Masuala Kumi Yanayoeleweka Vibaya Katika Uislam - 2


Suala Nambari 2 Linaloeleweka Vibaya


Ndani ya Uislamu, hakuna tatizo kukataa haki za binaadamu kwa sababu:

  • Uislamu unapingana na demokrasia iliyo safi.


  • Uislamu unakubaliana na utumwa.JIBU

Suala hilo haliendani na hoja zilizotolewa, na hoja hizo zinaacha habari zilizo nyingi kabisa.

Kama ilivyoelezwa awali, Uislamu ni njia iliyokamilika ya maisha. Kwa hili, sio jambo la kushangaa kwamba Muumba Ametuchagulia mwenendo ambao tutahitaji kujitawala. Kanuni kuu ambayo Taifa la Kiislamu ni lazima kuichunguza inaelezwa ndani ya Qur-aana (tafsiri inafuatia):

{{Enyi mlioamini! Mtiini Allaah na mtiini Mtume na wenye mamlaka juu yenu, walio katika nyie (Waislamu wenzenu). Na kama mkikhitalifiana juu ya jambo lolote basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume, ikiwa mnamwamini Allaah na Siku ya Mwisho. Hiyo ndiyo kheri, nayo ina matokeo bora kabisa.}} [4:59]

Kutokana na Aayah hii, ni wazi kwamba lengo la taifa katika utiifu kwa Muumba ni muhimu kama ambavyo ulivyo unyenyekevu kwa kila mtu. Hivyo, ni lazima kwa Taifa la Kiislamu kutunga sheria zake kutokana na Qur-aan na Sunnah. Kanuni hii inazuia Taifa la Kiislamu kuwa na hiari ya kuchagua mfumo wa siasa na uchumi, kama vile demokrasia safi, ubepari usio kuwa na kizuizi, ukomunisti, ujamaa, n.k. Kwa mfano, demokrasia safi inawaweka watu juu ya Qur-aan na Sunnah, na hili ni utomvu wa utiifu kwa Muumba. Hata hivyo, mbadala bora kwa demokrasia safi ni demokrasia ambayo inasimamisha na kutilia nguvu Shari’ah (Sheria ya Kiislamu).

Muumba pia Anaeleza ndani ya Qur-aan: (tafsiri):

{{Basi vyote hivi mlivyopewa ni starehe ya maisha ya dunia tu, lakini kilichoko kwa Allaah ni bora na cha kudumu (milele). Watakistahiki wale walioamini na wakawa wanamtegemea Mola wao. Na wale wanaojiepusha na madhambi makubwa na mambo mabaya, na ambao wanapokasirika husamehe. Na wale waliomuitikia Mola wao (kwa kila amri Zake) na wakasimamisha Swalah, na wanashauriana katika mambo yao na wanatoa katika yale Tuliyowaruzuku.}} [42:36-38]

Allaah Anatuamirisha ndani ya Aayah hii kufanya mambo yetu kwa kuchukua ushauri kutoka miongoni mwetu, au kwa mmoja kushauriana na mwengine. Huu ni utaratibu wa Taifa la Kiislamu; kushauriana, lakini ni lazima kuiweka Qur-aan na Sunnah kileleni. Sheria yoyote ambayo inapingana na Qur-aan au Sunnah ni batili. Kanuni hii iliyo pana ya kushauriana, hakika ni pana kabisa kuingiza mfumo wa serikali ambapo watu wote wana pata haki ya kusikilizwa, ingawa ukweli ni kwamba wanahamasishwa kusikilizwa. Mataifa ya kale ya Kiislamu yalikuwa katika mfumo huu. Leo, serikali nyingi zilizo dhaifu za “nchi za Waislamu” hazitumii kanuni hii na ukweli wanatenda makosa mengi ya jinai dhidi ya watu.

