Mahakama ya India yawatoa hatiani wahusika wa mauaji ya Waislamu 1,000 akiwemo Waziri Mkuu Modi

Katika kile kinachotajwa kama hatua nyingine iliyo dhidi ya Waislamu, mahakama ya India imetoa hukumu ya kuwatoa hatiani waliokuwa viongozi wa jimbo la Gujarat, akiwemo waziri mkuu wa sasa wa nchi hiyo Narendra Modi ambao walihusika na mauaji ya Waislamu wapatao elfu moja wa jimbo hilo.
Kwa mujibu wa hukumu hiyo, Modi, ambaye wakati wa mauaji hayo ya halaiki ya Waislamu alikuwa Waziri Kiongozi wa jimbo la Gujarat, ametolewa hatiani yeye pamoja na maafisa wote wa polisi wa jimbo hilo.
Katika hukumu yake hiyo, mahakama ya India imedai kuwa hakuna nyaraka na ushahidi unaoweza kuwatia hatiani viongozi wa wakati huo wa jimbo la Gujarat kwa kuhusika na mauaji ya umati ya Waislamu.
Kamati ya uchunguzi wa faili la mauaji hayo ya Waislamu wa Gujarat imekanusha kutolewa amri yoyote na maafisa rasmi wa serikali ya kuwaua Waislamu, na kueleza kwamba kuuliwa kwa raia hao wa India kulijiri kama tukio tu.
Kwa uamuzi huo wa mahakama ya India, waziri mkuu wa nchi hiyo Narendra Modi ametolewa hatiani katika moja ya kesi nzito zilizokuwa zikimkabili.
Waislamu wapatao elfu moja wa jimbo la Gujarat waliuliwa mwaka 2002 katika shambulio lililofanywa na wahindu wenye misimamo ya kufurutu mpaka.

Itakumbukwa kuwa, mwezi uliopita wa Novemba, katika hukumu ya uonevu na upendeleo wa wazi iliyotolewa kwa manufaa ya Wahindu wenye misimamo ya chuki na kufurutu mpaka, Mahakama ya Juu Kabisa ya India iliamua kuwapatia Wahindu eneo walipoubomoa msikiti wa kihistoria wa Babri ili wajenge hekalu lao la Ram.
Zaidi ya Waislamu 2,000 waliuawa katika machafuko yaliyosababishwa na kitendo hicho cha Wahindu kuubomoa msikiti huo wa kihistoria katika mji wa Ayodhya jimboni Uttar Pradesh kaskazini mwa India mwaka 1992.
Juzi Jumatano pia, Baraza la Seneti la India lilipitisha muswada wa kuwapatia uraia wafuasi wa jamii za wachache wasio Waislamu, wanaohamia nchini humo kutoka mataifa jirani.

0 Comments