Utulivu Wa Nafsi (Sakiynatun-Nafs) - 2

Imekusanywa na Ukht Haliymah ‘AbdullaahIkiachwa maumbile (fitwrah) ya mwanaadamu na nafsi yake bila ya chenye kumuathiri cha nje anaishia kwenye Uislam. Imekuja katika Hadiyth Sahihi:

“Kila kiumbe anazaliwa katika umbile (fitwrah/ Uislam), wazazi wake ndio wanaomfanya (kumbadilisha kuwa) Yahudi au Naswara au Majusi” Al-Bukhaariy.

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

“Je! Wameumbwa pasipo kitu, au wao ndio waliojiumba. Au wameumba mbingu na ardhi? Bali hawana yakini (ya jambo lolote).” At-Twuur: 35-36.

Hapana budi hivyo kuwa kuna Aliyemuumba mwanadamu na ulimwengu huu mpana na hapana budi Awe Muumbaji Huyu ni Mwenye elimu pana, hikma iliyotimia, Anatekeleza Anayotaka, Mwenye uwezo mkubwa. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

“Huyo ndiye Allaah Mola wenu, Muumba wa kila kitu hakuna aabudiwaye kwa haki ila Yeye, basi mnageuzwa wapi? Namna hivi ndivyo walivyogeuzwa wale waliokuwa wakizikanusha Aayah za Allaah (mbele huko). Allaah ni Yule Aliyekufanyieni ardhi kuwa mahali pa kukaa, na mbingu kuwa dari (isiyoanguka), na Akakutieni sura, na Akazifanya nzuri sura zenu na Akakuruzukuni vitu vizuri. Huyo ndiye Mungu, Mola wenu. Basi Mwenye baraka zote hizi ni Allaah, Mola wa walimwengu wote.” Ghaafir: 62-64


3. Kuokoka Muumini Na Adhabu Ya Shaka Na Hayra

Kutokana na imani iliyokuja nayo wahyi na kuungwa mkono na akili na maumbile akasalimika Muumin na shaka na ikamtatulia kitendawili cha kuwepo, kujua chanzo chake mwisho wake na lengo. Akaelewa kwamba ana Mola naye ni Mola wa kila kitu Aliyemuumba na kumuwepesishia yaliyomo mbinguni na ardhini, akapata matumaini kwa Mola wake na kuhisi raha kuwa jirani naye. Akaelewa kwamba maisha haya mafupi wanayoishi watu yamechanganyika kheri na shari. Uadilifu kwa batili, haki kwa batili, ladha kwa uchungu, hii si lengo. Ni shamba la maisha mengine. Kila nafsi italipwa iliyochuma, atadumu kwa aliyoyatenda. Akastarehe Muumin kwa maswali mapana ya maisha na mauti kupata jibu kwamba ameumbwa kwa ajili ya maisha ya milele, mauti yatamuhamisha kutoka sehemu kwenda sehemu nyengine. Akaelewa hakuumbwa bure katika maisha haya wala hakuachwa bure bali Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) alituma Mitume wenye kuelimisha ili waongoke watu katika kheri wajue yanayomridhisha wafuate, na yanayomuudhi wayaepuke.

Muumin kwa imani yake anaelewa hayuko peke yake katika huu ulimwengu vyote vilivyomo vinamtukuza Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).

Zinamtukuza zote mbingu saba na ardhi na vilivyomo ndani yake. Na hakuna chochote ila kinamsabihi (Allaah) kwa sifa Zake njema. Lakini nyinyi hamfahamu kusabihi (kutukuza) kwake. Hakika Yeye Allaah ni mpole (na) mwingi wa kusamehe.” Al-Israa: 44

Wanaomkanusha Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) wanaishi maisha yasiyokuwa na ladha wamejawa na wasiwasi hawana matumaini hata kuwepo kwao duniani hawana jibu nani kawaleta.


4. Uwazi Wa Lengo, Njia Kwa Muumin

Asiye Muumin anaishi duniani katika matatizo ya aina mbalimbali yanamsumbua malengo mengi, daima ana ugomvi ndani ya moyo wake, ajiridhishe nafsi yake au airidhishe jamii kama kilivyo kisa mashuhuri cha baba na mwanae na punda wao.

