073-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Yanayohusiana Na Niya Ya Kutayammam

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

Mlango Wa Twahara

073-Yanayohusiana Na Niya Ya Kutayammam


·       
Niya ya kuondosha hadathi inatosheleza kuruhusika kuswali

Kauli za Maulamaa zilizo sahihi zaidi zinasema kwamba tayamumi inasimama mahala pa maji moja kwa moja. Yanayoruhusika kwa maji ndiyo yale yale yanayoruhusika kwa tayamumi, na utwahara wake huendelea kama unavyoendelea utwahara wa maji. Akitayamamu kwa ajili ya Swalaah ya Sunnah, anaweza pia kuswalia Swalaah ya faradhi na kinyume chake. Hii ndiyo kauli ya Maulamaa wengi kinyume na Maalik Allaah Amrehemu. [Al-Majmu’u (2/255), Al-Mughniy (1/158), Majmu’u Al-Fataawaa (12/436) na Al-Mabsuutw (1/117)]

Sheikh wa Uislamu anasema: [Majmu’u Al-Fataawaa (21/436)]
“Kauli hii ndio sahihi, na ndiyo iliyoashiriwa na Qur-aan, Sunnah na akili. Tunaona kwamba Allaah Ameifanya tayammum inatwaharisha kama Alivyoyafanya maji Akatuambia:
((فتيمموا صعيدا طيبا فامسحوا بوجوهكم وأيديكم منه ما يريد الله ليجعل عليكم من حرج ولكن يريد ليطهركم))
(( Basi ukusudieni mchanga mzuri, panguseni kwao nyuso zenu na mikono yenu. Allaah Hataki kuwafanyieni uzito lakini Anapenda kukutwaharisheni )). [Al-Maaidah (5:6) ]

Kwa hiyo, mwenye kusema kwamba mchanga hautwaharishi hadathi, basi amekhalifu Qur-aan na Sunnah. Na ikiwa unatwaharisha hadathi, haiwezekani hadathi ikaendelea kuwepo, kwani Allaah Amewatwaharisha Waislamu hadathi kwa tayamumi. Tayamumi inaondosha hadathi na inamtwaharisha mwenye hadathi, lakini uondoshaji huu ni wa muda mpaka pale atakapoweza kuyatumia maji. Tayamumi ni badali ya maji, nayo inabakia ni kitwaharisho madhali maji yamekuwa vigumu kupatikana”.

Ninasema: “Tayamumi imewekwa kisharia kwa ajili ya Swalaah, twawafu, kusoma Qur-aan, kugusa Msahafu na mengineyo yanayoruhusika mtu anapokuwa na wudhuu au baada ya kuoga madhali maji yamekuwa vigumu kupatikana. Mwenye kunuwiya kwa tayamumi yake kuondosha hadathi, ni halali kwake kufanya yale yote anayoruhusika anapokuwa na wudhuu na baada ya kuoga. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”.

Mwenye Kutayammamu Kwa Niya Ya Kuondosha Janaba, Je Itamtosheleza Na Wudhuu Pia?

Mwenye kutayamumi kwa niya ya kuondosha janaba, niya hiyo itamtosheleza na wudhuu pia kwa mujibu wa kauli sahihi ya Maulamaa kama Abuu Haniyfah na Ash Shaafi’iy. [Al-Mughniy (1/166)]

Na hii ni kwa mambo mawili:

1- Twahara ya viwili hivi ni moja. Inapoondoka moja, humwondosha mwenzake kama mkojo na kinyesi.

2- Tayamumi ni badali ya utumiaji maji, hivyo huchukua hukmu yake. Lenye nguvu zaidi ni kuwa kuoga, hutosheleza na wudhuu pia, na vile vile tayamumi.

Ama mwenye kutayamumi kwa niya ya kuondosha hadathi ndogo, je niya itatosheleza kuondosha janaba pia? Jibu hapa litaangaliwa; mwenye kuliangalia suala mtizamo wa sababu ya kwanza, jibu lake litakuwa ndiyo. Ama mwenye kuliangalia kwa mtizamo wa kuwa tayamumi ni badali ya maji, basi atazuia.

Maalik, Abuu Thawr, Mahanbali na Ibn Hazm, [Al-Mughniy (1/166) na Al-Muhallaa (2/138)]…..wao wanasema kwamba niya ya kimoja, haitoshelezi kingine kutokana na ujumuishi wa kauli ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
(( إنما الأعمال بالنيات، وإنما لكل امرئ ما نوى))
((Hakika matendo ni kwa niya, na kila mtu ni kwa lile alilolinuwiya)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (namba moja)].

0 Comments