Sehemu muhimu kabisa ya kipengee cha muswada huo wenye utata ambao umewasilishwa katika Buunge la India ni kutowahusisha Waislamu na uamuzi wa kuwapatia uraia wahajiri. Ni kwa kuzingatia ukweli huu, ndio maana weledi wa mambo wanautathmini muwada huo kwamba, ni hatua ya makusudi iliyo dhidi ya Waislamu
Katika mtazamo jumla inawezekana kusema kuwa, hatua ya sasa serikali ya India imefanyika katika fremu ya siasa za sasa za nchi hiyo zilizo dhidi ya Waislamu na ni njama mpya za chama tawala cha Bharatiya Janata (BJP) za kuwasukuma kando Waislamu wa nchi hiyo.
Wakati huo huo, inapasa kusema kuwa, kwa kuzingatia ukweli huu kwamba, sehemu kubwa ya Waislamu katika baadhi ya majimbo ya India kama Assam ni wahajiri Waislamu waliokimbilia nchini humo wakitokea Bangladesh, kupasishwa muswada kama huo na kuwa sheria kunaweza kuwa na matokeo hatari mno kwa serikali ya New Delhi.
Kanali ya Televisheni ya al-Jazeera inayorusha matangazo yake kwa lugha ya Kiingereza imeripoti kuwa:
Muswada huu unahesabiwa kuwa pigo jipya dhidi ya Waislamu wa India wanaoishi katika jimbo la Assam, kwani katika zoezi la sensa lililopita, walitangazwa kuwa ni watu wasio na uraia wa India. Baadhi ya Waislamu hao walikuwa wakiishi katika katika kambi za wakimbizi kwa muda mrefu. Hii ni katika hali ambayo, akthari yao wamekuwepo nchini India kwa miaka na miaka na wengine wamezaliwa na kusoma nchini humo.
Maandamano makubwa ya wapinzani wa muswada huo wenye utata yaliyofanyika katika mji mkuu New Delhi katika siku ya kwanza ya kuwasilishwa muswada huo katika Bunge la India, ni ishara za mwanzo kabisa za kupinga muswada huo fikra za waliowengi nchini humo.
Endapo wigo wa upinzani huo utapanuka na kufika katika mikoa ya mashariki mwa India ambayo wakazi wake wengi ni wahajiri, serikali ya sasa ya nchi hiyo itakabiliwa na changamoto na mashinikizo zaidi.
Katika mazingira kama haya, licha ya kuwa Bunge la India linadhibitiwa na chama cha Bharatiya Janata (BJP), lakini inatarajiwa kuwa, Wabunge wataamiliana na muswada huo kimantiki na kwa busara kubwa.
Hasa kwa kutilia maanani kwamba, hivi sasa siyo ndani ya India tu, bali hata katika eneo na dunia nzima, walimwengu wamefahamu kuwa, serikali ya India inawalenga na kuwakandimiza Waislamu wa nchi hiyo kwa namna ambayo haijawahi kushuhidiwa, na mwenendo huu katika kipindi cha muda mrefu hautaweza kudhamini maslahi ya serikali ya New Delhi.
0 Comments