Dalili na magonjwa yanayohusiana na ujauzito

Undani wa mimba mapacha

Mimba au ujauzito mapacha ni hali ya kuwepo zaidi ya mtoto mmoja katika mfuko wa uzazi wa mwanamke mjamzito. Ingawa ujauzito wa namna hii huambatana na changamoto zaidi ya kawaida, kwa upande mwingine imekuwa ni fahari kwa mwanamama kuwa na ujauzito wa namna hii.
Kwa kawaida mimba pacha huwa ni watoto wawili, lakini pia mapacha wanaweza kuwa watatu, wanne, watano au hata sita.

Dalili za mimba mapacha

Ujauzito wa mapacha huambatana na changamoto nyingi kuliko ujauzito wa mtoto mmoja. Kuongezeka kwa baadhi ya changamoto hizi huweza kuwa dalili ya mimba mapacha.
Dalili hizi zinahusisha kupata kichefuchefu na kutapika sana kiasi cha kushindwa kufanya kazi, moyo kuenda mbio, kukosa pumzi, kuvimba miguu, kupata bawasili, tumbo kuwa kubwa kuliko kawaida pamoja na mama kuhisi mtoto kucheza sana kuliko kawaida.

Aina za mapacha

Mimba mapacha zipo za aina kuu mbili ambazo ni pacha wa kufanana na pacha wasiofanana. Pacha wa kufanana, wao hufanana mwili mzima kuanzia jinsia, sura, akili, vipaji na hata namna ya kuongea. Kwa upande wa pacha wasiofanana, hawa huweza kuwa jinsia moja au tofauti na pia huweza kuwa na tofauti kama zile za watoto wa familia moja waliozaliwa katika mimba tofauti.

Pacha wanavyotokea

Kumekuwepo na mkanganyiko wa kwa namna gani pacha hawa hutokea. Kwa mapacha wanaofanana, hawa hutokea ikiwa yai moja la mama litarutubishwa na mbegu moja ya baba kisha kujigawanya na kufanya viini tete viwili vilivyotokana na mbegu moja kutoka kila mzazi. Viini tete hivi hufanana kila kitu, kisha hukua na kutengeneza Watoto wawili. Kwa upande wa mapacha wasiofanana, mayai mawili ya mama hurutubishwa na mbegu mbili tofauti za baba na kutengeneza viini tete viwili ambavyo kila kimoja kinatokana na ya mbegu tofauti kutoka kila mzazi. Kutegemeana na mbegu zilizorutubisha mayai haya, watoto hawa wanaweza kuwa na jinsia tofauti na kutofautiana katika nyanja mbalimbali.

Nani anapata mimba ya pacha?

Kwa upande wa mapacha wanaofanana, mwanamke yeyote anaweza kupata pacha wa namna hii. Hii ni kwa sababu, mpaka sasa haijabainika ni kwa sababu zipi kiinitete kimoja kinaweza kujigawanya na kutengeneza watoto wawili. Kwa upande wa pacha wasiofanana, zipo sababu mbalimbali zinazopelekea mwanamke kupevusha mayai mawili kwa pamoja. (Ijulikane kuwa, kwa kawaida yai moja hupevushwa kila mwezi).
Wanawake wanaoweza kupevusha mayai mawili kirahisi ni wale waliotokea kwenye familia zenye mapacha (upande wa mama tu), wanaotumia madawa yakusisimua uzazi, wenye miaka 35 au zaidi, waliozaa watoto watano au zaidi, wenye asili ya Afrika (weusi) pamoja na baadhi ya vyakula (ikiwemo vya Kinaijeria) huweza kusababisha kupevusha yai zaidi ya moja.

Mapacha wa baba tofauti

Ndugu msomaji, pengine umewahi kusikia kisa cha watoto mapacha wenye baba tofauti. Mapacha wa namna hii hutokea baada ya yai la mama kurutubishwa na mbegu ya kiume na kupevusha yai jengine (kwa kawaida upevushaji husitishwa baada ya urutubishaji) ambalo litarutubishwa na mbegu za mwanaume mwengine. Hivyo, kwa lugha rahisi tunaweza kusema kuwa mimba imetunga juu ya mimba nyingine.

Mapacha walioungana

Mapacha walioungana hutokea ikiwa kiinitete cha mapacha wa kufanana hakitajigawanya kikamilifu. Mapacha wa namna hii ni adimu sana kwani hutokea mara moja kwenye mimba elfu hamsini. Mapacha hawa huweza kuungana viungo mbalimbali vya mwili kama vile vichwa, vifua, tumbo, makalio, migongo na muda mwingine huweza kutokea vichwa viwili kwenye mwili mmoja.

0 Comments