Masuala Kumi Yanayoeleweka Vibaya Katika Uislam - 9


Uislamu ni dini ya kibaguzi, ni dini hasa ya Waafrika kwasababu:
·                     Nation Of Islam ‘Taifa la Kiislamu’[1] linafuata daraja kuu ya watu weusi
·                     Nation Of Islam ‘Taifa la Kiislamu’ linatambua Mungu kuwa ni mtu mweusi

Moja wapo ya masuala yanayoeleweka vibaya kuhusu Uislamu kwa karne ya ishirini ni kule kuita ‘Taifa la Kiislamu’ kuwa ni jamii ya Waislamu, au kwa ufafanuzi zaidi: jamii ambayo inanyenyekea kwa Allaah kwa kufuata Qur-aan na Sunnah. ‘Taifa la Kiislamu’ ni njia ya maisha iliyofanywa na watu iliyoazima aina fulani za Uislamu na kuzichanganya pamoja na mambo ya uzushi yaliyo mengi na uongo ili kufikia uamuzi wao wa leo.
Inatosha kueleza kwamba Taifa la Kiislamu limepotoka kwa njia mbili. Kwanza, wanakataa msingi wa Uislamu kwa kufanyiza simulizi ambayo Muumba anachorwa kwa mfumo wa mtu mweusi. Kwa mujibu wa machapisho yao ya kwenye mtandao, tunaona kwamba ‘Taifa la Kiislamu’ linaamini kwenye:

…Mungu mmoja (Allaah) na kwamba Allaah (Mungu) alijitokeza kwa njia ya Mwanaadamu kupitia kwa Mkuu W. Fard Muhammad, Julai, 1930, huyu ni Masihi wa Wakritso na ‘Mahdi’ wa Waislamu aliyekuwa akisubiriwa kwa muda mrefu…

Hata hivyo, Muumba Anaeleza ndani ya Qur-aan (tafsiri):
{{Macho hayamfikii (kumwona), bali Yeye Anayafikia macho (kuyaona na kuwaona hao wenye macho). Naye ni Mwenye kujua yaliyofichikana na yaliyo dhahiri.}} [6:103]

Pia ‘Taifa la Kiislamu’ linadai kwamba watu weupe ni ‘mashetani’, na kwamba watu weusi kwa ujumla ni bora kuliko makabila mengine. Hata hivyo, Kutokana na Sunnah, hususan ndani ya khutba ya kuaga ya Mtume wa Allaah, tunaona Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:
Watu wote wanatokana na Adam na Hawa, Muarabu hana ubora juu ya asiye kuwa Muarabu wala asiye kuwa Muarabu hana ubora juu ya Muarabu, pia mweupe hana ubora juu ya mweusi wala mweusi hana ubora juu ya mweupe – isipokuwa kwa Mcha Mungu na mwenye matendo mazuri.

Kuna dhana nyingi nyengine ambazo ‘Taifa la Kiislamu’ linakamatana nazo zinazolipeleka nje ya Uislamu. Ni ajabu kuona kwamba mnamo miaka ya kati ya 1970, walio wengi walitambua makosa yake na kubadilika kuingia kwenye Uislamu wa kweli. Lakini kuna kipande cha kikundi, ambacho bado kipo hai.

Itaendelea In Shaa Allaah...
 
[1] Maneno ya ‘Taifa la Kiislamu’ yaliyotumika hapa sio kwa Taifa halisi linalofuata Uislamu kwa misingi ya Qur-aan na Sunnah. Isipokuwa, ‘Taifa la Kiislamu’ lililokusudiwa hapa ni Jumuiya ya Waislamu weusi wanaoishi Marekani wanojulikana kama Nation Of Islam lilikokuwa likiongozwa na Elijah Muhammed, ni watu wasioelewa misingi sahihi ya Uislamu na Wanachuoni wamesema hao si Waislamu.[Mfasiri]

0 Comments