Muumini amesalimika na yote haya ana lengo moja tu la kumridhisha Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) hajali watu waridhike au wakasirike. Kama alivyojaalia Muumin matatizo yake (humuum) ni tatizo moja, nayo ni kufuata njia inayomfikisha katika kumridhisha Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) njia ambayo anamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) katika kila Swalah:

“Tuongoze njia iliyonyooka” Al-Faatihah: 6.

Ni njia moja isiyopinda. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

“(Na sema uwaambie) Na kwa hakika hii ndiyo njia yangu iliyonyoka. Basi ifuateni wala msifuate njia nyingine, zikakutengeni mbali na njia Yake (Allaah). Al-An’aam: 153.

Ni tofauti kubwa baina ya watu hawa wawili mmoja wao amejua lengo na njia akapata matumaini akastarehe, mwenzie kupotea anatenda bila lengo.

“Je! Anayekwenda akisinukia kwa uso wake ni muongofu au anayekwenda sawasawa katika njia iliyonyoka?” Al-Mulk: 22

Muumini kwa ajili ya kufikia lengo ameona ni madogo mazito, amepata kila aina ya tabu, amejitolea kwa kila kitu, anaendelea hali yuko radhi na kuwa na bishara njema, mfano Khabiyb bin Zayd aliposulubiwa hali wamemzunguka wanaomuadhibu wakadhani atatetereka, bali aliwatizama akiwa na yakini na kusema mashairi:

Wala sijali wakati nitakapouliwa Muislam,
kwa upande wowote marejeo yangu ni kwa Allaah
Na hilo ni kwa dhati ya Allaah,
na Akitaka Hubariki kwa kuunganisha vilivyotenganishwa.

Swahaba mwengine yupo vitani anaingia na mauti yapo machoni naye anasema:

“Nimefanya haraka kukujia, Mola wangu, ili uzidi kunipa radhi (zako).” Twahaa: 84.

Mwengine mkuki umemchoma kifuani umejitokeza mgongoni haikuwa kwake ila kusema:
‘Nimefaulu kwa Mola wa Ka’abah.’

Katika vita vya Al-Ahzaab walipata mitihani Waumini walitetemeshwa pindi walipowaijia maadui juu yao na chini ardhi ikawa dhiki pamoja na upana wake.

Katika hali hii ya kutisha ulikuwa msimamo wao Waumini utulivu na matumaini kwa waliyoahidiwa.

“Na Waislamu (wa kweli) walipoyaona majeshi (ya makafiri yamewashambulia hivyo), walisema, “haya ndiyo Aliyotuahidi Allaah na Mtume Wake (kuwa tutapata misukosuko,kisha tutashinda). Allaah na Mtume Wake wamesema kweli, na (jambo hili) halikuwazidishia ila imani na utii.” Al-Ahzaab: 22.

Nani aliwapa hawa wapiganaji utulivu na matumaini huku vita vikiendelea na mauti yapo machoni mwao. Ni imani peke yake. Anasema Allaah katika Qur-aan:

“Yeye Ndiye Aliyeteremsha utulivu katika nyoyo za Waislamu ili waongezeke imani juu ya imani yao. Na majeshi ya mbingu na ardhi ni ya Allaah, na Allaah ni Mwenye ujuzi (wa kila jambo) na Mwenye hikima.” Al-Fat-h: 4.


Ameelewa Muumin lengo na njia iliyonyooka ni njia aliyowaneemesha Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Manabii, Wakweli (Swidiyqiyn), Mashahidi na Watu wema (Swaalihiyn). Ni njia iliyonyooka (Swiraatw al-Mustaqiym) ambayo anaongoza nayo Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

“Na kwa yakini wewe unaongoza katika njia iliyonyooka. Njia ya Allaah Ambaye ni Vyake (peke Yake vyote) vilivyomo mbinguni na vilivyomo katika ardhi.” Ash-Shuuraa: 52-53.

Kutokana na njia hii iliyonyooka (Swiraatw al-Mustaqiym) alikuwa Muumin katika tabia na mwenendo wake mwenye matumaini bila ya kuwa na shaka, thabiti bila ya kukengeuka, muwazi bila ya kusitasita, mwenye msimamo bila ya kupinda, haimtii shaka mielekeo inayogongana, haimuadhibu migongano ya matakwa, haivunjiki shakhsiyah yake kwa migongano ya ndani ya nafsi, afanye (jambo) au aache? afanye hili au lile?

