Maandamano yashtadi nchini India kufuatia kupitishwa muswada ulio dhidi ya Waislamu

Maandamano ya kupinga muswada wa uraia nchini India na ambao uko dhidi ya Waislamu, yameendelea kupanua wigo wake ambapo baada ya majimbo ya kaskazini mashariki, pia yamesambaa katika maeneo mengine kama vile Uttar Pradesh, Bihar na New Delhi.
Jana Jumamosi waandamanaji wanaopinga muswada huo wenye utata wa kuwapatia uraia wahajiri wasio Waislamu walifanya maandamano katika miji tofauti ya nchi hiyo ukiwemo mji mkuu New Delhi, ambapo sambamba na kuikosoa serikali kuu na bunge la nchi hiyo walipiga nara za kulaani siasa zilizo dhidi ya Waislamu. Aidha siku ya Ijumaa raia wa India walifanya maandamano kama hayo katika maeneo mengine kama vile Assam, Tripura na Arunachal Pradesh. Hadi sasa maandamano hayo yamepelekea watu wasiopungua wanne kuuawa katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa nchi.
Kwa mujibu wa muswada uliowasilishwa bungeni na serikali ya Narendra Modi, Waziri Mkuu wa India, kuanzia sasa wahajiri wasio Waislamu wanaotoka nchi jirani kama vile Afghanistan, Bangladesh na Pakistan, watastahiki kupewa uraia. Muswada huo unaolenga kuwafukuza Waislamu, ulipitishwa hivi karibuni katika mabunge yote mawili ya India. Wakosoaji wamesema kuwa muswada huo ni sehemu ya melengo machafu ya chama kikuu cha Bharatiya Janata (BJP) kwa ajili ya kuwaondoa nchini humo wafuasi wa dini ya Kiislamu. Kuhusiana na suala hilo Asaduddin Owaisi, mmoja wa wabunge wa India amesema kuwa, muswada huo mbali na kukiuka kifungu cha 14 cha katiba ya nchi hiyo, ni mbaya zaidi kuliko sheria za Hitler ambao lengo lake ni kuwanyang'anya uraia Waislamu.

0 Comments