Utulivu Wa Nafsi (Sakiynatun-Nafs) - 3

Imekusanywa na Ukht Haliymah ‘Abdullaah
7. Muumin Anaishi Pamoja Na Urafiki (Suhba) Ya Manabii Na Wakweli 

Muumin hahisi kwamba ametengeka na nduguze Waumini, hakika wao ikiwa hawapo naye msikitini au nyumbani kwake daima wanaishi katika dhamira yake. Akiswali hata akiwa peke yake anaongea kwa jina lao:

“hakika Wewe Ndiye tunayekuabudu na Wewe tu Ndiye tunayekutaka msaada” Al-Faatihah: 5.

Akiomba du’aa anaomba kwa jina lao (tuongoze njia iliyonyooka), akijikumbuka nafsi yake anawakumbuka (amani iwe juu yetu na juu ya waja wema wa Allaah).

Muumin haishi na nduguze Waumini wa wakati wake tu bali anaishi na Waumini wa karne zote hata ikiwa imepita baina yao miaka anasema waliyosema watu wema:

Mola wetu! Tusamehe sisi na ndugu zetu waliotutangulia (kufa) katika Uislam.” Al-Hashr: 10.

Muumin anahisi anaishi kwa imani yake na matendo yake mema pamoja na Manabii wa Allaah na Mitume Wake. Na pamoja na kila mkweli, shahiyd, mtu mwema katika kila umma na kila zama:

“Na wenye kumtii Allaah na Mtume, basi hao watakuwa pamoja na wale Aliowaneemesha Allaah, Manabii na Mashahidi na Swaalihiyn (watu wema). Na uzuri ulioje (kwa mtu) watu hao kuwa rafiki (zake). An-Nisaa: 69.

Ni nani ana furaha zaidi ya yule anayefungamana na hawa? Mafungamano haya si ya kimwili na sura tu bali ni mafungamano ya kiroho, kifikra na kimoyo.


8. Swalah Na Du’aa Ni Vinavyopelekea Utulivu  

Katika sababu ya utulivu wa nafsi ambayo wamenyimwa wenye kuabudia mali wakaneemeshwa nayo Waumini wakawa wanaongea na Mola wao kila siku katika Swalah na dua …

Swalah ni fursa ya mtu kuisafisha nafsi yake na shughuli za kidunia asimame mbele ya Mola wake kwa kumtukuza hali akimuomba. Katika kuwasiliana na Allaah (katika Swalah) kunaipa nafsi nguvu na matumaini kwa roho nayo ni silaha ya Muumin anayoitumia katika vita vya kimaisha na kupambana na balaa zake na vyenye kutia uchungu. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

“Enyi mlioamini jisaidieni (katika mambo yenu) kwa subira na Swalah, bila shaka Allaah yu pamoja na wanaosubiri.” Al-Baqarah: 153.

Alikuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) likimtingisha jambo lolote anakimbilia Swalah na haikuwa Swalah yake ni picha tu bali ilikuwa ni katika kuwa faragha na kunong’ona na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), mpaka ikawa ikifika wakati wa Swalah anamwambia muadhini wake Bilaal (Radhiya Allaah ‘anhu):

“Tufurahishe kwayo ewe Bilaal”
na alikuwa akisema,

“Nimejaaliwa kitulizo cha macho yangu katika Swalah”.

Anasema Deen Carnegie katika kitabu chake ‘Acha yanayokutatiza na uanze maisha’:

“…Swalah inakuhakikishia mambo matatu haijalishi uwe ni Muumin au Mulhid (anayeitoa kasoro dini na kutoiamini).

1.     Swalah ni usaidizi katika kuelezea yanayoshughulisha nafsi yako na yaliyo mazito, wamebainisha wema waliopita kwamba haiwezekani kukabiliana na tatizo ambalo halijulikani, Swalah ni sawa na kitabu ambayo anaelezea mwenye fani ya Adab (Adiyb)  matatizo yake (humuum), tukitaka suluhisho la matatizo yetu ni wajibu kwetu iwe wazi katika ndimi zetu na hivi ndivyo tunavyofanya tukimuelezea matatizo yetu Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).

