Simu Katika Shariy'ah Ya Kiislamu-2

Imekusanywa Na: Sulaymaan ‘Iysaa4-Dakika na muda wa maongezi

Kipimo chake ni maneno ya kiusuli yasemayo:
  • Kila sehemu pana mazungumzo husika.
  • Na kila mazungumzo yana kipimo husika.
  • Katika kipindi cha nyuma kidogo na mpaka sasa baadhi ya mitandao ya simu imekuwa ikitoa ofa ya kuongea muda mrefu kwa gharama ndogo, na mtu bila kujali kuwa huu ni wakati wa kazi au usiku watu wamelala na kadhalika, anarefusha mazungumzo kisa na mkasa ni kwamba leo ana ofa ya kuongea bure masaa 24 au 12 kwa thamani ndogo ya vocha alizoingiza katika simu yake.

5-Maamkizi ya Kiislamu kwa mwenye kufanya mawasiliano mwanzo na mwisho

Mpigaji simu ni kama vile mjaji katika adabu za ziara, hivyo, atakaporuhusu au kupokea simu nduguyo fanya haraka kumtolea salamu ya Kiislamu “Assalaamu ‘Alaykum” kwani maamkizi haya ni nembo kuu za Uislamu na ni ufunguo wa amani na salama si hivyo tu bali ni sharaf ya Ummat Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika mambo yanayowauma sana wasiokuwa Waislamu na haswa Mayahudi ni kuwaona Waislamu na kuwasikia wakitoleana salaam hii “Assalamu ‘Alaykum wa RahmatuLlaahi wa Barakaatuh” na ni lazima kujibu kwa kusema “Wa ‘Alaykumus Salam wa RamatuLlaahi wa Barakaatuh” kwa atakayesikia salaam hii. 

Pamepokelewa katika Sunan Abiy Daawuud kutoka kwa Rabiu (Radhiya Allaahu ‘anhu) anasema, alitueleza mtu mmoja katika kabila la bani Aamir kwamba yeye alitaka idhini kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa ndani kwake – akasema yule mtu wakati anabisha hodi, “niingie?” Akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumwambia mfanyakazi wake: “Toka na umfundishe mtu huyu kubisha hodi – mwambie aseme – Assalaamu ‘Alaykum – Je. niingie? Akasikia yule mtu  akasema, “Assalaamu ‘Alaykum, je, ningie?” Akakaribiswa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaingia. 
Inafahamisha Hadiyth hii juu ya kutanguliza salamu kwa mwenye kufanya ziara – hiyo pia kwa mwenye kufanya mawasiliano na atangulize salaam ya kishari’ah – si kunyamaza au kuanza kwa kusema ‘hallo’ au ‘khabari’, ‘mambo’, n.k.


Hata hivyo baadhi ya salaam ni vizuri
Amepokea Imaam Muslim katika sahihi yake na Abuu Daawuud katika Sunnan yake kuwa Jaabir (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: 
“Nilitaka idhini ya kuingia kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema ni nani huyu anayebisha hodi? Nikasema, “mimi”. Akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), “mimi”, “mimi” – kama kwamba neno hilo lilimkera.”

Ikiwa itatokea mpokea simu hatakufahamu, akataka kujua nani anawasiliana naye, basi taja jina au sifa ya ujumla mfano ‘jina lako’ au ‘kun-yah yako’ na mfano wa hayo. 
 
Kadhalika kujifahamisha kwa jina lako la Kun-yah kama kusema, “mimi Abuu Hannaan” au “mimi Abuu Hasan” au “Abuu Maryam” na kadhalika ikiwa jina kama hilo wewe si maarufu nalo si vyema, bali wema waliotangulia hawakuwa wakijitambulisha hivyo – hili ni kwa wale hayakua majina yao ni maarufu –,  lakini waliojulikana sana kwa Kun-yah zao si vibaya kuyatumia kama ambayo alivyokuwa Abuu Bakr na Abuu Dharr na Ummu Haaniy (Radhwiya Allaahu ‘anhum) ambao walikuwa wakijulikana zaidi kwa majina hayo ya Al-kunaa kuliko majina yao ya asili.

Kisha kama ulivyoanza mazungumzo kwa salaam, kamilisha au funga mazungumzo yako kwa salaam. Ansema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
“Pindi atakapofika mmoja wenu katika kikao chochote basi atoe salaam na atakapo kuamka ili aondoke basi atoe salaam tena, kwani salaam ya mwanzo si kwenye haki (si bora zaidi) kuliko ya mwisho.” Amepokea Abuu Daawuud.


