Pakistan yaitaka OIC iwalinde Waislamu wa India

Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan ameitaka Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kuwatetea na kuwahami Waislamu wa India.
Shah Mehmood Qureshi amewaambia waandishi habari huko Multan katika jimbo la Punjab kwamba: Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu inalazimika kuwakusanya pamoja mawaziri wa mashauri ya kigeni wa nchi za Kiislamu kwa shabaha ya kutetea haki za Waislamu nchini India kupitia njia ya kupinga sheria mpya ya uraia nchini humo. 
Itakumbukwa kuwa tarehe 24 mwezi huu wa Disemba Kamisheni Huru ya Kudumu ya Haki za Binadamu ya OIC ilitoa taarifa ikilaani ukatili na mauaji yaliyofanyika nchini India katika maandamo yanayopinga sheria mpya ya uraia. Kamisheni hiyo iliitaka jamii ya kimataifa na Umoja wa Mataifa kuishinikiza serikali ya New Delhi ili ifute vipengee vinavyowabagua Waislamu katika sheria mpya ya uraia na kuheshimu vigezo vya kimataifa wakati wa kukabiliana na waandamanaji. 

Ombi la Pakistan la kutaka kufanyike mkutano wa dharura wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Kiislamu ili kuchukua msimamo mmoja wa kutetea haki za Waislamu wa India limetolewa katika fremu ya stratijia inayofuatwa na serikali ya Islamabad katika saisa zake za nje. Baada ya India kufuta mamlaka ya utawala wa ndani wa eneo la Kashmir na kulitwaa kikamilifu eneo hilo mwezi Agosti mwaka huu, Pakistan ilizidisha mashauriano na nchi mbalimbali kwa shabaha ya kuiwekea mashinikizo India na kusitisha siasa zake za kuwakandamiza Waislamu. 

Lengo la Paksitan katika hatua hii ya kuliweka faili la Kashmir katika meza ya kimataifa na kukabiliana na sera za New Delhi dhidi ya Waislamu hususan sheria mpya ya uraia inayowabagua wafuasi wa dini hiyo ni kuanzisha muungano dhidi ya India na kuilazimisha itupilie mbali ubaguzi mkubwa wa kidini unaofanyika nchini humo ambao umezidisha mbinyo na mashinikizo ya kisiasa na kijamii kwa Waislamu wa nchi hiyo. Hasa kwa kutilia maanani kwamba, India imeamua kukabiliana na maandamano ya amani ya Waislamu wanaopinga sheria mpya ya uraia kwa kutumia ngumi ya chuma na ukatili, suala lililopelekea kuuliwa makumi ya watu waliopigwa risasi moja kwa moja na askari usalama wa nchi hiyo. 

Katika mazingira kama hayo serikali ya Pakistan ambayo ina wasiwasi wa kushadidi zaidi ukatili, mauaji na ukandamizaji wa serikali ya India dhidi ya Waislamu, imetoa wito wa kuitishwa kikao cha mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Kiislamu ili kuchunguza ubaguzi na ukandamizaji wa India na kuchukua msimamo wa pamoja wa kukabiliana na hatua hizo kwa shabaha ya kukomesha sera za kibaguzi za serikali ya New Delhi.


0 Comments