, akasujudu na akaendelea na Swalah yake na huku akivuja damu.[4]

- Al-Albaaniy[5]  (Allaah Amrehemu) amesema: "Nayo iko katika hukumu ya Hadiyth Marfuu, kwa vile kwa kawaida haiyumkiniki  kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) asilijuehilo. Na lau kama damu nyingi ingelikuwa ni yenye kuvunja (kubatilisha Swalah), basi Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) angelibainisha, kwani kuchelewesha kubainisha (jambo) wakati ule wa kuhitajika, haifai kama inavyojulikana katika taaluma ya "usuul". Na kamatutachukulia kwamba hilo lilifichikana kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), basi halifichikani kwa Allaah Ambaye hakifichikani Kwake chenye kujificha sawasawa ardhini au mbinguni. Na lau kama (damu) ingelikuwa ni yenye kubatilisha au ni najisi, basi lingefunuliwa hilokwa Mtume kama ilivyo wazi, haifichikani kwa yeyote…..".

- Na katika kisa cha kuuawa ‘Umar bin Al-Khatw-twaab (Allaah Amridhie):  "Umar aliswali, na huku jeraha lake linachuruzisha damu".[6]

3- Ni kwa Hadiyth ya 'Aaishah katika kisa cha kufa kwa Sa'ad bin Mu’adh. Alisema: "Wakati Sa'ad bin Mu’adh alipojeruhiwa siku ya Khandaq, mtu mmoja alimpiga mshale wa kwenye mshipa wa damu mkononi. Mtume alimpigia hema msikitini ili amtazame kwa karibu. Na akiwa katika hali hiyo, usiku mmoja ghafla jeraha lake lilipasuka na damu ikachuruzika toka katika kidonda chake.  Wakasema: Enyi watu wa nyumba! Nini hiki kinatujia toka kwenu? Wakatazama. Na kumbe Sa'ad jeraha lake limepasuka na damu ikifoka, akafariki [7]    

Ninasema (Abuu Maalik): "Na wala haikupokelewa kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliamuru maji yamwagiwe juu yake na hasa kwa vile yuko msikitini kama alivyoamuru kumwagia maji juu ya mkojo wa bedui.

4- Kwamba Ibnu Rushdi wakati alipotaja hitilafu za Maulamaa kwa upande wa damu ya samaki, alieleza kwamba sababu ya kuhitalifiana kwao, ni kuhitilafiana kwao katika maiti yake. Basi mwenye kuifanya maiti yake inaingia chini ya ujumuishi wa kuharamishwa, ataifanya damu yake hivyo hivyo. Na mwenye kuitoa maiti yake, ataitoa damu yake kwa kupimia maiti yake.

Na tunasema: "Wao wanasema kuwa maiti ya mwanadamu ni twahara, na kwa hivyo damu yake vilevile (ni twahara) kwa mujibu wa kanuni yao".
Na kwa ajili hiyo, Ibnu Rushdi alisema baada yake: "Na matini bila shaka imeonyesha juu ya unajisi wa damu ya hedhi, na isiyokuwa hiyo, basi iko katika uasili uliokubaliwa na wenye kuzozana, nayo ni twahara. Na haitoki humo ila kwa matini ya kusimamishia hoja…".

Na ikiwa itasemwa: "Je, haipimiwi kwa damu ya hedhi, na damu ya hedhi ni najisi?
Tunasema: "Hiki ni kipimo pamoja na tofauti:
- Kwani damu ya hedhi ni damu ya maumbile ya asili kwa wanawake. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((ان هذا شيئ كتبه الله على بنات آدم))
((Hakika hiki ni kitu ambacho Allaah Amekiweka kwa mabinti wa Aadam (wanawake))[8]
Na akasema katika istihaadha:
((انه دم عرق))
((Hakika hiyo ni damu ya mshipa (asili))  [9]  Kisha hakika damu ya hedhi ni damu nzito iliyovunda na yenye harufu mbaya. Imefanana na mkojo na kinyesi, si damu yenye kutoka katika zisizo njia mbili.


3- DAMU YA MNYAMA MWENYE KULIWA

Mjadala kuhusu damu hii, ni kama mjadala kuhusu damu ya mwanadamu kwa upande wa kutokuwepo dalili juu ya unajisi wake. Kwa hivyo inaambatana na utwahara wa asili.
Kusema kuwa ni twahara kunaungwa mkono vilevile na:
Yaliyoelezewa na Ibnu Masoud, amesema:  "Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali mbele ya Ka’abah, na ilhali Abuu Jahli na marafiki zake wamekaa. Pale walipoambiana: Ni yupi kati yenu atakayewaendea  ngamia wa akina fulani, akakusudia taka zake, damu zake, na miji yake (wombs), kisha akamsubiri mpaka anaposujudu, halafu akamwekea mabegani mwake? Basi mwovu wao akachomoka haraka, na aliposujudu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), aliyaweka kati ya mabega yake, na Mtume Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi sallam alitulia tuli katika sijdah, na wao wakacheka.[10].  

Na lau kama damu ya ngamia ingelikuwa ni najisi, basi Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) angeliitupa (angeliidondosha) nguo yake, au angeliikatisha Swalah yake.

Na imethibiti kwa njia sahihi kwamba Ibnu Mas’uud aliswali nailhali katika tumbo lake kuna taka na damu ya ngamia aliowachinja, na wala hakutawadha.  [11]

Na ingawa tukiona pokezi hili "athar" linaweza kufanyiwa mvutano katika kutolea ushahidi juu ya utwahara wa damu ya mnyama, kwa vile Ibnu Mas’uud hakuwa akiona kwamba utwahara wa mwili na nguo ni sharti ya kusihi Swalah, bali anaona kuwa ni jambo linalopendeza (mustahab).

