Sisitizo la Waziri Mkuu wa Malaysia la kukabiliana na chuki dhidi ya Uislamu

Waziri Mkuu wa Malaysia amesisitiza katika Mkutano wa Viongozi wa nchi za Kiislamu wa "Kuala Lumpur 2019" juu ya udharura wa kukabiliana na kampeni za chuki dhidi ya Uislamu
Mahathir Muhammad amesema katika mkutano huo unaohudhuriwa na baadhii ya viongozi wa nchi za Kiislamu kwamba, ana matumaini mkutano huo utakuwa na matunda na matokeo mazuri kwa Waislamu na kufungua mlango wa kufanyika mambo ya kimsingi kwa minajili ya kuboresha mambo yao. Waziri Mkuu wa Malaysia ameongeza kuwa: Kuna haja ya kutafuta njia ya kupunguza mapungufu na utegemezi wetu kwa Magharibi, ili kwa njia hiyo tuweze kujilinda  dhidi ya maadui wa Uislamu.
Mkutano wa Viongozi wa nchi za Kiislamu wa "Kuala Lumpur 2019" ulianza asubuhi ya leo Alkhamisi katika ukumbi wa makongamano ya kimataifa katika mji mkuu wa Malaysia Kuala Lumpur kwa kuhudhuriwa na Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, viongozi wa nchi za Malaysia, Uturuki, Qatar na mamia ya shakhsia na watu wenye vipawa kutoka katika nchi mbalimbali za Kiislamu.

Hotuba ya Waziri Mkuu wa Malaysia kuhusiana na ulazima wa kukabiliana na propaganda za chuki dhidi ya Uislamu katika Mkutano wa Kuala Lumpur inabainisha dharura moja kubwa kwa ajili ya nchi za Kiislamu. Madola ya Magharibi kinara wao akiwa Marekani katika kipindi cha muongo mmoja uliopita na katika fremu ya siasa zao yametanguliza mbele kampeni za kueneza propaganda chafu na chuki dhidi ya Uislamu.
Mipango ya madola hayo ni kuyashinikiza mataifa ya Kiislamu, hatua ambayo imepelekea kuibuka mtazamo hasi dhidi ya Waislamu katika maeneo mbalimbali ya dunia.
Madola ya Magharibi yakitumia kisingizio cha kupambana na ugaidi, yaliweka sheria katika uwanja huo ambazo kivitendo ni hujuma za moja kwa moja dhidi ya Waislamu.
Madola hayo ambayo kimsingi yenyewe ndio waasisi na wazalishaji wa makundi ya kigaidi likiwemo la Daesh katika eneo la Asia Magharibi, yamekuwa yakivinasibisha na wafuasi wa dini ya Kiislamu vitendo vya mauaji ya kikatili ya kundi hili la kigaidi; na kupitia hilo yamekuwa yakisukuma mbele gurudunmu la siasa zao za chuki dhidi ya Uislamu na kuuonyesha Uislamu kwamba, ni dini ya utumiaji mabavu.

Massoud Shajareh, Mkuu wa Tume ya Kiislamu ya Haki za Binadamu (IHRC) yenye makao yake katika mji mkuu wa Uingereza, London anasema kuwa: Chuki dhidi ya Uislamu ni uhakika wenye kutia wasiwasi katika jamii ya Uingereza; na vyombo vya habari na wanasiasa ndio sababu ya kuongezeka chuki dhidi ya Uislamu. Wamelifanya hilo kama mtaji wao na wanazifungamanisha na Uislamu na Waislamu sheria za kupambana na ugaidi, ili kwa njia hiyo waweze kuhalalisha propaganda zao chafu na chuki dhidi ya Uislamu.
Matamashi ya Waziri Mkuuu wa Malaysia kuhusiana na udharura wa kukabiliana na chuki dhidi ya Uislamu yanatolewa katika hali ambayo, moja ya malengo muhimu ya "Mkutano wa Kuala Lumpur 2019" ni kuwa na fikra na mtazamo mmoja na kubadilishana mawazo kuhusiana na mikakati ya kukabiliana na siasa za chuki dhidi ya Uislamu za Magharibi ambazo zinalenga kueneza mtazamo mbaya na chuki dhidi ya Waislamu.

Mahathir Muhammad ambaye anajulikana kama "Mhandisi wa Ustawi wa Malaysia" ana hamu na shauku kubwa ya kutumiwa uwezo wa kiuchumi uliopo baina ya mataifa ya Kiislamu kwa ajili ya kusaidiana na kubadilishana uzoefu na uwezo mataifa ya Kiislamu kwa minajili ya kupunguza utegemezi kwa mataifa ya Magharibi.
Inaonekana kuwa, hatua ya kwanza ya kukabiliana na chuki dhidi ya Uislamu zinazoenezwa na madola ya Magharibi ni kuusafisha ulimwengu wa Kiislamu na uwepo wa baadhi watu ambao wamekuwa wakiutumia ugaidi kama wenzo wa vita vyao vya niaba katika eneo, ambapo hatua hii sambamba na kuchochea moto wa mizozo na mivutano katika nchi za Kiislamu, imekuwa ikitumiwa vibaya na maadui na hivyo kuufanya Uislamu utazamwe kwa jicho baya na hata watu kuuogopa.

0 Comments