Muumin ana misingi iliyo wazi… Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

“Bila shaka imekwishakufikieni nuru kutoka kwa Allaah na kitabu kinachobainisha (kila jambo). Kwa kitabu hicho Allaah Huwaongoza wenye kufuata radhi Yake katika njia za salama, na Huwatoa katika kiza kuwapeleka katika nuru kwa amri Yake, na Huwaongoza katika njia iliyonyooka.” Al-Maaidah: 15-16.

Kisa cha Nabii Ibraahiym aliporuzukiwa mtoto ukubwani akamlea kwa mapenzi makubwa kisha akatakiwa amchinje mwanae na hawakutetereka bali walijawa na utulivu na matumaini wakati wa shida. Hapa inatuonesha ujasiri na uthibiti wa baba kumtoa mhanga mwanae na subira ya mtoto mwema.

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

“Ndipo tukampa habari njema ya (kuwa atapata) mtoto mpole. (Basi akapata. Naye ndiye  Nabii  Isma’iyl.” As-Swaaffaat: 101 Mpaka aya ya 111 kisa chote.

Anayeabudiwa ni Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Pekee, Anasema katika Qur-aan:

“Sema, “kwa hakika mimi Mola wangu ameniongoza katika njia iliyonyoka, (katika) dini iliyo sawa kabisa ambayo ndiyo dini ya Ibraahiym aliyekuwa mwongofu, wala (kabisa) hakuwa miongoni mwa washirikina. Sema “hakika Swalah yangu, na ibaada zangu (zote zingine) na uzima wangu, na kufa kwangu (zote) ni za Allaah. Muumba wa walimwengu wote. Likinisibu jambolimenisibu kwa kutaka Allaah si kwa kutaka viumbe Vyake. Na yote ninayofanya nayafanya kwa ajili yake.’’
Hana mshirika Wake. Na haya ndio niliyoamrishwa, na mimi ni wa kwanza wa waliojisalimisha (kwa Allaah).” Sema je, nishike Mola mwengine asiyekuwa Allaah, na hali Yeye (Allaah) Ndiye Mola wa kila kitu?” Al-An’aam:161-164.

Kheri ya dunia na Akhera inapatikana katika kumfuata na kumridhia Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).

“Haiwi kwa mwanamume aliyeamini wala kwa mwanamke aliyeamini, Allaah na Mtume Wake wanapokata shauri wawe na hiari katika shauri lao.” Al-Ahzaab: 36.

“Haiwi kauli ya Waislamu wanapoitwa kwa Allaah na Mtume Wake ili ahukumu baina yao, ila kusema: “Tunasikia na tunakubali, “na hao ndio watakaofuzu.” An-Nuur: 51.


5. Kufarijika Muumin Kwa Vilivyomo Ulimwenguni

Muumin anaishi akiunganika na vilivyopo vyote na vinamliwaza Kwani huu ulimwengu si adui kwake wala kitu kigeni bali ni sehemu ya fikra zake na mazingatio katika kutazama kwake anazingatia madh-har ya neema za Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na athari ya Rehma zake.
Huu ulimwengu mpana unanyenyekea kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kama anavyonyenyekea Muumin na unamtukuza Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kama Muumin anavyomtukuza.

Muumin anatazama dalili itakayompeleka kwa Mola wake na rafiki atakayemliwaza katika matatizo na kwa hilo (mtizamo wa upendo unaokubali kuwepo kwake) kinapanuka kifua cha Muumin na maisha yake yanatanuka.
Hakuna kitu chenye dhiki kama moyo wa asiyemuamini Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) mwenye shaka na Akhera hakika maisha yake ni ya dhiki kuliko jela yupo mbali na chenye kuondoka (dunia) na kinachobaki (Akhera) hajui isipokuwa leo wala hajui katika siku hiyo ila matamanio ya kinyama na kuwepo kwake kimwili tu, huu ndio ukweli tangu aliposhuka Nabii Aadam na mkewe katika ardhi.

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

“Na ukikufikieni kutoka Kwangu uongofu, basi atakayeufuata uongofu Wangu hatopotea wala hatotaabika. Na atakayejiepusha na mawaidha Yangu (hayo), basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki …” Twahaa: 123-124.


