Polisi India yatishia kuwahamisha raia Waislamu wa nchi hiyo na kuwapeleka Pakistan

Polisi ya India imetishia kuwafukuza raia Waislamu wa nchi hiyo katika muendelezo wa uchukuaji hatua za chuki dhidi ya Waislamu hao.
Polisi ya mji wa Meerut katika jimbo la Uttar Pradesh imetishia kuwa, ikiwa Waislamu wataendelea kuandamana kupinga sheria mpya ya uraia, watapoteza haki ya kuishi nchini India na kuhamishiwa Pakistan.
Kauli hiyo ya polisi ya mji wa Meerut imekabiliwa na majibu ya wanasiasa mbali mbali wa India, akiwemo Priyanka Gandhi, kiongozi mwandamizi, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa chama kikuu cha upinzani cha Kongresi ya Taifa ya India (INC), ambaye amesisitiza kuwa, kwa mujibu wa katiba ya India, hakuna kiongozi yeyote mwenye haki ya kuwavunjia heshima raia na kuwataka waihame nchi yao.

Katika kipindi cha siku chache zilizopita, maeneo mbali mbali ya India ukiwemo mji mkuu New Delhi imekuwa ikishuhudia maandamano ya makumi ya maelfu ya watu wanaopinga kupitishwa mswada wa sheria mpya ya uraia.
Maandamano hayo yamekabiliwa na mkono wa chuma wa polisi na askari wa usalama, ambapo hadi sasa waandamanaji wapatao 30 wameuawa na mamia ya wengine wamejeruhiwa.
Hivi karibuni, Baraza la Seneti la India lilipitisha mswada wa sheria mpya ya uraia ambayo inawapa haki ya uraia wahajiri wasio Waislamu wanaolazimika kuhama nchi jirani za Bangladesh, Pakistan na Afghanistan na kuhamia India; lakini haki hiyo haitawahusu wahajiri kutoka nchi hizo ambao watakuwa ni Waislamu.

0 Comments