Mahathir Mohammad.: Malaysia itawapa hifadhi wakimbizi wa Uyghur kutoka China

Waziri Mkuu wa Malaysia Mahathir Mohammad amesema kuwa nchi yake haitawarejesha makwao Waislamu wa jamii ya Uyghur kutoka China iwapo wataomba hifadhi nchini humo.
Mahathir Muhammad amesema hayo katika Bunge la Malaysia akijibu maswali ya kambi ya upinzani kuhusiana na dhulma na ukandamizaji wa serikali ya China dhidi ya Waislamu walio wachache wa jamii ya Uyghur.
Waziri Mkuu wa Malaysia amesema kuwa, nchi yake inaheshimu msingi wa kutoingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine lakini jamii ya kimataifa inapaswa kukiri kwamba, Waislamu dunia kwa ujumla wakiwemo wa jamii ya Uyghur huko China wanasumbuliwa na mashinikizo na ukandamizaji na kwamba Waislamu hao wa China wana haki ya kuhofia usalama wa maisha yao.
Mahathir Mohammad amesema kuwa, iwapo Waislamu wa jamii ya Uyghur wataomba hifadhi na ukimbizi,  Malaysia haitawarejesha nchini kwao hata kama Beijing itaomba warejeshwe nchini humo.  
Mwezi Agosti mwaka jana Kamati ya Sheria ya Umoja wa Mataifa ilisema kuwa, China inawashikilia karibu Waislamu milioni moja wa jamii ya Uyghur katika kambi za siri.
Mwezi huo huo pia vyombo vya habari vilimnukuu  Gay McDougal ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Kupambana na Ubaguzi ya Umoja wa Mataifa akiripoti kuwa, Waislamu milioni moja wa Uyghur katika jimbo la Xinjiang nchini China wanashikiliwa katika kambi zilizoko maeneo ya mbali ambako wanatwishwa mitazamo makhsusi ya kisiasa na kulazimishwa kuacha dini yao.
Ripoti rasmi zinasema, kuna Waislamu milioni 30 nchini China na kwamba milioni 23 miongoni mwao wanatoka jamii ya Uyghur. Hata hivyo ripoti zisizo rasmi zinasisitiza kuwa, idadi ya Waislamu nchini humo inafikia watu milioni 100 yaani karibu asilimia 9.5 ya jamii yote ya watu wa China.

0 Comments