Umuhimu Wa Kuwa Na Rafiki Mwema


Bismillahir-Rrahmaanir-Rahiym. Alhamdulillaahi Rabbil Aalamin, waswalatu wassalam alaa RasuliLLaahi (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Ningependa kuwahusia enyi ndugu zangu kuhusu umuhimu wa kuwa na marafiki wema, kwa vile ni kawaida kwa  sisi binaadamu kuhitaji marafiki.

Kuchagua rafiki mzuri ni lazima kwa ajili ya kuhifadhi dini yetu. Waislamu wakiwa na tabia nzuri na wenye kufuata njia ya Allaah, basi uislamu utakuwa na nguvu, ni hivyo ndivyo inavyotakikana. Kufanya urafiki na watu wema wenye tabia nzuri, ni mojawapo ya njia ya kutufanya sisi  kuwa kwenye njia iliyonyooka.

Nabiy Muhammad ((Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)) amesema: “Mtu yamkini kufuata dini ya rafiki yake, kwa hivyo muangalie unaemfanya rafiki.” [Abu Dawuud na At-Tirmidhiy].

Lazima tuchague marafiki ambao wako radhi na dini yetu na tuepukane na wale ambao hawako radhi na dini yetu. Na tukiona marafiki zetu matendo yao sio mazuri, ni lazima tuepukane nao kwasababu tunaweza tukaiga tabia zao ambazo zinakwenda kinyume na dini yetu. Kutangamana na marafiki ambao wanakwenda kinyume na njia ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), inaweza ikatubadilisha tabia, fikra na mwenendo wetu. Lakini vile vile inatupasa kuwatendea wema.

Katika Hadiyth, Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema: "Mfano wa rafiki mwema na rafiki mbaya ni kama ule wa muuzaji wa misk na mhunzi. Basi kwa muuzaji wa misk, imma atakunusisha, au utanunua kwake ama angalau utafurahia harufu nzuri kwake. Na kwa yule mhunzi, imma atakuchomea nguo au utapata harufu mbaya kutoka kwake.” [Al-Bukhaariy na Muslim].


Katika tafsiri ya Hadiyth hii, Imam An-Nawawiy alisema: Nabiy ((Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)) alilinganisha rafiki mzuri na muuzaji misk kwasababu, kwa rafiki mzuri mwenye tabia ya upole, na elimu, utapata faida kwake. Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitukataza kukaa na wale wenye kufanya maovu.

Mwanachuoni mmoja amesema: “Kuweka uhusiano mzuri na watu wema, matokeo yake ni kupata elimu iliyo na faida, tabia nzuri, na matendo mema, ambapo kuweka uhusiano na waliopotoka, huzuia hayo mema yote.”

Allaah Anasema katika Qur-aan:

وَيَوْمَ يَعَضُّ الظَّالِمُ عَلَىٰ يَدَيْهِ يَقُولُ يَا لَيْتَنِي اتَّخَذْتُ مَعَ الرَّسُولِ سَبِيلًا ﴿٢٧﴾
Na siku dhalimu atakapotafuna mikono yake akisema: “Laiti ningeshika njia pamoja na Rasuli. 

يَا وَيْلَتَىٰ لَيْتَنِي لَمْ أَتَّخِذْ فُلَانًا خَلِيلًا ﴿٢٨﴾
 “Ee ole wangu! Laiti nisingelimfanya fulani kuwa rafiki mwandani.”


لَّقَدْ أَضَلَّنِي عَنِ الذِّكْرِ بَعْدَ إِذْ جَاءَنِي ۗ وَكَانَ الشَّيْطَانُ لِلْإِنسَانِ خَذُولًا ﴿٢٩﴾
 “Kwa yakini amenipoteza mbali na Ukumbusho baada ya kunijia.” Na shaytwaan kwa insani daima ni mwenye kutelekeza.  [Al-Furqaan 25: 27-29].


Allaah (‘Azza wa Jalla) Anasema pia:
 الْأَخِلَّاءُ يَوْمَئِذٍ بَعْضُهُمْ لِبَعْضٍ عَدُوٌّ إِلَّا الْمُتَّقِينَ﴿٦٧﴾
  Rafiki wapenzi Siku hiyo watakuwa maadui wao kwa wao isipokuwa wenye taqwa. [Az-Zukhruf 43: 67].


Ibn Kathiyr ameeleza kuhusu Aayah hii, kisa ambacho kimepokewa na ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa, urafiki wowote ambao si kwa ajili ya Allaah, hugeuzwa ukawa wa uadui isipokuwa chochote kilichokuwemo kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). 

