Majuto Ya Nafsi - 1

Baada ya kuitwaharisha nafsi kwa kuomba Tawbah ya kweli, nafsi itakuwa katika hali ya kuridhiwa na Mola wake, na kutoka hapo tena Muumin  aendelee kurudi kwa Mola wake kila mara anapokosea, bila kuvuka mipaka, na huku akijishughulisha na vitendo vyema kwa khofu ya kuiharibu hali yake ya nafsi akaja kujuta siku atakapokutana na Mola wake.

}}وَأَنِيبُوا إِلَى رَبِّكُمْ وَأَسْلِمُوا لَهُ مِن قَبْلِ أَن يَأْتِيَكُمُ الْعَذَابُ ثُمَّ لَا تُنصَرُونَ{{

{{Na rejeeni (kutubu) kwa Mola, na jisalimisheni Kwake kabla haijakufikieni adhabu kisha hamtonusuriwa.}} [Az-Zumar: 54].

Maana; kimbilieni kuomba Tawbah na kufanya mema kabla ghadhabu za Allaah سبحانه وتعالى hazijakufikieni. 

Kisha zikaendelea aya kutuhimiza kufuata Qur-aan ambayo ndio uongofu wetu kamili tunaohitaji, kwani humo yamo tuliyoamrishwa na tuliyokatazwa kutenda. Na kutofuata Qur-aan humpelekea mtu akawa yumo mbioni katika mambo ya dunia tu bila ya kufikiria Aakhirah, na hivyo yanapomjia mauti kwa ghafla basi huwa hawezi tena kujisaidia kwani hakuna yeyote wala chochote kile alichokuwa akishughulika nacho duniani kuwa kitamfaa wakati huo. 

}}وَاتَّبِعُوا أَحْسَنَ مَا أُنزِلَ إِلَيْكُم مِّن رَّبِّكُم مِّن قَبْلِ أَن يَأْتِيَكُمُ العَذَابُ بَغْتَةً وَأَنتُمْ لَا تَشْعُرُونَ{{

{{“Na fuateni yaliyo mazuri zaidi (katika) yale mliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wenu kabla haijakufikieni adhabu ghafla na hali nyinyi hamtambui.”}}  [Az-Zumar: 55].

Na hapo tena ndipo mtu anapojuta majuto makubwa yasiyomsaidia, kwani atatamani kurudi tena duniani atende mema lakini wapi! Kama Anavyosema Allaah سبحانه وتعالى:
}}هَيْهَاتَ هَيْهَاتَ{{
{{Hayawi! Hayawi}} [Al-Muuminuwn: 36].

 Majuto ya nafsi  yanaelezewa  katika aya zifuatazo:

}} أَن تَقُولَ نَفْسٌ يَا حَسْرَتَى علَى مَا فَرَّطتُ فِي جَنبِ اللَّهِ وَإِن كُنتُ لَمِنَ السَّاخِرِينَ{{

{{Isije nafsi ikasema: “Ee majuto (makubwa mno) yangu kwa yale niliyokusuru katika upande wa Allaah! Na hakika nilikuwa miongoni mwa wenye kufanya mzaha.”}}
 [Az-Zumar: 56].

Nafsi hulalamika hapo kwa mengi iliyoacha kutenda duniani katika yaliyo mema, na pia kulalamika kwa kujuta kwa mengi iliyoyafanya kwa kutenda yaliyo maovu!
·        Ya hasrataa!  (Ee majuto yangu!) kwa kutokumtii Allaah سبحانه وتعالى  na Mtume wake صلى الله عليه وآله وسلم
·        Ya hasrataa! Kwa kutotimiza Fardhi
·        Ya hasrataa! Kwa kutowatii wazazi wangu.
·        Ya hasrataa! Kwa kutoungana na jamaa zangu.
·        Ya hasrataa! Kwa kufanya maovu.
·        Ya hasrataa! Kwa kupoteza wakati wangu kwa yasiyomridhisha Allaah سبحانه وتعالى  
·        Ya hasraata! Ulimi wangu umeniponza kusema wenzangu na kuwafitinisha.
·        Ya hasraata! Kwa kutojielimisha dini yangu!
·       Ya hasrataa! Kwa kutohudhuria darsa na vikao vya elimu!
·        Ya hasraata! Ya hasrataa! Yahasrataa …!

Al muhim, hapo nafsi itajuta kwa mengi ya kila aina!!  Na kama ayah inavyosema pia kuwa ilikuwa nafsi hiyo ikifanya maskhara kwa kutokuamini mambo ya haki aliyoambiwa mtu na aidha wazazi wake, au walimu wake, au wenzake walioongoka!

Au pia maskhara hayo yalikuwa ya kufanyia istihzai ayah za Allaah سبحانه وتعالى kwa kutaka kufurahisha watu tu aonekane kuwa yeye ni mchekeshaji watu.  Au istihzai katika  amri za Allaah سبحانه وتعالى  na Mtume صلى الله عليه وآله وسلمwake kama mfano wale wanaofanya istihzai katika mavazi ya Waumini wanawake na wanaume wenye kutekeleza Sunnah za Mtumeصلى الله عليه وآله وسلم  au kumfanyia istihzai mwenye kufuga ndevu, mwenye kuvaa kanzu fupi, au aina yoyote ya istihzai.


(Majuto ya Nafsi inaendelea…)

0 Comments