2.     Swalah inakufanya uhisi huko peke yako katika kutatua matatizo yako na yanayokuhuzunisha (humuum), mara nyingi matatizo yatukutayo ya kibinafsi tunashindwa kuwaelezea hata watu walio karibu yetu lakini kwa mapana tunamuelezea Allaah ‘Azza wa Jalla katika Swalah.


Madaktari wa nafsi wanakubaliana kwamba tiba ya maradhi ya kinafsi (Tawaatur Al-‘Aaswab) kwa kuwaelezea marafiki wa karibu sana na ndugu mpenzi sababu ya matatizo uliyonayo, tusipopata wa kumueleza anatutosha Allaah kuwa msaidizi wetu.

3.     Swalah ni hatua ya mwanzo kuiendea kazi. Inawezekana mtu akawa anaswali siku baada ya siku bila ya kupata faida yaani haiboreshi hali yake na kutatua yamkumbayo.

Ikiwa hii ni hali ya Swalah kwa ujumla (kwa wasio Waislamu) basi Swalah katika Uislamu ina athari zaidi ya hivi ndani yake kuna twahara inayochangamsha mwili, Qur-aan isomwayo nacho ni Kitabu cha kudumu, kuhuisha jama’ah ambayo imesisitiza na kuhimiza Uislam.

Utulivu ulioje anaohisi Muumin pindi anapomwelekea Mola wake wakati wa matatizo na siku ya shida anamuomba kama alivyoomba Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):

“Ewe Allaah, Mola wa mbingu saba, na Mola wa ‘arshi tukufu, Mola wetu na Mola wa kila kitu, Mwenye kuichanua tembe ya mbegu na kokwa, na Aliyeteremsha Tawraat na Injiyl na Qur-aan, najikinga Kwako kutokana na shari ya kila kitu, Wewe Ndiye mwenye kukamata utosi wake, Ewe Allaah Wewe Ndiye wa mwanzo, hakuna kabla Yako kitu, na Wewe Ndiye uliye wazi, hakuna juu yako kitu chochote, na Wewe Ndiye uliyefichika, hakuna kilichojificha chini Yako, tulipie madeni yetu, na utuepushe na ufakiri.” Muslim

Dokezo: Du’aa hii pia ni katika du’aa za kusoma wakati wa kulala usiku ipo katika kitabu kidogo cha du’aa ‘Hiswnul Muslim.’

Na ni ipi matumaini kama aliyoshushiwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) moyoni mwake alipokuwa anarudi kutoka Twaaif miguu miwili ikiwa inavuja damu, amejeruhiwa moyo kutokana na mabaya aliyokumbana nayo kwa watu hao, haikuwa kwake ila kunyanyua mikono yake mbinguni huku moyo wake ukiwa baridi na salama na kusema:

“Ewe Allaah mimi nashtakia udhaifu wa moyo wangu na uchache wa hila yangu na kudharauliwa na watu. Ewe mwenye kurehemu mwingi wa rehma, Wewe Ndiye Mola wa wenye kutiwa udhaifu (Mustadhw’afiyn), nawe Ndiye Mola wangu…”


9. Muumin Haishi Baina Ya ‘Lau’ Na ‘Layta’

Sababu kubwa ya matatizo (Qalaq) ambayo anakosa mwanaadamu utulivu wa nafsi, amani, radhi ni kujutia wakati uliopita na kukasirikia wakati uliopo na khofu ya wakati ujao.

Baadhi ya watu inawashukia misiba anabaki nayo miezi na miaka anajikumbushia maumivu yake wakati mwengine akijuta na wakati mwengine akiwa na matumaini laiti ningefanya, laiti ningeacha, lau ningefanya vile ingekuwa hivi.

Madaktari wa nafsi wao pamoja na waelekezaji wa kijamii na watu wa malezi na kazi, wanatoa nasaha kwamba mwanaadamu asahau maumivu yaliyopita na aishi sanjari na wakati uliopo Kwani wakati uliopita haurudi.

