Mesut Ozil afutwa kwenye mchezo wa video China baada ya kuwaita waislamu wa Uighur Mashujaa

Kiungo wa Arsenal Mesut Ozil ameondoshwa kwenye mchezo wa video wa Pro Evolution Soccer (PES) 2020 toleo la Uchina baada ya kuikosoa nchi hiyo kwa kuwatesa jamii ya Waislamu ya Uighur.

Ozil, 31, ambaye ni Muislamu, amewaita Wauighur (Wachina wa asili ya Kiislamu) ‘mashujaa wanaokabiliana na mateso’.
Pia ameukosoa utawala wa Uchina na ukimya wa Waislamu katika kuwatetea wenzao nchini humo.
Kampuni ya NetEase, ambayo inatoa video za PES nchini China, imesema kiungo huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Ujerumani ameondolewa kwenye matoleo matatu yaliyopo nchini humo.
Arsenal imesema kuwa klabu hiyo si ya kisiasa na wizara ya mambo ya nje ya Uchina imedai kuwa mchezaji huyo mwenye asili ya Kituruki amedanganyika na habari za uongo za mtandaoni.
Makundi ya haki za binaamu yanadai kuwa takribani watu milioni moja – wengi wao kutoka jamii ya Waislamu ya Uighur – wanashikiliwa bila ya kufunguliwa mashtaka katika magereza yenye ulinzi mkali.
Uchina imekuwa ikikanusha kuwa inawanyanyasa Waislamu wa Uighur na kudai kuwa watu hao wanapatiwa mafunzo katika vituo vya ufundi stadi ili kukabiliana na ugaidi.

0 Comments