Ama kwa utumwa, Uislamu upo tofauti kabisa miongoni mwa dini nyengine; Uislamu una azma iliyojikita ndani kabisa, ya kuondosha utumwa kwa njia za salama. Kabla ya kuingia Uislamu, utumwa ulienea duniani kote. Mtume wa Uislamu ametufundisha kwamba kuwaachia huru watumwa lilikuwa ni tendo bora kwa uoni wa Allaah. Kutokana na Sunnah, hususan ndani ya somo la Sunnah linaloitwa Sahih al-Bukhaariy, tunaona:

Amesimulia Abuu Hurayrah: Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema, “Yeyote anayeacha huru mtumwa aliye Muislamu, Allaah Ataviokoa viungo vyote vya mwili wake kutokana na Moto kama alivyoviachia huru viungo vya mtumwa.” Sa'iyd bin Marjana amesema kwamba ameisimulia Hadiyth hiyo kwa ‘Aliy bin Al-Hussain na kuachia huru mtumwa ambaye ‘Abdullaah bin Ja’far alikwishataka kumpatia Dirhaam alfu kumi au Dinaar alfu moja. [3:46:693]

Halikadhalika kutokana na Sunnah, hususan somo la Sunnah linaloitwa Muwattwa ya Maalik, tunaona:

Amesimulia Ummul Mu’miniyn 'Aaishah: Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa ni mtumwa gani aliye bora kumuachia huru. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), alijibu: “Mtumwa aliye ghali na mwenye thamani zaidi kwa bwana wake.” [38:9:15]

Muumba pia Amelifanya zoezi la kuwapatia uhuru wao watumwa, kuwa ni jepesi. Kutoka kwenye Sunnah, hususan somo la Sunnah linaloitwa Sahih al-Bukhaariy, tunaona:

Amesimulia Abuu Hurayrah: Mtume amesema, “Yeyote anayesamehe sehemu ya mtumwa wake aliye muhimu basi amsamehe mtumwa huyo moja kwa moja kwa kulipa thamani yake iliyobaki kutoka kwenye pesa zake kama anazo pesa zinazotosha; ikiwa si hivyo, thamani ya mtumwa itakisiwa na mtumwa asaidiwe kufanya kazi bila ya uzito hadi atakapolipa thamani iliyobaki” [3:46:704]

Masharti ya utumwa ni tofauti kabisa ndani ya Uislamu kuliko yale masharti mazito yaliyolazimishwa na wasio kuwa Waislamu au Waislamu wasio watiifu. Kutoka kwenye Sunnah, hususan ndani ya somo la Sunnah linaloitwa Sunan Abuu-Daawuud, tunaona:

Amesimulia Abuu Hurayrah: Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Asiseme miongoni mwenu: “Mtumwa wangu” (abdi) na “Mtumwa wangu wa kike” (amaati), na mtumwa asiseme: “Mtawala wangu” (rabbi au rabbati). Bwana (wa mtumwa) aseme: “Kijana wangu wa kiume” (fataya) na “Kijana wangu wa kike” (fataati), na mtumwa aseme: “Bwana wangu” (sayyidi) na “Bibi yangu” (sayyidati), kwani nyote ni watumwa (wa Allaah) na Mtawala ndie Allaah, Aliye Mkuu.” [41:4957]

Ama kutoka kwenye Sunnah, hususan ndani ya somo la Sunnah linaloitwa Sahih al-Bukhaariy, tunaona:

Amesimuliwa Al-Ma’ruur bin Suwaid: Nimemuona Abuu Dhar Al-Ghifari amevaa joho, na mtumwa wake pia, alikuwa amevaa joho. Tulimuuliza kuhusu hilo (yaani kwanini wote walikuwa wamevaa majoho yaliyofanana). Alijibu, “Mara moja nilimvunjia heshima mtumwa mmoja na alinishtakia kwa Mtume. Mtume akaniuliza, “Umemvunjia heshima kwa kumtukana mama yake?” Akaongeza,“Watumwa wenu ni ndugu zenu ambamo Allaah Amekupeni uongozi. Hivyo, kama mmoja ana ndugu mmoja chini ya uongozi wake, mmoja wenu awalishe kama ambavyo anavyokula, na kuwavisha namna ambavyo anavyovaa. Usiwakalifishe kwa yale ambayo hawawezi kuyahimili, na kama mkifanya hivyo, wasaidieni (kwenye kazi zao ngumu).” [3:46:721]

Matokeo ya mafundisho haya ya Uislamu ni kuwa; utumwa kwa kiwango kikubwa ulikaribia kuondoshwa moja kwa moja kutoka sehemu nyingi za Waislamu ulimwenguni, kwa amani na bila ya kumwaga damu.Itaendelea in shaa Allaah…

0 Comments