Udhaifu wa mwanaadamu unawakumba wengi unawajaalia watwange unga uliokwishatwangwa wanalilia wakati uliopita wanang’ata vidole vyao kujutia yaliyopita. Muumin wa kweli amesalimika na hisia hizi Kwani anaamini Uwezo na makadirio ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) hajisalimishi nafsi yake kutokana na matukio yaliopita anaitakidi kwamba jambo Analotaka Allaah  huwa.

Muumin anaelewa Alilokadiria Allaah huwa hivyo, kwanini akasirike?
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

“Hautokei msiba katika ardhi wala katika nafsi zenu ila umekwishaandikwa katika Kitabu (cha Allaah) kabla Hatujaumba. Kwa yakini hilo ni sahali kwa Allaah.
“Ili msihuzunike sana juu ya kitu kilichokupoteeni (na kinachokupoteeni), wala msifurahi sana kwa Alichokupeni (na kwa Anachokupeni). Na Allaah Hampendi kila ajivunaye,ajifakharishaye.” Al-Hadiyd: 22-23.

Katika vita vya Uhud ambapo waliuawa Waislamu sabini, Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Alielezea hali za wanafiki wenye maradhi ya moyo na madhaifu wa imani walioishi baina ya ‘lau’ na kujutia kwa kusema ‘layta’ laiti..

“Na kulikuwa kundi jingine nafsi zao zimewashughulisha (hawajijui hawajitambui); wakimdhania Allaah dhana zisizokuwa ndizo, dhana za ujinga; wakisema “Ah! Tuna amri sisi katika jambo hili?” Sema: “Mambo yote ni ya Allaah. Wanaficha katika roho zao (hao wanafiki) wasiyokubainishia. Wanasema: “Tungekuwa na chochote katika jambo hili tusingeuawa hapa”. Sema: “Hata mngalikuwa majumbani mwenu, basi wangelitoka wale walioandikiwa kufa, wakenda mahali pao pa kuangukia wafe.” Al-‘Imraan: 154.

Akawarudi (Allaah) hao waliowaambia Ndugu zao hali wao hawakwenda:

“Wale waliosema juu ya Ndugu zao na (wao wenyewe) wamekataa kwenda (hawakwenda) vitani: “Wangalitutii wasingeuawa.” Sema: “Jiondoleeni mauti (nyinyi wenyewe msife maisha) ikiwa mnasema kweli.”  Al-‘Imraan: 168.


Muumin hawi kama hawa wanafiki wala Ndugu zake makafiri ambao Qur-aan imekataza kujifananisha nao katika kujuta kwao na matamanio yao ya kihuzuni.

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

“Enyi mlioamini! Msiwe kama wale waliokufuru na wakasema juu ya Ndugu zao waliposafiri katika nchi au walipopigana (wakafa): “Wangalikuwa kwetu wasingalikufa wala wasingaliuawa.” (Amewatia Allaah dhana hii) ili Afanye hayo kuwa majuto katika nyoyo zao. Na Allaah Anahuisha na kufisha na Allaah Anaona yote mnayotenda.
“Na kama mkiuawa katika njia ya Allaah au mkifa (si khasara kwenu) Kwani msamaha na rehema zinatoka kwa Allaah (kukujieni) ni bora kuliko vile wanavyokusanya (hapa ulimwenguni.” Al-‘Imraan: 156-157.

Alama (shi’aar) ya Muumin daima ni kusema “Amekadiria Allaah na Analotaka huwa, Namshukuru Allaah kwa kila hali”. Na kwa hilo hatajutia yaliyopita wala haishi kwa kukumbukia machungu inamtosha kusoma neno lake Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

“Haufiki msiba wowote ila kwa idhini ya Allaah, na anayemuamini Allaah Huuongoza moyo wake (kwendea maliwaza mazuri). Na Allaah ni Mjuzi wa kila kitu.” At-Taghaabun: 11. 


WabiLlaahi At-Tawfiyq               

0 Comments