Swalah Ya Dhwuhaa - Rakaa Zake, Fadhila Zake na Wakati Wake

SWALI LA KWANZA:
Naomba kujuwa kuhusu swala ya Dhuhaa hii nikwa ushahidi wa rasulallahi (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)? na ina rakaa ngapi na inaanzia wakati gani?.

SWALI LA PILI:
Kuna sala ya dhuha.. je hii sala hii inasaliwa mwezi gani? wakati gani? na ni rakaa ngapi? na ni kwa muda gani? na ni kwa madhumuni gani


JIBU:
Sifa zote njema anastahiki Allah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Swalah ya Dhuhaa ni kati ya sunnah za Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) imepokewa kutoka kwa Jaabir bin Nufair, kutoka kwa Abu Dar-daa na Abu Dharr, kutoka kwa Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema: amesema Allah Mtukufu, "Ewe mwanadamu Swali kwa ajili (kutafuta radhi) Zangu, rakaa (chache) mwanzo wa mchana (Dhuhaa) Mimi Nitakuwa tosha yako wakati wa jioni" (At-Tirmidhiy Hadiyth Namba 475, Abu Dawuud Hadiyth Namba 1289 na Shaykh Al-Albaaniy katika Ir-waul-Ghaliyl Namba 1465).
Swalah hii haina miezi maalumu ya kuswaliwa, bali ni kuiswali kila siku katika maisha yake Muislamu kwa mwenye kuweza. 

IDADI YA RAKAA ZAKE:

Zifuatazo ni kauli za wanachuoni:   
Kauli ya kwanza: Wingi wa rakaa zake kwa mujibu wa madhehebu Malikiyah, Shafiiyyah, na Hanabilah. (ni rakaa nane) na ushahidi wao ni Hadiyth ya:


عـَن أُمِّ هـَانئ   رضي الله عنها قالت ذَهَبتُ إلى رسول ِ الله ِ صلى الله عليه وسلم عام الفـَتْح فـَوَجـَدْتُهُ يـَغْتـَسِل فـَلـَمَّا فـَرَغَ مـِنْ غـُسْلِه صَـلى ثـَمانيَ رَكَعاتٍ ، وذَلكّ الضـُّحى"  ـ متفق عليه
Ummu Haaniy (Radhiya Allahu ‘anhaa) anasimulia ya kwamba alikwenda nyumbani kwa Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mwaka ulipofunguliwa mji wa Makkah akamkuta anajiosha, alipomaliza aliswali rakaa nane… na hiyo ni Dhuhaa”


 Kauli ya pili: ni kauli ya jamhuri ya wanachuoni, Wao wanasema Swalah ya Dhuhaa haina idadi maalum kwa ushahidi wa Hadiyth ya  Bi ‘Aaishah (radhiya Allahu ‘anha)
  
 كَان رسولُ الله ِ صـَلى الله عليه وسلم يـُصـَلْي الضُّحـَى أرْبـَعاً، ويـَزيدُ ما شـَاءَ الله ـ رواه مسلم
 Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali Dhuhaa nne na huongeza Masha Allah” (Alivyomjaalia Allah) [Muslim]


WAKATI WAKE:


Ama kuhusu wakati wa Swalah ya Dhuhaa unaanza robo saa mara baada ya kuchomoza kwa jua, mpaka kabla ya kuingia kwa wakati wa adhuhuri, yaani kama robo saa hivi ili usije kuingia wakati wa makruuh (uliochukiza kuswaliwa).

FADHILA ZAKE:

عـَن أبي هـُريْرَة رضيَ الله عنه قال : أوصـَانـِي خـَليلي صـَلـَّى الله عليه وسلم بـِصـِيامِ ثـَلاثـَة ِ أيـَّام ٍ مـِنْ كـُل شـَهر ٍ، وَ ركـْعـَتي الضـُّحى ، وأنْ أوتـِرَ قبلَ أنْ أرقـُـد "  ـ متفق عليه ـ


Kutoka kwa Abu Hurayrah (radhiya Allahu ‘anhu) kwamba “Ameniusia rafiki yangu Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam kufunga siku tatu katika kila mwezi, Rakaa mbili Dhuhaa na niswali Witr kabla ya kulala” [Al-Bukhaariy na Muslim]عـَن أبي ذَرٍّ رضي الله ُ عنه ، عن النـَبي ِّ صلـَّى الله عليه وسلم قال: ((يـُصـْبـِحُ عـَلى كـُلِّ سـُلامى مـِنْ أحـَدِكـُمْ صـَدَقةُفـَكُل تـَسْبـِيحـَةِ صـَدَقةٌ ،وَ كُل تـَحمِيدة صـَدَقةٌ ، وكُلُ تـَهْـليْلةٌ صـَدَقـَةٌ، وكُلُّ تـَكْبِيْرةِ صـَدقةٌ ، وأمرٌ بالمـَعرُوف صـَدقةٌ ، ونـَهىٌ عـَنِ المـُنْكرِ صـَدقةٌ ويـُجْزئ مـِنْ ذلكَ رَكـْعتـَانِيـَركَعُهُما مـنَ الضـُّحى))  رواه مسلم


Kutoka kwa Abu Dharr (Radhiya Allahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa alihi wa sallam) amesema: ((Kila kiungo katika mwili wenu hupambaukiwa kikihitaji kutolewa sadaka, kwa hiyo kila tasbiyh (kusema ‘SubhaanaAllah’) ni sadaka na kila tahmiyd (kusema ‘AlhamduliLlaah’) ni sadaka na kila tahliyl (kusema ‘La Ilaaha Illa Allah’) ni sadaka  na kila takbiyr (kusema ‘Allahu Akbar’) ni sadaka na kuamrisha mema ni sadaka na kukataza maovu ni sadaka na itamtosheleza (Mtu) kwa Rakaa mbili za Dhuhaa)) [Muslim]


Na Allah Anajua zaidi

0 Comments