6-Simu na mwanamke

Pindi awapo mmoja kati ya wenye kufanya mawasiliano ni mwanamke, basi na achukue tahadhari yake ya Kiislamu kutolainisha na kuiremba sauti yake, kwani Allaah (Subhanahu wa Ta’ala) Aliwakataza wake wa Nabii Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mama wa Waumini (Radhiya Allaahu ’anhunna) ambao hakuna yeyote awezae kuwatamani! (kwani kuna yeyote awezae kumtamani mama yake? Ila aliye punguwani) na walikatazwa kulainisha na kuremba sauti zao pindi waongeapo na Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) katika zama tukufu na bora, zama za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum). Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):
“Na wala msilainishe sauti zenu kwa neno lolote mlisemalo akatamani yule ambaye katika moyo wake pana maradhi ya kutamani. Na semeni maneno mema.” Al-Ahzaab: 32

Vipi kwa wanawake wa zama zetu? Uongeavyo na mumeo; mumeo mrembee na umpambie sauti na maneno pia. Zama zisizo bora, zama zilizojaa uovu na uchafu wa kila aina? Hakika kulainisha na kuremba sauti zao kunakatazwa zaidi. Hivyo mcheni Mola wenu enyi wanawake wa Kiislamu msilainishe wala kuziremba sauti zenu pindi muongeapo na watu wasi Mahrim zenu (ajnabiy) iwe ndani ya simu au laa; kwa ufupi usiongee na mwanaume yeyote kama

Kadhalika si vizuri kuchukua muda mrefu kuongea na kutoa sauti kubwa isiyokuwa na haja ya kunyanyuliwa isipokuwa kiasi cha kusikilizana wao wawili tu.  Na itakapokuwa hali ni kama hivi tulivyoeleza (yaani mwanamke anaongea kwa sauti laini iliyojaa kila aina za kurembwa, inakuwa ni haramu mwanaume kwa kuhofia fitna kuendelea kumsikiliza na kuongea nae hata kama mwanamke huyo anasoma Qur-aan kwa sauti iliyo jaa mahaba na kadhalika).

Na hapa tunajifunza pia, kwa mwanaume mwenye wivu na mwenye kuijua dini yake vizuri mchunga wa familia yake kimaadili na kitabia, kama anavyojihifadhi kiafya – basi na aijifadhi na yaliyo haramu, asiwe mwanamke ni wa kwanza kupokea simu, kuitikia, na kukaribisha mbisha hodi pindi awapo mwaname nyumbani.

Tumeona  katika sehemu ya (5) Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndiye aliyekuwa akiuliza nani mbisha hodi? Na si wake zake au watoto wake wa kike.

Imetukuka kimaadili nyumba ile ambayo ipo chini ya msimamizi, mchunga, mwenye akili na mwenye elimu, si mkali wala mwenye hasira, ila mwenye kumuudhi Allaah. Na imepata hasara nyumba ile ambayo haina msimamizi, mchunga mwenye akili, wala elimu. Simu ya baba mwenye nyumba kila mtu ni yake; ikiita tu mara mtoto kapokea, au mke wake, au mfanyakazi wake wa ndani, na kila mmoja kati ya wao aigombea si mdogo wala mkubwa!! Maskini aliyepiga hajulikani au ajulikana basi akiipokea mke ataongea kama vile anamjua, au kama ni baba yake mzazi aliyepotezana nae muda mrefu – Ya Allaah Mola wetu – ni mara ngapi matatizo hutokea katika majumba yetu kwa sababu hizi? Ee Mola wetu kwa upole Wako na sitara Yako tusitiri wewe ni Mwingi wa rahma na huruma tuhurumie, Aamiyn, Aamiyn.


7-Simu na miito (kengele) au miziki

Watu (watumia simu) katika hili wamegawanyika pande mbili zenye kupingana:
(1) Kuna watu ambao simu zao zikiita au ukiwapigia patasikika zikiita kwa kutoa sauti za pumbao miongoni mwa nyimbo na muziki na kadhalika, hili ni haramu.

(2) Na kuna watu ambao simu zao zikiita au ukiwasiliana nao patasikika katika simu zao sauti za Qur-aan ikisomwa au dhikri na kadhalika na pindi iitapo simu hapawezekani kabisa kusubiri mpaka msomaji afike mwisho wa Aayah wala dhikri au Hadiyth iishe. Hivyo, panatokeya kusimamisha au kupokea simu katika Aayah kabla ya jumla (sentensi) haijakamilika; kwani ni vigumu mno kusubiri kwa kuzingatia yafuatayo:

(a) Ikiwa aliyepiga simu mtu anayemdai muda mrefu na aliahidi kuwa leo saa fulani atawasiliana nawe ili mkutane sehemu apate kukulipa deni lako, kwa tamaa na hamu ya kulipwa deni lako, hutoweza kusubiri mpaka Aayah imalizwe!

(b)  Ikiwa aliyepiga simu mathalani ni mmoja kati ya jamaa zako aliyekuwa amebaki na mgonjwa wenu hospitalini au nyumbani na hali yake haikuwa nzuri bali yu hoi taabani kadhalika katika hali kama hii pia hapawezekani kusubiri mpaka msomaji afike mwishoni mwa Aayah au jumla au pia Hadiyth iishe.
Hivyo kutampelekea kusimama au kupokea simu sehemu isiyoridhiwa kishariy’ah mfano Suwratul Anfaal Aayah 1:
يَسْأَلُونَكَ عَنِ الْأَنفَالِ 
“Wanakuuliza kuhusu ngawira…”
Akipokea simu kabla jumla haijaisha: يَسْأَلُونَكَ عَنِ الْأَنف 
Maana inakua:  “Wanakuuliza kuhusu pua”, na si “wanakuuliza kuhusu ngawira” (mali igawiwayo baada ya vita), hili nalo halifai (yaani kujaalia Qur-aan ndiyo mwito wa kukuita ili upokee simu au dhikri au mawaidha au du'aa na kadhalika).  

