Msimamo wa Waziri Mkuu wa Malaysia kuhusu Waislamu wa Uyghur wa China

Waziri Mkuu wa Malaysia amesisitiza kuwa, nchi yake haitawarejesha makwao Waislamu wa jamii ya Uyghur kutoka China iwapo wataomba hifadhi nchini humo.
Mahathir Muhammad amesema hyo katika Bunge la Malaysia akijibu maswali ya kambi ya upinzani kuhusiana na dhulma na ukandamizaji wa serikali ya China dhidi ya Waislamu walio wachache wa jamii ya Uyghur kwenye eneo lenye utawala wa ndani la Xinjiang la kaskazini magharibi mwa China. Amesema: "Iwapo Waislamu wa Uyghur watakuja Malaysia na kuomba hifadhi ya ukimbizi, bila ya shaka hatutojali upinzani wa serikali ya China na hatutowarudisha makwao Waislamu hao."
Waziri Mkuu wa Malaysia amesema kuwa, nchi yake inaheshimu msingi wa kutoingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine lakini jamii ya kimataifa inapaswa kukiri kwamba, Waislamu dunia nzima kwa ujumla wakiwemo wa jamii ya Uyghur huko China wanasumbuliwa na mashinikizo na ukandamizaji na kwamba Waislamu hao wa China wana haki ya kuhofia usalama wa maisha yao.

Msimamo huo wa Waziri Mkuu wa Malaysia unatokana na misimamo aliyokuja nayo tangu aliporejea madarakani mwezi Mei 2018 huko Malaysia. Msimamo wa Mahathir Mohamad wa kuwaunga mkono Waislamu wa Uyghur unaonesha kuwa, hashughulishwi na misimamo ya kisiasa ya Malaysia ambayo ni moja ya nchi kubwa za Kiislamu katika kulinda uhusiano wake na China, bali anachojali zaidi na haki za binadamu na hicho ndicho kigezo kikuu cha msimamo wake huo. 
Msimamo wa Waziri Mkuu wa Malaysia wa kuwaunga mkono Waislamu wa maeneo tofauti duniani hauishii tu kwa Waislamu wa Yughur huko nchini China. Kampeni mpya ya viongozi wa hivi sasa wa India ya kuwakandamiza Waislamu nchini humo ikiwa ni pamoja na hatua yao ya kupasisha muswada wa kuwabana na kutowapa uraia Waislamu wa nchi hiyo, ni miongoni mwa masuala yaliyolalamikiwa sana na viongozi wa Malaysia wakiongozwa na Waziri Mkuu, Mahathir Mohamad. 
Mwezi Septemba mwaka huu, Mahathir Mohamad alisema kwenye hotuba yake katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwamba siasa za serikali ya chama cha BJP cha India kuhusu eneo la Kashmir haukubaliki kabisa. Aliilaumu serikali ya Waziri Mkuu Narendra Modi wa India kutokana na kutumia nguvu kubwa za kijeshi kukandamiza Waislamu wa Kashmir.

Msimamo huo wa Mahathir Mohamad uliikasirisha serikali ya India kiasi kwamba wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo ilimtaka alinde uhusiano mzuri wa Malaysia na India na asiingilie masuala ya Kashmir. Hata hivyo msimamo huo wa India haukumfanya Mahathir Muhammad kubadilisha msimamo wake wa kuwatetea Waislamu wa India. Waziri Mkuu huyo wa Malaysia aliilaumu vikali serikali ya chama cha BJP cha Narendra Modi huko India kwa kupasisha muswada wa kutowapa uraia Waislamu nchini India. Serikali ya New Delhi nayo ilikasirishwa na msimamo huo wa Malaysia na kumwita mjumbe maalumu wa nchi hiyo huko India kwenye ofisi za wizara ya mambo ya nje kumkabidhi malalamiko yake hayo.
Misimamo hiyo ya wazi ya Waziri Mkuu wa Malaysia yanaonesha wazi kuwa Mahathir Mohamad hayuko tayari kunyamazia kimya dhulma wanayofanyiwa Waislamu hata kama baadhi ya nchi zitakasirishwa na msimamo wake huo.
Ni wazi kuwa, msimamo huo wa Waziri Mkuu wa Malaysia hauwezi kuifurahisha hata kidogo China ambayo mara kwa mara imekuwa ikipinga taarifa kwamba inawakandamiza Waislamu nchini humo. Hata hivyo, licha ya China kuchukua msimamo huo, lakini idadi ya Waislamu wa Uyghur wanaoikimbia nchi hiyo na kuomba hifadhi nchi nyingine inazidi kuongezeka. Inaonekana ni kwa sababu hiyo ndio maana mwezi Julai mwaka huu wa 2019, nchi 22 wanachama wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa zilitoa tamko la pamoja zikiitaka China iache kuwatia nguvu kwa umati Waislamu wa Uyghur. 

0 Comments