Erdogan: Inasikitisha taasisi za Kiislamu zimefeli kushughulikia matatizo ya Waislamu

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki ameelezea kusikitishwa kwake na udhaifu wa taasisi na jumuiya za Kiislamu ambazo zimeshidnwa kupatia ufumbuzi changamoto na matatizo yanayozikabili nchi za Kiislamu.
Akihutubu katika kikao cha viongozi wa nchi za Kiislamu cha "Kuala Lumpur 2019" huko Malaysia Rais wa Uturuiki amesema kuwa, "Nasisitiza kuwa taasisi hizo zimefeli kwa kuwa hatujapiga hatua yoyote ya maana katika kadhia ya Palestina, tumekosa kustafidi na rasilimali zetu na pia tumeshindwa kuzuia kuporomoka ulimwengu wa Kiislamu kwa misingi ya tofauti za kimadhehebu."
Erdogan ameonekana kuashiria kwa njia isiyo ya moja kwa moja Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ambayo imeshindwa kuchukua hatua madhubuti za kuunga mkono masuala ya Waislamu duniani. Katika hali ambayo Mfalme wa Saudi Arabia amekataa kushiriki mkutano huo wa Malaysia, Jana Jumatano OIC ilisema haiungi mkono hatua ya jamii za Kiislamu kufanya mikutano nje ya makao makuu ya jumuiya hiyo yaliyoko Saudia.
Rais wa Uturuki ameeleza bayana kuwa, mkutano huo wa Kuala Lumpur ungetoa fursa kwa viongozi wa Kiislamu 'kujadili kwa uwazi' masuala yao ya msingi, kuanzia kadhia ya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu, ugaidi, migawanyiko, mizozo ya ndani katika eneo, pamoja na migogoro ya kimadhehebu na kijamii.

Kwingineko katika hotuba yake, Erdogan ametoa mwito wa kupanguliwa muundo wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kulifanya liweze kuwakilisha watu bilioni 1.7 wa ulimwengu wa Kiislamu.
Amesema dunia ni kubwa zaidi ya nchi tano wanachama wa kudumu wa baraza hilo. Nchi hizo ni Marekani, Uingereza, China, Russia na Ufaransa.
Naye Mahathir Mohamad, Waziri Mkuu wa Malaysia ambaye ni mwenyeji wa mkutano huo amesema lengo la kikao hicho ni kujaribu kutathmini ni kwa nini ulimwengu wa Kiislamu upo katika hali ya mgogoro, akisisitiza kuwa, mapendekezo yatakayotolewa kwenye mkutano huo yatakuwa chachu ya kuanzishwa jitihada za kupatiwa ufumbuzi matatizo hayo. 

0 Comments