Sayyid Al-Istighfaar (Bwana Wa Du'aa Zote Za Tawbah)

Allaah Anasema:

{{Na ambao pindi wafanyapo uchafu au wakajidhulumu nafsi zao humkumbuka Allaah na wakamwomba msamaha kwa dhambi zao - na nani anaye futa dhambi isipo kuwa Allaah? - na wala hawaendelei na waliyo yafanya na hali wanajua.}}[Al-‘Imraan: 135]

Imesimuliwa kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Allaah huifurahia toba ya mja wake kuliko mmoja wenu anapokuwa juu ya mnyama wake jangwani akamuangusha na kumkimbia.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy]

Na katika riwaya ya Muslim na wengine:

((Allaah huifurahia toba ya mja wake kuliko mmoja wenu anapokuwa juu ya mnyama wake jangwani akamuangusha na kumkimbia. Mnyama huyo akiwa amebeba chakula chake na maji yake, kisha mtu huyo akakata tamaa, akauendea mti na kuegemea chini ya kivuli chake akiwa keshakata tamaa ya kumuona mnyama wake tena. Na anapokuwa katika hali hiyo, ghafla anamuona mnyama wake mbele yake. Akazishika hatamu zake, kisha akasema kwa furaha: "Mola wangu Wewe ni mja wangu na mimi ni mola wako". Alikosea kwa wingi wa furaha.))

Na maana ya Allaah kuifurahia toba hiyo ni kuwa anaridhika na nia ya mja wake huyo juu ya kuwa alikosea kutamka.

Miongoni mwa du’aa za kuomba maghfira, ni hii du’aa inayoitwa 'Sayyidul-Istighfaar'(Du’aa bora ya kuomba maghfira kupita zote) aliyotuusia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Du’aa ambayo ndani yake imekusanya maana zote za tawbah na kukiri, na kwamba hapana mwenye kusamehe makosa isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).

Imeposimuliwa kutoka kwa Shaddaad bin ‘Aws (Radhiya Allaahu ‘Anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Bwana wa kuomba maghfira ni kusema:
اللَّهُمَّ أَنْتَ رَبِّي لا إِلَهَ إلا أَنْتَ خَلَقْتَنِي وَأَنَا عَبْدُكَ وَأَنَا عَلَى عَهْدِكَ وَوَعْدِكَ مَا اسْتَطَعْتُ أَعُوذُ بِكَ مِنْ شَرِّ مَا صَنَعْتُ أَبُوءُ لَكَ بِنِعْمَتِكَ عَلَيَّ وَأَبُوءُ لَكَ بِذَنْبِي فَاغْفِرْ لِي فَإِنَّهُ لا يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلا أَنْتَ.
Allaahumma anta Rabbiy laa ilaaha illa Anta. Khalaqtaniy wa ana ‘abduka. Wa ana ‘alaa ‘ahadika wa wa’adika ma statwa’atu. A’udhu bika min sharri ma swana’atu. Abu-u laka bini’imatika ‘alayya wa abu-u laka bidhanbiy, faghfirliy, fainnahu laa yaghfiru dhunuuba illaa anta.

Akasema: Atakayesema hayo wakati wa mchana akiwa na yakini juu yake akafa siku hiyo kabla ya usiku kuingia, huyo ni katika watu wa Peponi. Na atakayesema hayo wakati wa usiku akiwa na yakini juu yake akafa kabla ya asubuhi kuingia, huyo ni katika watu wa Peponi.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy, At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy na wengine]


Maana Yake


Ee Allaah. Wewe ni Mola wangu hapana anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Wewe
اللَّهُمَّ أَنْتَ رَبِّي لا إِلَهَ إلا أَنْتَ
Umeniumba na mimi ni mja Wako
خَلَقْتَنِي وَأَنَا عَبْدُكَ
Na mimi nimo katika kutekeleza maamrisho Yako na waadi Wako niwezavyo
وَأَنَا عَلَى عَهْدِكَ وَوَعْدِكَ مَا اسْتَطَعْتُ
Ninajikinga Kwako na kila shari niliyoitenda
أَعُوذُ بِكَ مِنْ شَرِّ مَا صَنَعْتُ
Ninakiri Kwako kwa neema Zako juu yangu
أَبُوءُ لَكَ بِنِعْمَتِكَ عَلَيَّ
Na ninakiri Kwako juu ya dhambi zangu
وَأَبُوءُ لَكَ بِذَنْبِي
Kwa hivyo unisamehe kwa sababu hapana mwenye kusamehe madhambi isipokuwa Wewe
فَاغْفِرْ لِي فَإِنَّهُ لا يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلا أَنْتَ.

0 Comments