Sheikh Kundecha atia neno hukumu umri wa ndoa

“Mahakama yetu imetoa hukumu katika matokeo ya uhusiano lakini haisemi ni kwa namna gani tatizo litadhibitwa. Ni kichekesho kwa anayehangaika kunyoosha kivuli na kuacha mti ukipinda,”

Hayo ni maneno ya Amir wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Mussa Kundecha aliyoongea kwenye kongamano la Misk ya Roho lililofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam, Jumapili iliyopita.

Sheikh Kundecha alisema: “Upo uelewa unaotakiwa kufanyiwa marekebisho ya kutosha katika suala la umri wa ndoa kwa sababu hapa Tanzania kuna kitu kinaitwa, ‘Ndoa za utotoni na mimba za utotoni’ dhana ambayo si sahihi.”

Sheikh Kundecha aliiambia hadhira iliyokusanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee kuwa hakuna mtoto awezaye kushika ujauzito isipokuwa baada ya kuvunja ungo au kubalehe.

“Hakuna mtoto anayeshika mimba au kumpa mimba mtu hata kama atakunywa Alkasusu pipa zima, lakini mtoto mdogo akifikia rika lake (umri wa utu uzima) anaweza kupata mimba, na kama ni mvulana anaweza kumpa mimba msichana,” alisema.

Aidha, Amir huyo wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu hapa nchini alizitupia lawama mamlaka husika kwa kushindwa kudhibiti vitendo vya zinaa.

“Ikiwa hawawezi kuzuia watoto wadogo kupata ujauzito na wanawazuia kuolewa, maana yake wanawapa majukumu wazazi wa watoto hawa waendelee kubeba mzigo wa kuwalea wao na watoto watakaowazaa kwa sababu sheria haitaki kuwatambua wale waliowapa ujauzito.”

Alisema mtoto ni matunda ya uhusiano kati ya mwanamke na mwanaume, hivyo mamlaka zinaposhindwa kudhibiti uhusiano huo, zisitoe hukumu katika matokeo ya uhusiano huo.

Sheikh Kundecha alihoji: “Sheria hutengeneza ufumbuzi wa matatizo. Mbona hawa wanataka kutengeneza matatizo katika jamii badala ya kuisaidia?”

0 Comments