September 16, 2018

Hali Ya Nyuso Za Watu Waovu Na Watu Wema Siku Ya Qiyaamah

Tunaendelea na Aayah katika Suratuz-Zumar baada ya nafsi iliyojidhulumu kufikwa na majuto na kuwa katika khasara kubwa, atakumbushwa mtu ujeuri wake aliokuwa nao alipokuwa duniani kwa kutokukubali haki:
 }}بَلَى قَدْ جَاءتْكَ آيَاتِي فَكَذَّبْتَ بِهَا وَاسْتَكْبَرْتَ وَكُنتَ مِنَ الْكَافِرِينَ{{
{{Wapi! Bila ya shaka zilikujia Ishara Zangu, nawe ukazikadhibisha, na ukajivuna, na ukawa miongoni mwa makafiri!}} [Az-Zumar: 59].

Maana; ewe unayejuta uliyoyafanya, Aayah za Mola wako zilikufikia ulipokuwa duniani pamoja na dalili na ushahidi kwako, lakini ulizikanusha ukawa mjeuri sanakuzifuata ukawa miongoni mwa wale waliozikufuru. [Tafsiyr Ibn Kathiyr]
}}وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ تَرَى الَّذِينَ كَذَبُواْ عَلَى اللَّهِ وُجُوهُهُم مُّسْوَدَّةٌ أَلَيْسَ فِي جَهَنَّمَ مَثْوًى لِّلْمُتَكَبِّرِينَ{{
{{Na Siku ya Qiyaamah utawaona waliomsingizia uongo Allaah nyuso zao zimesawijika. Je! Si katika Jahannamu makaazi ya wanaotakabari?}} [Az-Zumar: 60].
Maana; hao ni waliomkufuru Allaah سبحانه وتعالى  kwa kumhusisha Aliyoepukana nayo,kama kumshirikisha na mtu, au kusema ana msaidizi, au mtoto. Na hapa inahusu pia yeyote atakayemhusisha na sifa zisizokuwa na dalili. 

Vile vile inamhusu atakayetunga sheria isiyokuwa ya haki inayomhusu Allaah سبحانه وتعالى  na ikatangaa na kufuatwa na watu. Lakini hii haiwahusu 'Ahlul Ijtihaad' 'Wale wanaojitahidi' wanapokosea katika jitihada yao ya kutumia Qiyaas kutoka katika ushahidi wa dalili na hukmu.

Wala haimpasi mtu kusema Allaah سبحانه وتعالى Kasema, au Kaamrisha jambo bila ya kutoa dalili kutoka katika Qur-aan na Sunnah.

Siku ya Qiyaamah watagawanywa katika makundi mawili, watu wema na watu waovu. Na Allaah سبحانه وتعالى  Ametofautisha aina za nyuso za makundi hayo mawili; nyuso za watu wema siku hiyo zitakuwa nyeupe zenye nuru, zinazong'ara na zenye furaha  
}}وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ مُّسْفِرَةٌ{{  
{{ Siku hiyo ziko nyuso zitazonawiri}}
}} ضَاحِكَةٌ مُّسْتَبْشِرَةٌ{{  
{{Zitacheka, zitachangamka}} ['Abasa: 38-39].

 Na kamaAlivyosema pia katika Suratul-Ghaashiyah:
}}وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ نَّاعِمَةٌ{{  
}} لِسَعْيِهَا رَاضِيَةٌ{{
{{Siku hiyo nyuso nyengine zitakuwa kunjufu}}
{{Zitakuwa radhi kwa juhudi yao}} [Al-Ghaashiyah: 8-9].

Ama nyuso za watu waovu zitakuwa ni nyeusi zenye kuchoka, na zilizojaa huzuni kwa majuto:
}} وَوُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ عَلَيْهَا غَبَرَةٌ  {{
 }}تَرْهَقُهَا قَتَرَةٌ{{
 }}أُوْلَئِكَ هُمُ الْكَفَرَةُ الْفَجَرَةُ{{
{{Na nyuso siku hiyo zitakuwa na mavumbi}}
{{Giza totoro litazifunika}}
{{Hao ndio makafiri watenda maovu}} ['Abasa: 40-42].
}}وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ خَاشِعَةٌ{{
}}عَامِلَةٌ نَّاصِبَةٌ  {{
{{Siku hiyo nyuso zitainama}}
{{Zikifanya kazi, nazo taabani}} [Al-Ghaashiyah: 2-3].


 *********

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only