Majimbo Tofauti nchini India yakataa kutekeleza sheria mpya ya uraia

Mawaziri viongozi wa majimbo tofauti nchini India wamekataa kutekeleza sheria mpya ya uraia.
Vyombo vya habari nchini India vimetangaza kwamba V. Narayanasamy, Waziri Kiongozi wa jimbo la Puducherry sambamba na kukosoa upasishwaji wa muswada mpya wa uraia katika bunge la seneti nchini humo, amesema kuwa sheria hiyo inawabagua Waislamu na kamwe hatoitekeleza. Akiashiria uamuzi hatari wa serikali na ulio dhidi ya jamii za dini za wachache nchini humo V. Narayanasamy, amesema kuwa kwa mujibu wa katiba, jamii zote za walio wachache ni lazima ziwe na haki sawa na raia wengine wa nchi hiyo, lakini sasa serikali ya New Delhi inatekeleza sheria ya ubaguzi wa kidini.

Mjumbe huyo wa ngazi ya juu wa chama cha Kongresi nchini India amesisitiza kwamba majimbo yote ambayo chama hicho kina nguvu, hakutotekelezwa sheria hiyo mpya ya uraia. Kwa upande wake Mamata Banerjee, Waziri Kiongozi wa jimbo la Bengal Magharibi, sambamba na kupinga amri ya serikali ya India ya kujenga kambi moja kubwa maalumu kwa ajili ya kuwashikilia wahusika wa maandamano ya hivi karibuni ya kupinga sheria ya ubaguzi wa kidini, amesema kuwa kamwe hatoruhusu kujengwa kambi hiyo. Tangu wiki mbili zilizopita India imekuwa ikishuhudia maandamano makubwa ya kupinga sheria mpya ya uraia ambapo kwa akali watu 25 wameuawa na maelfu ya wengine kutiwa mbaroni. 

0 Comments