011-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Je, Ni Lazima (kutumia) Maji Katika Kuondosha Najisi? Au Inajuzu Kuondosha Kwa Vimiminika Vinginevyo Au Mada Nyinginezo?

Maulamaa wamehitalifiana katika suala hili juu ya kauli mbili mashuhuri:


KAULI YA KWANZA

Ni sharti kutumia maji kwa ajili ya kuondosha najisi, na wala haisihi kwa kinginecho ila kwa dalili.
Na hili ndilo mashuhuri katika madhehebu ya Maalik na Ahmad. Na pia ni madhehebu ya Ash-Shaafi'iy katika "Al-Jadyd" (rai mpya). Ash-Shawkaany na waliomfuata,[1] ameliunga mkono hili. Na hoja yao ni:

1- Neno Lake Ta'aala
((وَيُنَزِّلُ عَلَيْكُم مِّن السَّمَاء مَاء لِّيُطَهِّرَكُم بِهِ))
«Na Anawateremshieni maji toka mbinguni ili Awatwaharisheni kwayo »  [2]

2- Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliamuru kumwagia maji juu ya mkojo wa bedui [3]  
Wamesema kwamba amri ni ya ulazima, na kwa hivyo haitoshelezi katika kuondosha najisi isipokuwa kwa maji!!

3- Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kama ilivyo katika Hadiyth ya Abuu Tha'alabah, aliamuru kukiosha chombo cha Ahlul-Kitaab kwa maji [4]    

4-Amesema Ash-Shawkaany: "Maji ndio asili katika kutwaharisha najisi kwa kuelezewa kwake na Mwekaji sheria kuwa ni twahara yenyewe yenye kutwaharisha kinginecho. Basi hayaachwi kikatumika kingine ila kama litathibiti hilo toka kwa Mwekaji sheria. Na kama si hivyo, basi haiwezekani. Kwani hiyo ni kuachana na kinachojulikana kwamba maji ni twahara kwenda kwenye kisichojulikana kuwa ni twahara. Na hiyo ni kutoka nje ya vile mikondo ya kishariy'ah  inavyokwenda…".


KAULI YA PILI

Inatosheleza kujitwaharisha kwa kila chenye kuondosha najisi, na si lazima maji.

Na haya ndio madhehebu ya Abuu Haniyfah, na riwaya nyingine toka kwa Maalik na Ahmad, na kauli ya zamani ya Ash-Shaafi'iy, na Ibnu Hazm. Nalo ndilo chaguo la Shaykh wa Uislamu Ibnu Taymiyah, na pia Mwanachuoni Mkubwa Ibnu 'Uthaymiyn [5] Ni kauli yenye nguvu kwa yafuatayo:

1- Kwamba maji kuwa ni twahara yenyewe na yenye kutwaharisha kingine, hakuzuii kingine kuwa ni chenye kutwaharisha vilevile. Kwani kanuni inasema: "Kukosekana sababu maalumu, hakuhukumii kuondoka kisababisho maalumu, sawasawa ikawa dalili au sio dalili". Kwa vile chenye kuathiri kinaweza kuwa ni kitu kingine. Na hii ndio hali halisi kwa upande wa najisi [6]
Ninasema (Abuu Maalik): "Bali baadhi ya vimiminika kama vile siki na madawa ya kusafishia ya viwandani, huondosha najisi kama maji au zaidi kuliko maji".

2- Kwamba Mwekaji sheria Ameamuru kuondosha najisi kwa maji katika masuala maalumu, na wala Hakuamuru amri jumuishi kwamba kila najisi iondoshwe kwa maji.

3- Kwamba shariy'ah imeruhusu kuondosha baadhi ya najisi bila maji kama kustanji kwa jiwe, au kuvisugua viatu kwa mchanga, au kutwaharika nguo inayoburuzika kwa (kugusana na) ardhi, na mengineyo yaliyotangulia.

4- Kwamba kuondosha najisi si katika mlango wa kilichoamriwa, bali ni katika mlango wa kujiepusha na kilichokatazwa. Na ikitokea (ikaondoshwa) kwa sababu yoyote ile, hukumu itathibiti. Na kwa ajili hiyo, nia haishurutishwi katika kuondosha najisi. Lakini kama itaondoka kwa kitendo cha mtu aliyenuia, basi atalipwa thawabu kwa hilo. Na kama si hivyo, kamaitaondoshwa bila kitendo chake wala nia yake, madhara yataondoka, na wala hatokuwa na thawabu wala hatokuwa na madhambi.

Na hili linatiliwa nguvu na kwamba pombe inapobadilika na kuwa siki, basi inakuwa imetwaharika – kwa wale wanaosema kuwa pombe ni najisi – kwa makubaliano ya Waislamu.

Ninasema (Abuu Maalik): "Lenye nguvu ni kuwa najisi inapoondoka kwa kitu chochote, hukumu yake inaondoka na inakuwa ni twahara".


HAPA KUNA FAIDA KADHAA

1- Faida ya suala hili ni kuwa mtu ambaye kwenye nguo yake au katika mwili wake kuna najisi, na akatumia chochote katika madawa twahara ya kusafishia – yasiyo maji – ili kuondosha najisi hiyo, basi hilo humtosheleza na wala si lazima aoshe kwa maji.

2- Haijuzu kutumia vyakula au vinywaji katika kuondoshea najisi bila dharura, kwani huo ni uharibifu wa mali [7]

3- Kwamba utwaharishaji bila maji kwa (kutumia) vimiminika vingine au mada nyinginezo, bila shaka hufanyika katika (kiini cha) najisi yenyewe inayokuwepo katika nguo au mwili au mahala. Ama utwaharishaji wa kihukumu (twahara ya hadathi) kama vile wudhuu, kuoga na mfano wake, haitotosheleza isipokuwa kwa maji.


[1]     "Bidaayatul Mujtahid" (1/99), na "Al-Ummu" (1/49), na "As-Saylu Al-Jarraar" (1/49).  
[2]    Surat Al-Anfaal-Aya ya 11. 
[3]   Imekubaliwa na wote. Na imetangulia hivi punde. 
[4]   Imekubaliwa na wote. Imetolewa na Al-Bukhaariy (5170), na Muslim (1930).

[5]    "Al-Badaai'i (1/83), na "Fathul Qadyr" (1/200), na "Majmu'u Al-Fataawaa" (21/475), na "Al-Muhallaa" (1/92-94), na "Ash-Sharhu Al-Mumti'i"(1/361-363). 
[6]    Ash-Sharhu Al-Mumti'i (1/362).
[7]    "Majmu'u Al-Fataawaa" (21/475).

0 Comments