Kila Nafsi Itaonja Mauti Na Hakuna Atakayebakia Isipokuwa Allaah سبحانه وتعالى

Anasema Allaah سبحانه وتعالى:

  كُلُّ نَفْسٍ ذَآئِقَةُ الْمَوْتِ وَإِنَّمَا تُوَفَّوْنَ أُجُورَكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ فَمَن زُحْزِحَ عَنِ النَّارِ وَأُدْخِلَ الْجَنَّةَ فَقَدْ فَازَ وَما الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلاَّ مَتَاعُ الْغُرُور   
((Kila nafsi itaonja mauti. Na bila ya shaka mtapewa ujira wenu kamili Siku ya Qiyaamah. Na atakayeepushwa na Moto na akatiwa Peponi basi huyo amefuzu. Na maisha ya dunia si kitu ila ni starehe ya udanganyifu)) [Al-'Imraan: 185]

Tokea kuumbwa kwa Nabii Aadam عليه السلام   hadi  leo na mpaka siku ya Qiyaamah hakuna kiumbe kitakachobakia isipokuwa Mwenyewe Mola Mtukufu kama Anavyosema:
 كُلُّ شَيْءٍ هَالِكٌ إِلَّا وَجْهَهُ
((Kila kitu kitaangamia isipokuwa Yeye)) [Al-Qaswas: 88]

Vile vile Anasema Allaah سبحانه وتعالى :

 ((كُلُّ مَنْ عَلَيْهَا فَانٍ))
 ((وَيَبْقَى وَجْهُ رَبِّكَ ذُو الْجَلَالِ وَالْإِكْرَام))

((Kila kilioko juu Yake kitatoweka))
((Na Atabakia Mwenyewe Mola wako  Mwenye utukufu na ukarimu)) [Ar-Rahmaan: 26-27]

Baada ya kupulizwa Swuur (baragumu) siku ya Qiyaamah viumbe vyote vitakufa kwa mpangilio Anaoutaka Mwenyewe Allaah سبحانه وتعالى. Kisha mwisho atabakia Malakul Mawt (Malaika mtoaji roho) na Allaah سبحانه وتعالى. Kisha Allaah سبحانه وتعالى  Atamuamrisha Malakul Mawt ajitoe roho yake mwenyewe. Atakapokufa Malakul Mawt Atabakia Allaah سبحانه وتعالى   Pekee wa Mwanzo na wa Mwisho, Al-Hayyul-Qayyuum (Mwenye uhai wa maisha, Msimamia kila jambo). Allaah سبحانه وتعالى  Siku hiyo Atazikusanya ardhi na mbingu katika Mikono Yake,

  ((وَالْأَرْضُ جَمِيعًا قَبْضَتُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَالسَّماوَاتُ مَطْوِيَّاتٌ بِيَمِينِهِ))

((Na Siku ya Qiyaamah ardhi yote itakuwa mkononi Mwake, na mbingu zitakunjwa katika mkono wake wa kuume)) [Az-Zumar: 67]

Na Hadiyth kutoka kwa Ibn 'Umar رضي الله عنه   kwamba:

  ((يطوي السموات والأرض بيده، ثم يقول: أنا الملك، أنا الجبار، أنا المتكبر، أين ملوك الأرض؟ أين الجبارون؟ أين المتكبرون؟))  مسلم

((Allaah Atazikunja mbingu kwa Mikono Yake, kisha Atasema, Mimi ni Mfalme, Mimi ni Al-Jabbaar (Mwenye Kushurutisha), wako wapi wafalme wa dunia? Wako wapi majabbaar (wanaolazimisha), wako wapi wanaotakabari?)) [Muslim]

Hapo tena Atauliza mara tatu: 
  ((لِّمَنِ الْمُلْكُ الْيَوْمَ))
((Ufalme ni wa nani leo?)) [Ghaafir:16]

Hakutakuwa na mtu wa kujibu, basi Atajibu Mwenyewe,
  ((لِلَّهِ الْوَاحِدِ الْقَهَّار))  

((Ni wa Allaah Mmoja Mtenda Nguvu)) [Ghaafir 16]

Na hapo tena ndipo kila mtu atakuta hesabu yake ya matendo aliyoyatenda duniani ikiwa ni mema au mabaya, hakuna atakayedhulumiwa hata chembe, kwani Allaah سبحانه وتعالى  Atahukumu kwa uadilifu baina ya viumbe Vyake. Kila jema Atalilipa kwa mara kumi na kila ovu atahesabiwa mja kwa ovu moja.

  ((الْيَوْمَ تُجْزَى كُلُّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ لَا ظُلْمَ الْيَوْمَ إِنَّ اللَّهَ سَرِيعُ الْحِسَابِ))  

((Leo kila nafsi italipwa kwa iliyochuma. Hapana dhulma leo. Allaah  ni Mwepesi wa kuhisabu)) [Ghaafir: 17]


************

0 Comments