Palestina yataka walowezi wa Kizayuni watambuliwe rasmi kuwa ni magaidi

Wizara ya Mambo ya Nje ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina imetoa wito wa kuwekwa jina la walowezi wa Kizayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina katika orodha ya magaidi.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imelaani hatua za kigaidi za utawala wa Kizayuni wa Israel na kuitaka jamii ya kimataifa kuliweka jina la walowezi wa Kizayuni katika orodha ya magaidi kutokana na jinai zinazofanywa mara kwa mara na walowezi hao. 
Taarifa ya wizara hiyo pia imesema kuwa, ripoti za hivi karibuni na matamshi ya maafisa usalama wa Israel vinaonesha kuwa, kuna ongezeko kubwa la mashambulizi na jinai zinazofanywa na walowezi wa Kiyahudi dhidi ya raia wa Palestina. Imeongeza kuwa kiwango cha hasara zilizosababishwa na mashambulizi hayo kimeongezeka mara dufu.

Katika miezi ya karibuni walowezi wa Kizayuni wamezidisha mashambulizi dhidi ya raia wa Palestina, kuvamizi mali na milki zao na kuuvunjia heshima Msikiti wa al Aqsa. 
Harakati za mapambano ya ukombozi wa Palestina zikiwemo Hamas na Jihad Islami zimetahadharisha kuhusu mashambulizi hayo na kutangaza kwamba, Msikiti wa al Aqsa ni mstari mwekundu ambao haupaswi kuvukwa.

0 Comments