6. Muumini Anaishi Katika Upamoja Na Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala)

Hakuna katika maisha haya kikubwa kama nafsi. Kibaya wanachofanyiwa wafungwa ni kuwekwa peke yao na kukosa hisia za kuchanganyika na wenzao, je, ni vipi anayejitia nafsi yake mwenyewe jela akaishi kwa hisia zake na muono wake pekee japo dunia imejaa binaadamu pembezoni mwake na haya ni maradhi (ya nafsi) mabaya kabisa anapuuzia vinavyomzunguka haoni ila anayotaka kila ageukapo haoni ila nafsi yake, jela aliyojitia haina milango wala madirisha kimbilio lake liko wapi?

Maradhi haya ya nafsi inadhihiri athari yake katika mwili kama inavyodhihiri katika harakati zake na ayatendayo inaweza kumpata kizunguzungu kutokwa na jasho moyo kwenda mbio kana kwamba anaogopa adui mwenye nguvu au anapelekwa sehemu nzito au kunyata kama anayetaka kutoroka.
Anasema Dr. Moses Gilbert mkuu wa idara ya afya ya wagonjwa wa akili iliyopo New York, “Hakika maradhi ya kuhisi mwanadaamu yupo peke yake ni sababu ya msingi ya kuchanganyikiwa kiakili.”

Madaktari na wajuzi wa nafsi wamefanya juhudi kubwa na majaribio katika kutafuta tiba hawakufanikiwa mpaka baadhi yao mwishoni wakaelekeza tiba kuelekea dini na kushikamana na imani na kufarijika mgonjwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).

Imani yenye nguvu ndio dawa ya maradhi haya ya hatari na ni kinga bora ya shari yake.

Dr. Frank Lupark mjuzi wa elimu ya nafsi wa Kijerumani anasema, “Vyovyote itakapofikia hisia yako ya upweke jua hupo peke yako kamwe ukiwa upande wa njia tembea hali ukiwa na yakini kwamba Mungu Yupo upande wa pili.”

Itikadi ya Muumin ni zaidi ya hivyo Kwani yeye anaamini yupo naye popote (kwa elimu Yake), popote atakapokuwa basi Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anamuona na siyo upande wa pili wa njia.

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) katika Hadiyth Al-Qudsiy,

“Mimi Nipo katika dhana ya mja Wangu, Niko naye anaponitaja.”

Anasema katika Qur-aan:

“Basi msiregee na kutaka suluhu, (piganeni nao maadui zenu), maana nyinyi ndio mtakaoshinda, na Allaah Yu pamoja nanyi, wala Hatokunyimeni (thawabu za) vitendo vyenu.” Muhammad: 35

Anasema mshairi wa Kimagharibi katika kuupokea mwaka, “nilimwambia mtu aliyesimama mlango wa kuingilia nipe mwanga niangaze katika kiza cha njia, akasema weka mkono wako katika mkono wa Mungu atakuongoza katika njia.”

Hao sio waumini wa kweli ama Muumin wa kweli anaamini mkono wake upo na mkono wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na usaidizi Wake u pamoja naye, na macho Yake hayafumbi anaondokana na hisia ya upweke na ndoto mbaya.

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

“Na mashariki na magharibi ni ya Allaah. Basi mahala popote mgeukiapo (alikokuamrisheni Allaah mtakuta) huko wajihi wa Allaah. Bila shaka Allaah ni mwenye wasaa (mkubwa kabisa) na Mwenye kujua kukubwa kabisa vilevile.”  Al-Baqarah: 115.

“Naye yu pamoja nanyi popote mulipo (kwa elimu yake). Na Allaah Anaona mnayotenda (yote).” Al- Hadyd: 4

Anapata hisia (shu’ur) aliyopata Nabii Muusa pindi alipowaambia Bani Israail:

“Mola wangu Yu pamoja nami, bila shaka ataniongoza (tuokoke sote).” Ash-Shu’araa: 62.

Na hisia alizokuwa nazo Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pangoni pindi alipomwambia Swahibu wake (Abu Bakr):

“Usihuzunike kwa yakini Allaah Yu pamoja nasi.”At-Tawbah: 40.

Hisia ya Muumin kuwa karibu na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) daima inamjaalia kuliwazika na neema ya kumkaribisha kwake anahisi daima nuru imeufunika moyo wake hata kama atakuwa katika giza la usiku anahisi utulivu umejaa katika maisha yake hata kama atakuwa katika ubaya wa anaoishi nao na kuchanganyika.

Itaendelea in shaa Allaah…

0 Comments