November 2, 2018

Abu Muusa Al-Ash'ariy (Radhiya Allaahu 'anhu)

Muhammad Faraj Saalim As-Sa’y


Alipowasili mji wa Basra, baada ya kuteuliwa na ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Llaahu ‘anhu) kuwa gavana wa mji huo, Abu Muusa Al-Ash’ariy (Radhiya Llaahu ‘anhu), aliwakusanya watu wa mji huo na kuwahutubia akiwaambia:
"Khalifa wa Waislam ‘Umar bin Al-Khattwaab amenileta kwenu ili nikufundisheni Kitabu cha Mola wenu na mafundisho ya Mtume wenu na ili nikusafishieni barabara".

Watu walipigwa na mshangano kwa sababu wao wanajuwa kuwa kuwafundisha watu Kitabu cha Mwenyezi Mungu na mafundisho ya Mtume wake (Swalla Llaahu ‘‘alayhi wa sallam) ni katika jukumu la gavana, lakini lililowashangaza ni pale aliposema kuwa amekuja pia ili awasafishie barabara.

Huyu ndiye ‘Abdullaah bin Qays (Radhiya Llaahu ‘anhu) maarufu kwa jina la Abu Muusa Al-Ash’ariy.
Huyu ndiye Abu Muusa Al-Ash’ariy (Radhiya Llaahu ‘anhu) ambaye Hasan Al-Baswriy (Radhiya Llaahu ‘anhu) alisema juu yake:
"Hajapata kuja katika mji huu wa Basra mtu mwema kwa watu wake kuliko huyu."

Mara baada ya kusikia kuwa Mtume mpya aliyekuwa akisubiriwa kwa hamu kubwa sana amekwishakuja, Abu Muusa (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliifunga safari ndefu kutoka katika nchi yake ya Yemen na kuelekea Makkah kwa ajili ya kuutafuta ukweli na ili ajiunge na Mtume huyo katika dini hii mpya inayohubiri juu ya kumuabudu Mungu mmoja tu Asiye na mshirika.

Alipoonana na Mtume wa Mwenyeezi Mungu (Swalla Llaahu ‘‘alayhi wa sallam) na kuzitamka shahada mbili, Abu Muusa (Radhiya Llaahu ‘anhu) alirudi nchini kwake Yemen, na haukupita muda mrefu akarudi tena Makkah, lakini safari hii akiwa na watu wa kabila lake wapatao hamsini waliosilimu mkononi mwake wakiwemo ndugu zake wawili, Abu Ruhmu na Abu Burdah (Radhiya Llaahu ‘anhum).

Kuwasili kwake Makkah kulisadifu kuwasili kwa Ja’afar bin Abi Twaalib (Radhiya Llaahu ‘anhu) aliyerudi kutoka nchi ya Uhabeshi, na ilipotolewa amri ya kuhama kwenda Madiynah, Abu Muusa (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa mionogni mwa wa mwanzo kuhajir.

Tokea siku hizo, Abu Muusa (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa msitari wa mbele katika kuipigania dini hii kwa hali na mali.
Abu Muusa (Radhiya Llaahu ‘anhu) ni mchanganyiko wa ajabu; alikuwa mpiganaji vita hodari sana anapolazimika, jambo lililomfanya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘‘alayhi wa sallam) aseme juu yake:
"Bwana wa mashujaa ni Abu Muusa".

Abu Muusa (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa pia mtu anayependa amani zaidi kuliko vita. Alikuwa akijulikana kuwa ni mtu mwema sana na mcha Mungu, na alikuwa mwingi wa hekima na hodari wa kutoa uamuzi wenye kusibu.

Alipigana vita vingi chini ya uongozi wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘‘alayhi wa sallam), na baada ya kufa kwake (Swalla Llaahu ‘‘alayhi wa sallam) alipigana chini ya Makhalifa wake watukufu (Radhiya Llaahu ‘anhum).
Hebu tumsikilize Abu Muusa (Radhiya Llaahu ‘anhu) akituhadithia juu ya mojawapo ya siku alizoishi na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘‘alayhi wa sallam):
"Tulikuwa safarini katika vita pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), na ulipoingia usiku tukasimamisha msafara kwa ajili ya mapumziko, na ghafla Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akatoweka.
Nikatoka kumtafuta kwa kuhofia asije akadhuriwa, maana tulikuwa vitani. Nikamuona mmoja katika Maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) naye pia akitafuta kile mimi nilichokuwa nikitafuta. Tulipokuwa tumesimama, ghafla akatokea mbele yetu Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), tukamuambia:
"Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, sisi tumo vitani, na hatuaminishi kukuacha peke yako wasije wakakudhuru maadui. Ukiwa na haja yoyote ile, mwambie mmoja wetu afuatane nawe.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akatuambia:
"Nilisikia sauti kama sauti ya nyuki, akanijia aliyenijia kutoka kwa Mola wangu Mtukufu, akanitaka nichaguwe moja kati ya mawili; ama waingie nusu ya umma wangu Peponi au nipewe uwezo wa kuwaombea shifaa. Nikachagua kuwaombea Shifaa kwani nilijuwa kuwa kwa kuwaombea shifaa wataingia wengi zaidi Peponi.
Akanitaka tena nichaguwe baina ya kuingia theluthi ya umma wangu Peponi na baina ya kuwaombea shifaa. Nikachagua kuwaombea shifaa, kwa sababu nilijuwa kuwa wataingia wengi zaidi".
Anasema Abu Muusa (Radhiya Llaahu ‘anhu):
"Tukamuambia:
"Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu; muombe Mwenyezi Mungu Atujaalie tuwe miongoni mwa wanaostahiki shifaa yako".
Anasema Abu Muusa (Radhiya Llaahu ‘anhu):
"Akatuombea du’aa."

Abu Muusa (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikuwa miongoni mwa Maswahaba waliokataa kujiingiza katika vita vya wenyewe kwa wenyewe baina ya majeshi ya ‘Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) na ya Mu’aawiyah (Radhiya Llaahu ‘anhu), na katika mazungumzo ya amani baina yao, watu wa upande wa ‘Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhu) walipendekeza achaguliwe Abu Muusa kuuwakilisha upande wao.

Abu Muusa (Radhiya Llaahu ‘anhu) alikufa katika mwaka wa arubaini baada ya Hijra akiwa na umri wa miaka sitini na mitatu.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only