Ninasema (Abuu Maalik): Lau kama imethibiti kwa ijmaa kwamba damu ni najisi, basi hatutaziangalia dalili za waliofuatia baadaye. Na kama haikuthibiti, basi asili ni utwahara na sisi hatuhitajii dalili hizo. Na lililodhihiri kwangu - baada ya kuchagua kauli (isemayo kuwa) damu ni twahara kwa kipindi cha miaka kumi - ni kwamba ijmaa katika suala imethibiti. Ijmaa hii imenukuliwa na Maulamaa wengi na hakikuthibiti chenye kuitengua. Na nukuu ya juu zaidi kati ya hizo ni yale yaliyonukuliwa toka kwa Imaam Ahmad, kisha yale aliyoyanukuu Ibn Hazm, kinyume na yule aliyedhani kwamba madhehebu yake yanasema kwamba damu ni twahara!! Na kati ya niliyoyafahamu katika hilo ni:

Ibnu Al-Qayyim katika "Ighaathat Allahafaan" (1/420) amesema:

Ahmad aliulizwa: "Je, damu na usaha kwako ni sawasawa"? Akasema: "Hapana, watu hawakuhitilafiana kuhusu damu".

Na alisema mara moja: "Usaha kwangu ni afadhali kuliko damu…".

Na imenukuliwa toka kwa Ibnu Hazm katika   "Maraatib Al-Ijmaa": "Kukubaliana Maulamaa juu ya unajisi wa damu".

Vile vile Al-Haafidhw katika "Al-Fat-h" (22/420) amekunukuu kukubaliana huko.

Na Ibnu Abdul-Barri katika "At-Tamhiyd" (22/230) anasema:

"Na hukumu ya kila damu ni kama damu ya hedhi, isipokuwa damu kidogo husamehewa kwa vile Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ameweka sharti ya unajisi wa damu kuwa iwe ni yenye kuchuruzika, na hapo inakuwa ni uchafu, na uchafu ni najisi. Na hii ni ijmaa ya Waislamu kwamba damu yenye kuchuruzika ni uchafu na najisi..".

Na Ibnu Al-Arabiy katika "Ahkaam Al-Qur-aan" (1/79) anasema:

"Maulamaa wamekubaliana kwamba damu ni haramu na ni najisi kwa kinacholiwa na kisichopatiwa manufaa. Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ameiainisha hapa kwa kuifanya ni yoyote ile (mutwlaq), na katika Surat Al-An 'Aam Ameiainisha kwa kuiwekea mpaka (muqayyad) ile tu ya kuchuruzika. Na Maulamaa kwa ijmaa hapa, wameichukulia damu yoyote wakaiacha iliyowekewa mpaka….".

Na An-Nawawy katika Al-Majmu’u (2/576) amesema:
"Na dalili juu ya unajisi wa damu zinatiliana nguvu zenyewe kwa zenyewe, na mimi sijui kama kuna hitilafu yoyote toka kwa Muislamu yeyote ila tu yale aliyoyaelezea mtunzi wa Al-Haawiy toka kwa baadhi ya Maulamaa wa tawhiyd. Amesema kuwa ni twahara, lakini Maulamaa wa tawhidi maneno yao hayachukuliwi katika ijmaa au mahitalifiano…".


Ninasema (Abuu Maalik): Ninalolipa nguvu na uzito ni kuwa damu ni najisi kwa kuthibiti ijmaa mpaka inukuliwe toka kwa Imaam mwingine atakayempiku Imaam Ahmad – (Allaah Amrehemu) – kwa kusema kuwa damu ni twahara. Na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi.
 
[1]  Tafsiri ya Al-Qurtuby (2/ 221), Al-Majmuu (2/511), Al-Muhalla (1/102), Al-Kaafy (1/110), Bidaayatul Mujtahid, As-Saylul Jarraar (1/31), Ash-Sharhul Mumti'i (1/376), As-Silsilatu Asw-Swahiyhah na Tamaamu Al-Minnah (uk.50).
[2]  Surat Al-An ‘aam: 145

[3]   Isnadi yake ni sahihi. Imepokelewa na Al-Bukhaariy ikiwa "muallaq" (1/336). Na Ibnu Abu Shaybah ameiunganisha kwa sanad sahihi kama ilivyo katika Al-Fath (1/337).
[4]   Hadiyth Sahihi: Al-Bukhaariy ameifanya "mu’allaq" (1/336), na Ahmad na   wengineo wameiunganisha, nayo ni sahihi.  
[5]   Tamaam Al-Minnah (51,52) 

[6]    Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Maalik (82), na amepokea toka kwake Al-Bayhaqiy (1/357) na wengineo kwa sanad sahihi.

[7]    Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Abuu Daawuud (3100) kwa ufupi, na At-Twabaraaniy katika (Al-Kabiyr) (6/7).

[8]    Hadiyth Sahihi: Al-Bukhaariy (294), na Muslim (1211).
[9]   Hadiyth Sahihi: Al-Bukhaariy (327), na Muslim (333).
[10]   Hadiyth Sahihi: Al-Bukhaariy (240) na Muslim (1794).
[11]  Isnadi yake ni sahihi: Muswannaf Abdur-Raaziq (1/25), na Ibnu Abuu Shaybah (1/392).

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only