Watu wawili ambao ni marafiki kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa); mmoja wao akifariki, hupewa bishara nzuri kuwa amejaaliwa kuingi Jannah (Peponi), basi humkumbuka rafiki yake na kumuombea dua akisema: “Ee Rbb wangu, rafiki yangu alikuwa akiniamrisha kukutii na kumtii Rasuli Wako Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na alikuwa akiniamrisha kufanya mema na alikuwa akinikataza kufanya maovu. Na aliniambia kuwa nitakutana na Wewe. Ee Rabb wangu, basi usimuache kupotea baada ya mimi kuondoka, na muoneshe haya ulionionesha mimi, Na Uwe Radhi naye kama Ulivyoridhika na mimi.” Basi ataambiwa: “Laiti ungelijua aliyoandaliwa rafiki yako, basi ungefurahi sana na ungelia kidogo.” Kisha rafiki yake akifariki, roho zao zinakusanywa, na wote wanaambiwa watoe maoni kuhusu kila mmoja. Basi kila mmoja anamwambia mwenzake: “Ulikuwa ndugu mzuri kabisa, mwenzangu mzuri kabisa, na rafiki mzuri kabisa.” Na mmoja wa wale marafiki wawili wasioamini anapokufa na kupewa bishara za moto wa Jahannam, humkumbuka rafiki yake na kusema: “Ee Rabb wangu, rafiki yangu alikuwa akiniamrisha nikuasi na nimuasi Rasuli Wako Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na alikuwa akiniamrisha kufanya maovu na kunikataza kufanya mema, na akaniambia sitokutana na wewe. Ee Rabb wangu, usimuongoze baada ya mimi kufa, na Muoneshe haya ulonionesha mimi, na Usiwe Radhi nae kama ambavyo Huko Radhi na mimi.” Kisha yule rafiki mwengine akifa na nyoyo zao zikikusanywa, wote wawili wanaambiwa watoe maoni kuhusu kila mmoja. Basi kila mmoja anamwambia mwenzake: “Ulikuwa ndugu mbaya kabisa, mwenzangu mbaya kabisa, na rafiki mbaya kabisa.” 

Kwa hivyo, ni katika urafiki mwema ndio Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Humuokoa aliyepotea na kumuongoza aliyekosa. Faida ya kutangamana na marafiki wema ni kubwa kupita kiasi na In Shaa Allaah itakuwa wazi zaidi kwetu siku ya Qiyaamah, kama tulivyoona kwenye Aayah na visa tulivyotaja.

Na katika Hadiyth nyengine pia, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuamrisha  kutangamana na Muumin peke yake. [Abu Dawuud na At-Tirmidhiy] Na pia, mtu atakuwa na wale awapendao. [Al-Bukhaariy na Muslim].

Kwa hivyo, tukiwapenda na kuwaandama waliopotoka, lazima tujiogopee mwisho wetu.

‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alisema: "Tangamana na watu wema wapole, utakuwa mmoja wao; na epukana na watu waovu usalimike na maovu yao."

Muumin ni kioo cha ndugu yake, akiona makosa ya Muumin mwenzake inampasa amueleze kwa uzuri na kumsaidia kurekebisha kosa hilo.

Ibn Hazm amesema: “Yeyote anayekukosoa, anajali urafiki wako. Na yeyote ambae anachukulia wepesi makosa yako, basi hajali urafiki wako.”

Kwa hivyo ikiwa tunafikiria kuhusu mwisho wetu, lazima tutambue kuwa,wale ambao wanatuepusha na Kumkumbuka Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na kumfuata Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wale ambao hawatukumbushi Swalaah zetu na wala hawatupi mawaidha mazuri kuhusu Dini yetu, basi wao kweli ni maadui si marafiki zetu. 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala ) Anasema:

وَمَن يَتَوَلَّ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَالَّذِينَ آمَنُوا فَإِنَّ حِزْبَ اللَّـهِ هُمُ الْغَالِبُونَ ﴿٥٦﴾
Na atakayemfanya Allaah kuwa ni Mlinzi na Rasuli Wake na wale walioamini, basi hakika kundi la Allaah ndio washindi.  [Al-Maaidah: 56].


Hitimisho

Namuomba Allaah Atujaaliye tuwe miongoni mwa waja Wake wema na Atupe katika marafiki ambaowatatuepusha na ghadhabu Yake, na watakaotuelekeza kwenye njia ya Allaah na Radhi Zake  NamuombaAllaah Atujaaliye tuwe miongoni mwa waja Wake wema ambao watakutana kwa furaha na kusifianakama kile kisa tulichokisikia. Na Atujaaliye tuingie katika  Jannah Yake ya Firdaus kwa Rahmah Zake.  Aamiyn

0 Comments