Wanaopinga Sifa Za Allaah (Ahlul-Bid'ah) Hawana Dalili Za Msingi

Wanaopinga Sifa Za Allaah (Ahlul-Bid'ah) Hawana Dalili Za Msingi
Shaykh-ul-Islam Ahmad Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah)
Chanzo: Al-Fataawaa al-Hamaawiyyah, ukurasa 19.

Kuna kauli tele kutoka kwa Salaf kuhusiana na suala hili.[1]
Kwa upande mwingine, hakuna herufi hata moja kwenye Kitabu cha Allaah (’Azza wa Jalla), wala Sunnah ya Mtume Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) au Maswahaba wake, au waliokuja baada yao na Maimaam wa Ummah; kauli zao hazikwenda kinyume. Hakuna maandishi kutoka kwao, au hata mfano wa kitu kinachoashiria hilo.
Kamwe hata mmoja hakuwahi kusema kwamba Allaah hayupo juu mbinguni.
Kamwe hata mmoja hakuwahi kusema kwamba Allaah hayupo juu ya kiti Chake cha enzi.
Kamwe hata mmoja hakuwahi kusema kwamba Allaah yupo kila mahali.
Kamwe hata mmoja wakuwahi kusema kuwa kila mahali [poote] ni sawa na Allaah.
Kamwe hata mmoja hakuwahi kusema kwamba Allaah hayupo ndani ya uumbaji, nje ya uumbaji.
Kamwe hata mmoja hakuwahi kusema kwamba ni makosa kuashiria kwa kidole juu kwa Allaah, na kadhalika.
Ukweli ni kuwa imepokelewa Hadiyth kutoka kwa Jaabiyr bin 'Abdillaah (Radhiya Allaahu ’anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) kasema wakati wa khutbah yake ya mwisho:
"Je, nimefikisha? "Wakasema: "Ndiyo." Kisha [baada ya hapo] akapandisha kidole chake akikielekeza mbinguni kisha akakiteremsha na kusema: ”Allaah shuhudia.” [Muslim 1218][1] Yaani ni kauli ambayo inathibitisha Majina na Sifa za Allaah. Hapa chini kunafuatia baadhi ya kauli za Salaf (Radhiya Allaahu 'anhum) ambazo zinaonesha wazi kabisa na dhahiri kuwa Muumbaji wa viumbe yupo juu mbinguni:
1 - Imaam Muhammad bin Is-haaq (Rahimahu Allaah) kasema:
“Juu ya kiti cha enzi yupo Yule ambaye ana Ukuu na Utukufu.” (Al-'Uluww, ukurasa wa 150., kutoka kwa Imaam Adh-Dhahabiy)
2 - Imaam 'Abdur-Rahmaan al-Awzaa'iy (Rahimahu Allaah) kasema:
“Yupo juu ya kiti Chake cha enzi kwa namna ileile ambayo Yeye mwenyewe kaieleza.”(ukurasa 138)
3 - Imaam Hammaad bin Zayd (Rahimahu Allaah) kasema kuhusu Jahmiyyah:
“Hoja yao ni kwamba hakuna mungu yeyote juu ya mbingu.” (ukurasa 146)
4 - Imaam Maalik bin Anas (Rahimahu Allaah) kasema:
“Allaah Yuko juu ya mbingu. Elimu [maarifa] Yake yapo kila mahali na hakuna kitu kinachoepuka [pinga] hilo.” (ukurasa 140)
5 - Kulisemwa kwa Imaam ’Abdullaah bin al-Mubaarak (Rahimahu Allaah):
“ Vipi tutajifunza kumjua Mola wetu?” Akasema:
“Kwa kujua kwamba yupo juu ya mbingu saba na juu ya kiti Chake cha enzi. Hatusemi kama jinsi Jahmiyyah wanavyosema kuwa Yupo hapa duniani.”
6 - Imaam Jariyr adh-Dhabbiy (Rahimahu Allaah) kasema:
“Kauli ya Jahmiyyah inaanza kwa asali na inakwisha kwa sumu. Wanajaribu kusema kwamba hakuna mungu yeyote juu ya mbingu.” (ukurasa. 151)
7 - Imaam 'Aliy al-Madiyniy (Rahimahu Allaah ) kasema:
“Jahmiyyah wanataka kukataa kwamba Allaah Aliongea na Musa, na kwamba Yupo juu ya kiti Chake cha enzi. Naonelea kuwa wanatakiwa kufanya tawbah. Ima watubie au wanyongwe.“ (ukurasa wa 169.)
8 - Imaam Wahb bin Jariyr (Rahimahu Allaah) kasema:
“Jitengeni mbali na fikra za Jahmiyyah. Wanataka kusema kwamba hakuna mungu yeyote juu ya mbingu. Hakuna la zaidi isipokuwa Ibliys ndio kawateremshia wahyi [kuhusu hili]. Si kitu kingine bali ni Ukafiri” (ukurasa 170)
9 - Imaam Abu Zur'ah ar-Raziy (Rahimahu Allaah) kasema:
“Yupo juu ya kiti Chake cha enzi na elimu Yake ipo mahali pote. Laana ya Allaah imshukiye yule atakayesema kitu kingine chochote kinyume na hili.” (ukurasa 203)
10 - Imaam 'Uthmaan bin Sa’iyd ad-Daarimiy (Rahimahu Allaah) kasema:
“Waislamu wamekubaliana kwamba Allaah yupo juu ya kiti Chake cha enzi na juu ya mbingu Zake.” (ukurasa 213)

0 Comments