Bakwata wampongeza Rais Wa Tanzania kwa kwasamehe wafungwa 5,000

Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA) limeadhimisha miaka 51 tangu kuanzishwa kwake kwa mafanikio kadhaa, huku likimpongeza Rais John Pombe Magufuli wa nchi hiyo kwa namna anavyowatumikia wanyonge ikiwamo kuwapatia msamaha zaidi ya wafungwa 5,000 hivi karibuni

Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA) limetoa wito kwa wafungwa walioachiliwa, kutumia fursa ya maisha yao kutenda mema na kutumikia nchi yao kama nguvu kazi muhimu katika jamii na wasirejee tena katika vitendo vya uhalifu na uovu.
Akihutubia hapo jana jijjini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA) Nuhu Mruma alisema kuwa, taasisi hiyo inampongeza sana Rais Magufuli kwa kuwasamehe wafungwa hao ambao bado walikuwa hawajamaliza muda wao wa kukaa gerezani.
Katika maadhimisho ya miaka 58 ya uhuru wa Tanganyika yaliyofanyika mkoani Mwanza Disemba 9 mwaka huu, Rais John Pombe Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliandika historia mpya kwa mara ya kwanza tangu nchi ipate uhuru kwa kutangaza msamaha kwa wafungwa 5,533.

Wakati Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA) likimpongeza Rais Magufuli kwa msamaha wake kwa wafungwa, baadhi ya wafungwa walioachiliwa huru hivi karibuni kwa msamaha wa Rais wameripotiwa kujihusisha na vitendo vya uhalifu na hata mauaji. Inaarifiwa kuwa, mtu mmoja ambaye aliachiwa huru kwa msamaha wa Rais Dkt. John hivi karibuni aliwavamia na kuwachoma visu watu 6 huku mmoja wao akifariki dunia hapo hapo. Tukio lilitokea katika eneo la Stendi Kuu ya Mabasi yaendayo mikoani katika Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera. Baada ya mtuhumiwa kutekeleza tukio hilo, wananchi wenye hasira kali walimvamia na kuanza kumshambulia hadi kumuua.

0 Comments