21-Umuhimu Wa Tawhiyd Na Fadhila Zake: Tawhiyd Ni Sharti Ya Kupata Shafaa’ah Ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)

Umuhimu Na Fadhila Za Tawhiyd

21-Tawhiyd Ni Sharti Ya Kupata Shafaa’ah Ya
Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
Sharti la kwanza kuweza kupata Shafaa’ah Siku ya Qiyaamah ni kuthibitisha Tawhiyd. Hadiyth ya Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema:

قُلْتُ يَا رَسُولَ اللهِ مَنْ أَسْعَدُ النَّاسِ بِشَفَاعَتِكَ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ؟ قَالَ رَسُولُ اللهِ صَلى اللهُ عليهِ وَسَلَّمَ: ((لَقَدْ ظَنَنْتُ يَا أَبَا هُرَيْرَةَ أَنْ لا يَسْأَلَني عَنْ هذَا الْحَدِيِثِ أَحَدٌ أَوَّلَ مِنْكَ لِما رَأَيْتُ مِنْ حِرْصِكَ عَلَى الْحَدِيثِ أَسْعَدُ النَّاسِ بِشَفَاعَتِي يَوْمَ الْقِيَامَةِ مَنْ قَالَ: لا إِلهَ إِلاَّ اللهُ خَالِصَاً مِنْ قَلْبِهِ أَوْ نَفْسِهِ))
“Nilisema: Ee Rasuli wa Allaah! Nani atakayefurahika kabisa kwa Shafaa’ah (uombezi) wako Siku ya Qiyaamah: Akasema Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam): ((Nilidhani ee Abaa Hurayrayh kwamba hakuna yeyote asiyekuwa wewe atakayeniuliza maelezo haya kwa vile jinsi nilivyoona himma yako juu ya jambo hili. Atakayefurahika zaidi kati ya watu kwa Shafaa’ah yangu Siku ya Qiyaamah ni atakayesema: laa ilaaha illa Allaah – hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah, kwa niyyah safi moyoni mwake au nafsi yake)). [Al-Bukhaariy]

Na Hadiyth ya ‘Abdullaah bin ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa):

قال النَّبيُّ صلى الله عليه وسلم: ((إِنَّ الشَّمْسَ تَدْنُو يَوْمَ القِيَامَةِ حَتَّى يَبْلُغَ العَرَقُ نِصْفَ الأُذُنِ، فَبَيْنَمَا هُمْ كَذَلِكَ اسْتَغَاثُوا بِآدَمَ، ثُمَّ بِمُوسَى، ثُمَّ بِمُحَمَّدٍ صلى الله عليه وسلم فَيَشْفَعُ لِيُقْضَى بَيْنَ الخَلْقِ، فَيَمْشِي حَتَّى يَأْخُذَ بِحَلقَةِ البَابِ، فَيَوْمَئِذٍ يَبْعَثُهُ اللهُ مَقَامًا مَحْمُودًا، يَحْمَدُهُ أَهْلُ الجَمْعِ كُلُّهُمْ))
Amesema: “Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakika jua litakaribia Siku ya Qiyaamah mpaka majasho ya watu yatafikia karibu na masikio. Watakapokuwa katika hali hiyo, wataomba msaada kwa Aadam, kisha kwa Muwsaa kisha kwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam). Ataomba Shafaa’ah kwa Allaah ili Ahukumu baina ya viumbe Vyake. Ataendelea mpaka atakamata kikamatio cha mlango. Siku hiyo basi Allaah Atamuinua Maqaaman Mahmuwdaa [cheo cha kusifika] na watu wote wa mkusanyiko watamsifu)). [Al-Bukhaariy]

Shafaa’ah hiyo ndiyo Maqaaman Mahmuwdaa ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

وَمِنَ اللَّيْلِ فَتَهَجَّدْ بِهِ نَافِلَةً لَّكَ عَسَىٰ أَن يَبْعَثَكَ رَبُّكَ مَقَامًا مَّحْمُودًا ﴿٧٩﴾
Na katika usiku, amka uswali (tahajjud) kuisoma (Qur-aan); ni ziada ya Sunnah kwako Asaa Rabb wako Akakuinua cheo kinachosifika. [Al-Israa: 79]

Ama makafiri ambao duniani waliwaelekea wengine kuwaomba na kutaka uombezi kwao wakakanusha Tahwiyd ya ‘Uluwhiyyah (Kumpwekesha Allaah katika ‘ibaadah):

وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ وَيَقُولُونَ هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ ۚ قُلْ أَتُنَبِّئُونَ اللَّـهَ بِمَا لَا يَعْلَمُ فِي السَّمَاوَاتِ وَلَا فِي الْأَرْضِ ۚ سُبْحَانَهُ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ﴿١٨﴾
Na wanaabudu pasi na Allaah ambavyo haviwadhuru wala haviwanufaishi na wanasema: “Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah.” Sema: “Je, mnamjulisha Allaah kwa yale Asiyoyajua katika mbingu na ardhini?” Subhaanah! (Utakasifu ni Wake) na Ametukuka kwa ‘Uluwa kwa yale yote wanayomshirikisha. [Yuwnus: 18]


Huko Aakhirah, hawatopata Shafaa’ah ya yeyote yule kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

فَمَا تَنفَعُهُمْ شَفَاعَةُ الشَّافِعِينَ﴿٤٨﴾
Basi haitowafaa uombezi wowote wa waombezi. [Al-Muddath-thir: 48]


Juu ya hivyo hao wanaowaabudu watakanusha kuabudiwa kwao:

وَالَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِهِ مَا يَمْلِكُونَ مِن قِطْمِيرٍ ﴿١٣﴾
Na wale mnaowaomba badala Yake hawamiliki hata kijiwavu cha kokwa ya tende.


إِن تَدْعُوهُمْ لَا يَسْمَعُوا دُعَاءَكُمْ وَلَوْ سَمِعُوا مَا اسْتَجَابُوا لَكُمْ ۖ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكْفُرُونَ بِشِرْكِكُمْ ۚ وَلَا يُنَبِّئُكَ مِثْلُ خَبِيرٍ ﴿١٤﴾

Mkiwaomba, hawasikii maombi yenu, na hata wakisikia, hawatakuitikieni.  Na Siku ya Qiyaamah watakanusha ushirikina wenu, na wala hakuna atakayekujulisha vilivyo kama Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika. [Faatwir: 13-14]


0 Comments