November 30, 2018

Swalaat-un-Naariyah Ni Nini? Na Je, Yafaa Kishari'ah?

بسم الله الرحمن الرحيم

Kumezuka Du'aa maarufu iliyoenea haswa miaka ya karibuni iitwayo Swalaatun Naariyah, Du'aa hiyo imeenea katika jamii yetu ya Kiswahili, watu wameshughulishwa nayo. Na la kusikitisha zaidi ni kwamba inaaminiwa sana hata imekuwa ni ibada kubwa ya kutegemewa mtu kutakabaliwa haja zake. Wanaacha kutumia du'aa zilizo sahihi na kutumia hii ambayo ni uzushi na juu ya hivyo ina maneno ya shirk.
Du'aa hiyo husomwa hivi:
''ALLAHUMA SWALLI SWALAATAN KAAMILATAAN, WASALIM SALAAMAN TAAMMAN, 'ALAA SAYYIDINA MUHAMMADIN LADHIY TANHALLU BIHIL 'UQADI, WATANFARIJU BIHIL KURAB, WATUQDHWA BIHIL HAWAAIJ, WATUNAALU BIHI-R-RAGHAAIB, WA HUSNUL KHAWAATIM, WA YUSTASQAL GHAMAAM, BI WAJHIL KARIYM, WA 'ALAA AALIHI WASWAHBIHI FI Y KULLI LAMHATIN WA NAFAS, BI'ADADI KULLI MA'ALUUMIN LAK''
Du'a a hii huwa yasomwa mara 4444 (Elfu nne, mia nne na arobaini na nne), nayo hujulikana sana kama SWALAATUN NAARIYAH. Du'aa hii inaaminika kuwa imeanzia huko Bara Hindi na haswa India. Husomwa zaidi wakati mtu anapopatwa na Matatizo yake ya kidunia, mikosi, majanga n.k.

Sasa nini HUKUMU yake kishari'ah? Dini inasemaje kuhusiana na Du'aa ya mfumo huu?
Je, nini maana ya hayo maneno hapo juu, na je, kuna aina yoyote ya ushirikina ndani ya maneno hayo?
Je, kuna ubaya gani kusoma ikiwa hakuna shirki ndani yake? Kwa maana ni aina ya Utajo ambao ndani yake kuna kumtaja Allaah na pia watu hukusanyika pamoja na kuwa karibu na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ili kuondosha Msiba kwa kumuomba. 
Jawabu Na Hukmu:
Kwanza maana au tarjama ya hiyo Du'aa ni hii: ''EWE MOLA, MPE REHMA ILIYOKAMILIKA NA AMANI ILIYOTIMU BWANA WETU MUHAMMAD, KWA FADHILA ZAKE (MTUME Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)VIZUIZI VYOTE VINAONDOKA, MAZONGE  YANAPOA, NA SHIDA ZOTE ZATATULIKA, NA MAHITAJI YAKIDHIKA, NA MWISHO MWEMA WAPATIKANA NA KWA FADHILA ZAKE YULE MWENYE USO MTUKUFU, MAWINGU (MVUA) HUOMBWA KUNYESHA,  NA RAHMAH NA AMANI ZIWE JUU YA AHLI ZAKE NA MASWAHABA WAKE  KWA KILA MUDA NA KILA PUMZI, KWA IDADI YA KADIRI YA ELIMU YAKO''.
Maana ya maneno haya kwanza yanajiweka wazi kuonyesha Uzushi uliomo katika Du'aa hii.
Pili, Du'aa hii imekusanya maneno mengi yasiyokubalika katika Uislamu na yanayopelekea katika shirki. Ni vizuri sana mtu kujiepusha na jambo kama hili kwa sababu zifuatazo:
1- Du'aa hii husomwa wakati wa matatizo, nalo jambo hili halijathibiti na linahitaji dalili; kinyume chake ni Uzushi.
2- Inasomwa kwa idadi maalum, ambayo ni  mara 4444, ambao huu ni muundo potofu  wa Uzushi wenye idadi katika 'ibaadah.
3- Inatakiwa kusomwa kwa muundo wa kukusanyana watu, nalo hili ni jambo lisilokubalika na uzushi katika tendo la 'ibaadah.
4- Inakusanya maneno ambayo yanakwenda kinyume na dini, na ambayo yanavuka mpaka katika kumtukuza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallamna kumpa sifa ambazo anastahiki nazo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) pekee, mfano sifa zile zilizohusishwa na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwenye hiyo Du'aa, nazo ni: ''KWA FADHILA ZAKE (MTUME Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) SHIDA ZA WATU KUTATULIWA, VIZUIZI KUONDOLEWA, MAZONGE (MISUKOSUKO) KUPOOZWA, MAHITAJI KUKIDHIWA NA MWISHO MWEMA WA DUNIA AU AKHERA KUPATIWA!!''
5- Haya yote ni mambo ambayo yanaonyesha kumpa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam uwezo ambao si wake na asiostahiki.  Na sifa hizo za kuweza kuyafanya yote hayo, ni sifa tu anazoweza kuzifanya Allaah na wala si kiumbe Wake yeyote!  Kwa hiyo, Du'aa hii inapelekea katika USHIRIKINA na haifai kabisa kwa Muislam kuisoma wala kushiriki ndani yake.
Allaah Anasema kumwamuru ( Mtume Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)awaambie Makafiri wa Makkah((Sema: Mimi sikumilikiini kukudhuruni wala kuwaongoeni))  Kwa mujibu wa maneno ya Allaah tunapata ushahidi kuwa Mtume(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hana uwezo wa kumsaidia  mja wala kumuongoza au kumpoteza, hayo yote yako katika uwezo wake Allaa(Subhaanahu wa Ta'aalaa)  pekee.
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) naye katika kuukaripia uzushi anasema: ((Yeyote atakayezusha chochote  katika jambo letu hili (UISLAM), basi hilo alizushalo hurejeshewa nalo mwenyewe)) [Imesimuliwa na Maimaam Al-Bukhaariy na Muslim]
Kwa shahidi hizo hapo juu, ndugu Waislam jichungeni mno na aina zote za uzushi na shirki, hakika mambo hayo yanapelekea katika maangamizi na upotofu. Tumtiini Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kumpenda ilivyo Mtume wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallamlakini tusivuke mipaka katika mapenzi hayo tukaja kujikuta tunaingia katika shirk.
Wa Allaahu A’lam

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only