Mambo Kumi Miongoni Mwa Yanayosababisha Kupata Mapenzi Ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)

Yafuatayo ni baadhi ya mambo yatakayosababisha kupata mapenzi ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):


Kuwa na iymaan

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):   

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَتَّخِذُ مِن دُونِ اللَّـهِ أَندَادًا يُحِبُّونَهُمْ كَحُبِّ اللَّـهِ ۖ وَالَّذِينَ آمَنُوا أَشَدُّ حُبًّا لِّلَّـهِ ۗ  
Na miongoni mwa watu wako wenye kuchukua asiyekuwa Allaah na kuwafanya kuwa ni wanaolingana (na Allaah) wanawapenda kama kumpenda Allaah. Na wale walioamini wana mapenzi zaidi kwa Allaah. [Al-Baqarah 2: 165].


Kumfuata Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

  
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):


قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللَّـهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّـهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٣١﴾

  Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Mkiwa mnampenda Allaah, basi nifuateni mimi, Atakupendeni Allaah na Atakughufurieni dhambi zenu. Na Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu”. [Aal-‘Imraan: 31]


Kujikurubisha kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa kumdhukuru mno na pia kurejea Kwake kwa kila jambo:

Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):  


 عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ قَالَ قَالَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ (( يَقُولُ اللَّهُ تَعَالَى: أَنَا عِنْدَ ظَنِّ عَبْدِي بِي وَأَنَا مَعَهُ إِذَا ذَكَرَنِي، فَإِنْ ذَكَرَنِي فِي نَفْسِهِ ذَكَرْتُهُ فِي نَفْسِي، وَإِنْ ذَكَرَنِي فِي مَلَإٍ ذَكَرْتُهُ فِي مَلَإٍ خَيْرٍ مِنْهُمْ، وَإِنْ تَقَرَّبَ إِلَيَّ بِشِبْرٍ تَقَرَّبْتُ إِلَيْهِ ذِرَاعًا، وَإِنْ تَقَرَّبَ إِلَيَّ ذِرَاعًا تَقَرَّبْتُ إِلَيْهِ بَاعًا، وَإِنْ أَتَانِي يَمْشِي أَتَيْتُهُ هَرْوَلَةً)) البخاري، مسلم، الترمذي و ابن ماجه

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema, ((Allaah Ta’aalaa, Anasema: Mimi ni vile mja Wangu anavyonidhania. Niko pamoja naye Anaponikumbuka katika nafsi yake, Ninamkumbuka  katika nafsi Yangu, anaponikumbuka katika hadhara, Ninamkumbuka katika hadhara bora zaidi. Na anaponikaribia shibiri Ninamkaribia dhiraa; anaponikaribia dhiraa, Ninamkaribia pima, anaponijia kwa mwendo (wa kawaida) ninamwendea mbio)) [Al-Bukhaariy, Muslim, At-Tirmidhiy na Ibn Maajah]


Kutimiza fardhi kwanza kisha kuzidisha ‘amali za Sunnah:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ قَالَ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((إِنَّ اللَّهَ قَال:َ مَنْ عَادَى لِي وَلِيًّا فَقَدْ آذَنْتُهُ بِالْحَرْبِ، وَمَا تَقَرَّبَ إِلَيَّ عَبْدِي بِشَيْءٍ أَحَبَّ إِلَيَّ مِمَّا افْتَرَضْتُ عَلَيْهِ،  وَمَا يَزَالُ عَبْدِي يَتَقَرَّبُ إِلَيَّ بِالنَّوَافِلِ حَتَّى أُحِبَّهُ، فَإِذَا أَحْبَبْتُهُ كُنْتُ سَمْعَهُ الَّذِي يَسْمَعُ بِهِ، وَبَصَرَهُ الَّذِي يُبْصِرُ بِهِ، وَيَدَهُ الَّتِي يَبْطِشُ بِهَا، وَرِجْلَهُ الَّتِي يَمْشِي بِهَا، وَإِنْ سَأَلَنِي لَأُعْطِيَنَّهُ، وَلَئِنْ اسْتَعَاذَنِي لَأُعِيذَنَّهُ)) البخاري

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amesema: “Atakayemfanyia uadui kipenzi changu Ninatangaza vita dhidi yake. Mja Wangu hanikaribii na kitu chochote Ninachokipenda kama ‘amali nilizomfaridhishia. Na mja Wangu huzidi kunikaribia kwa ‘amali za Sunnah ili nimpende. Ninapompenda, huwa masikio yake yanayosikilizia, macho yake anayoonea, mikono yake anayonyoshea, miguu yake anayotembelea nayo, lau angeniomba kitu bila shaka ningempa, lau angeniomba himaya bila shaka ningelimkinga.”[Al-Bukhaariy]


 Na Ibn Qayyim Al-Jawziyy (Rahimahu Allaah) ametaja katika kitabu chake: Madaarij As-Saalikiyn alama kumi zifuatazo zinazosababisha mapenzi ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):   


1. Kusoma Qur-aan kwa kuzingatia na kufahamu maana yake.


2. Kujikurubisha kwa Allaah ('Azza wa Jalla)  kwa ‘amali za Nawaafil (Sunnah) baada ya yaliyofaridishwa kwani yanamfikisha mtu daraja kubuwa kabisa ya mapenzi. (Kama ilivyotajwa katika Hadiyth ya Qudsiyy hapo juu).


3. Kumdhukuru Allaah katika kila hali; kwa ulimi, moyo, vitendo. Daraja ya mapenzi hulingana na kadiri ya ‘amali za mja. 


4. Kukhiari Anayoyapenda Allaah ('Azza wa Jalla)  kuliko unayoyapenda pale unapoghilibiwa na matamanio yako.


5. Kuufanya moyo wako uzingatie Majina na Sifa Zake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kuzishuhudia, kuzitambua, na kuzifanyia kazi mafunzo yake.


6. Kukumbuka fadhila na neema Zake nyingi, zinazodhihirika na zilofichika, kwani zinapeleka kwenye mapenzi Yake.


7. (Na ajabu zaidi ni) Kuulainisha moyo wako kwa kila hali, kuwa na unyenyekevu, kujidhalilisha unapomwabudu Allaah ('Azza wa Jalla).


8.  Kujipwekeksha Kwake Anapoteremka thuluthi ya mwisho ya usiku kwa kuomba kuokoka, kusoma maneno Yake (Qur-aan), kusimama (katika Qiyaamul-Layl) kwa unyenyekevu na kwa adabu nzuri kisha umalizie kwa kuomba maghfirah na tawbah.


9.  Kushikamana na wenye mapenzi ya kweli katika vikao vyao unufaike na kauli (na mafunzo) yao.


10.  Kujiweka mbali na kila kinachosababisha moyo kuwa mbali na Allaah (‘Azza wa Jalla), na kuu zaidi ni kujiepusha na matamanio yanayopeleka kwenye shirki hasa katika kutafuta mapenzi ya Allaah ('Azza wa Jalla).

0 Comments