Bali Qur-aan haikuletwa ila iwe ni mawaidha na kuwaonya na kuwaelekeza watu wazuri na kuwakataza watu mabaya tazama Suwrat Yaasiyn (69–70) haikuwa Qur-aan ila ni ukumbusho na Kitabu kibainishacho kila yanayohitajiwa ili imwonye aliye hai hai na ihakikike kauli (ya kuadhibiwa) juu ya Makafiri. 

Hivyo kuifanya Qur-aan ndio mwito wa wewe kupokelea simu ni jambo baya kabisa mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) ni madharau ya Kitabu Chake na ni kejeli na maneno Yake.

Watu wema walikuwa wakiheshimu mno maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) bali hata ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mfano mmoja tu katika hilo kisa cha Imaam Daarul Hijrah, Imaam Maalik (Rahimahu Allaah) alipokuwa akidarisisha (akifundisha) Hadiyth za bwana Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika kitabu chake “Al-Muwatwaa” katika Msikiti wa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) huko Madiynah, ghafla akang’atwa na nge (mdudu mkali mwenye sumu kali mno – baadhi ya watu wakiumwa na mdudu huyu hupoteza fahamu, wengine hutokwa na povu jingi mdomoni, wengine hubaki na maumivu muda wa masaa 12 na wakati mwengine masaa 24) nge huyo alimng’ata Imaam Maalik (Rahimahu Allaah) mara tatu! Na kila mara Imaam anashtuka kidogo lakini hakatishi Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumaliza akawaambia wanafunzi wake, angalieni hapa chini kuna nini? Wakafungua na kunyanyua tandiko alilokalia tahamaki wanamuona nge. (Imaam Maalik (Rahimahu Allaah) akawaonyesha sehemu alizomuuma mara wanazikuta ni tatu!
Wakasema wanafunzi kwanini  Imaam usikatize Hadiyth mara alipokuuma tu, tukamuua kisha ukaendelea na Hadiyth? Akawajibu Imaam maneno yenye maana: “Haikuwa kwangu ni rahisi kukatisha maneno ya bwana Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa sababu ya nge aliyening’ata!

Ona hiyo heshima waliyokuwa nayo, kisha tazama hali tulizo nazo sisi na maneno ya Allaah!! Tazama hali tulizonazo sisi na Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)!! Kwetu ni miito ya kutujulisha kwa kuna mtu kakupigia simu!! Yaa Allaah ya Kariym, Kwake pekee twashtakia unyonge wetu – tutengeneze Yaa Allaah hali zetu.


8-Kutorekodi maneno ya mwenzio

Adabu ya nane na ya mwisho, ni kutorekodi maneno ya mwenzio vyovyote yatakayokuwa maneno – ya kidini au kidunia ila kwa idhini yake au kwa kumjuilisha kabla –, hakika pamethibiti Hadiyth sahihi kama ilivyokuja katika Sunnan At-Tirmidhiy au Abuu Daawuud na Musnad Ahmad bin Hanbal (Rahimahum Allaah) kutoka kwa Jaabir bin Abdillaah Al-Answaariy (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
“Pindi atakapozungumza mtu na mtu kabla ya kuzungumza akatazama huku na huku basi hiyo ni dalili tosha kuwa hiyo ni amana.”
Imamu Raaghib (Rahimahu Allaah) anasema, siri zipo aina mbili:

(1) Ni ili aisemayo mwana mwana Aadam akataka ifichwe kwa kusema kwake mwishoni mwa mazungumzo: “Hii ni siri baina yangu mimi na wewe” au “ficha siri hii” au “usimwambie mtu haya.”

(2) Siri ijulikanayo bila kuambiwa bali mazingira yanatosha kukufahamisha hii ni siri usiitoe kama kujitahidi mzungumzaji maneno yenu yawe yenu tu – kwa kutoka pembeni au kukunong’oneza au kwa kuangalia huku na huku… na kadhalika.

Na simu inaingia katika hali zote hizi mbili, hivyo kusajili au kurekodi bila idhini yake ni khadaa na makosa, bali kosa kubwa kabisa ni kule kurekodi bila idhini yake na kumjuilisha kisha ukayaeneza yale mliyoongea naye kwa watu wengine, Hilo ni baya mno na ni kubomoa amana.

Allaah Atuhifadhi na yote mabaya Allaahumma Aamiyn.


Mwisho


Nimekusanya Adabu hizi toka sehemu tofauti, lakini kubwa zaidi nimerejea sana katika risala ya Shaykh Bakr bin 'Abdillaah Abuu Zayd (Rahimahu Allaah) aliyoiita “Aadabul-Haatwif.”

0 Comments