6 wauawa katika maandamano ya kupinga sheria tata dhidi ya Waislamu India

Watu sita wameuawa huku wengine kadhaa wakijeruhiwa katika maandamano ya kupinga sheria iliyo dhidi ya Waislamu nchini India, huku taasisi za kimataifa, nchi na shakhsia mbalimbali duniani wakiendelea kukosoa hatua ya kupasishwa sheria hiyo tata.
Maafisa wa serikali ya New Delhi wamesema leo Jumapili kuwa, watu wanne wameuawa kwa kupigwa risasi na askari polisi katika maandamano hayo.
Habari zaidi zinasema kuwa, mtu mmoja ameuawa baada ya duka alikokuwa amelala kuteketezwa kwa moto huku wa sita akiuawa baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana kwenye maandamano hayo. 
Taharuki imetanda nchini India hususan katika majimbo ya kaskazini mwa nchi, huku maandamano ya kupinga sheria hiyo ya kibaguzi iliyopasishwa siku ya Jumatano yakishtadi.
Sheria hiyo inaruhusu kupatiwa uraia wahajiri wa jamii za Wahindu, Mabudha na hata Wakristo wanaotokea nchi za Pakistan, Bangladesh na Afghanistan, huku ikizuia kupewa uraia Waislamu wanaotoka katika nchi hizo.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu wa Japan ameakhirisha safari yake ya India iliyotazamiwa kuanza leo Jumapili. Shinzo Abe alitazamiwa kuwasili leo Jumapili katika mji wa Guwahati jimboni Assam, kaskazini mashariki mwa India, ambapo alitarajiwa kukutana na kufanya mazungumzo na maafisa wa ngazi za juu wa serikali ya New Delhi akiwemo Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Narendra Modi.

Aidha Waziri wa Mambo ya Nje wa Bangladesh, A.K. Abdul Momen amefuta ziara yake ya kuitembelea India, huku maandamano ya kulaani sheria hiyo tata yakienea nchi nzima.
Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imeitaja sheria hiyo kuwa ya kibaguzi. Wakosoaji wamesema kuwa sheria hiyo ni sehemu ya melengo machafu ya chama kikuu cha Bharatiya Janata (BJP) kwa ajili ya kuwaondoa nchini humo wafuasi wa dini ya Kiislamu.

0 Comments